Vilio
vya furaha kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki, vimetawala katika
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam
jana, baada ya kuwasili kwa madereva 10 wa Tanzania waliotekwa na
kunusurika nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Madereva
hao waliwasili katika uwanja huo saa 9 alasiri, wakitoka Kigali, Rwanda
kwa ndege ya Shirika la Ndege la Rwanda na kukutana na familia zao kwa
mara ya kwanza baada ya kuokolewa.
Wakiwa
uwanja wa ndege, walizungumza na waandishi wa habari na kueleza namna
walivyotekwa na waasi waliovalia sare za jeshi zisizofanana na
walivyosafirishwa zaidi ya kilometa 50 porini usiku na mchana,
wakitembea kwa magoti na kupoteza tumaini la kupona huku baadhi
wakifanikiwa kutoroka na wengine kuokolewa.
Kabla
ya kuwasili kwa madereva hao, ndugu hao walikusanyika uwanjani hapo
wakiwa na shauku ya kukutana na madereva hao ambao Septemba 14, mwaka
huu, walikumbwa na kadhia ya kutekwa na kundi la wanamgambo huku magari
waliyokuwa nayo yakichomwa moto na hatma yao kutojulikana.
Hata
hivyo, kutokana na juhudi za Serikali ya DRC na Tanzania, madereva hao
walifanikiwa kuokolewa na kupatiwa matibabu ambapo jana walirejea nchini
rasmi.
Baada
ya madereva hao kumaliza kuzungumza na waandishi wa habari, walitoka
nje kwenda kuonana na ndugu zao waliokuwa wamekusanywa pembeni, lakini
walipowaona tu walishindwa kujizuia na kuwakimbilia madereva hao ambao
nao waliwakimbilia huku wakilia na kutamka maneno ya kumshukuru Mungu
kwa kuonana tena.
Baadhi
ya familia ziliambatana na watoto wa madereva hao, ambao katika hali ya
kutia simanzi baada ya kuwaona wazazi wao, waliangua kilio kwa sauti
huku wakiwaita baba zao na kuwakumbatia kwa furaha.
Madereva
waliookolewa kutoka Tanzania na waliowasili jana ni Kumbuka Selemani,
Hussein Mohammed, Bakari Nassoro, Issa Omary, Amdani Zarafi, Adam James,
Mbwana Said, Ali Juma, Athuman Fadhil na Amis Mshana.
Familia za madereva zazungumza
Mke
wa dereva Ali Juma, Jamila Ali, alisema anamshukuru Mungu kwa kuonana
tena na mumewe, jambo ambalo hakulitarajia kwani baada ya kupewa taarifa
za kutekwa kwake, walikata tamaa ya kumuona tena. Pia alizishukuru
Serikali zote mbili kwa juhudi za haraka, walizochukua baada ya kupata
taarifa ya kutekwa kwa mumewe na wenzake.
“Mimi
nilipata taarifa kutoka kwa mwanangu mkubwa aliyenisihi nimpigie simu
baba yake, lakini baada ya kupiga simu ilikuwa ikipokewa na kuwekwa
pembeni bila mtu kuongea, lakini nilisikia watu wakiongea kwa lugha ya
kifaransa mpaka nikamaliza vocha yangu ya Sh 10,000,” alisema.
Alisema
wakati akipiga simu hiyo, alikuwa hafahamu chochote kuhusu kutekwa kwa
mumewe, ila baadaye alisikia kwenye taarifa ya habari, ndipo alipotambua
kuwa na mumewe yupo miongoni mwa madereva waliotekwa kutokana na
kampuni iliyotajwa ambao ni Simba Logistics.
Mariam
Ayoub ambaye ni mke wa Mbwana Said, alisema anamshukuru Mungu baada ya
mumewe kurejea salama na kwamba siku ya jana ni ya furaha kwake na
familia yake.
Alisema
tangu apate taarifa za kutekwa kwa mumewe kupitia taarifa ya habari
hakuweza kula, wala kulala usingizi huku akiwa na mtoto mdogo wa mwaka
mmoja na nusu.
“Leo nina furaha kubwa wala siwezi kuelezea zaidi,” alisema huku akilia.
Naye
dada wa Bakari Nassoro, Halima Juma ambaye alikuwa akielezea furaha ya
kuonana na ndugu huku akilia, alisema familia yake ilishakata tamaa ya
kumuona tena ndugu yao huyo kutokana na simulizi za kutisha, walizokuwa
wakihadithiwa kuhusu waasi wa DRC.
Baada
ya kuonana na familia zao, madereva hao walipiga picha ya kumbukumbu na
kisha kuondoka uwanjani hapo kila dereva na familia yake.
Madereva wasimulia
Awali
wakati akisimulia kama sinema juu ya kilichowapata wakati wakitekwa,
Kumbuka Selemani, alisema siku hiyo ya Septemba 14, mwaka huu katika
eneo la Namoya Jimbo la Kivu Kusini mwa nchi ya DRC, madereva hao
walitoka kushusha mzigo wa saruji kilometa 12 kutoka eneo walilotekewa.
Alisema
mara baada ya kushusha mzigo huo wakati wakirejea, walikuwa
wakiongozana na magari mengine ya kampuni hiyo ya Simba Logistics yeye
akiwa dereva wa gari namba nane.
Alisema
wakati akikaribia eneo la Kivu, ghafla alisimamishwa na mtu aliyekuwa
amebeba silaha nzito huku amevaa mavazi ya jeshi yasiyoeleweka, kwa
maana ya kuchanganywa na kumtaka ashuke kwenye gari hilo na amkabidhi
kila kitu, ikiwemo hati yake ya kusafiria na kadi ya gari.
“Wakati
nimeshashuka niko chini namkabidhi vitu vyangu, mara lilitokea gari la
tisa ambalo baada ya kumuona yule mwanajeshi, lilisimama na kuanza
kugeuza kwa maana ya kukimbia. Ndipo yule askari akaachana na mimi
akaanza kulirushia risasi lile gari lililokuwa linaendelea kugeuza,” alisimulia.
Alisema
risasi zile kwa bahati zilipiga kwenye kioo cha pembeni cha lori
lingine la 10 lililokuwa linalokuja ambalo nalo baada ya kuona hali ile
liligeuza. “Mimi nilipoona ameelekeza mawazo yake kwenye yale magari nikapata upenyo na kukimbilia porini.”
Alisema
aliingia msituni na kuanza kutembea umbali mrefu akitafuta kujiokoa
hadi alipoona kikosi kingine cha polisi ambacho alilazimika kukichunguza
kwanza ili kujua kama ni wale watekaji au askari halali wa nchi hiyo.
Alisema
alibaini kuwa ni askari halali kutokana na mavazi yao kuwa ya kawaida
ya kipolisi bila kuchanganywa ndipo alipojitokeza na kujisalimisha kwa
kunyoosha mikono juu. Askari wale walimchukua na kumhoji na kisha
kumpatia huduma za kawaida ikiwemo chakula.
“Wakati
najiandaa kupanda pikipiki kwenda kula nikashangaa namuona na mwenzangu
(Mshana) ambaye naye alitoroka nikaunganishwa naye,” alisema.
Kwa
upande wake Mshana, alisema naye alisimamishwa na kuamriwa ashuke
kwenye gari na kukabidhi kila kitu ikiwemo hati yake ya kusafiria na
simu. Aliunganishwa na wenzake aliowakuta tayari wametekwa na kuongozwa
kuelekea porini huku wakiwa wamefungwa mikono.
Alisema
katika msafara huo, mmoja wa askari alitangulia mbele na wengine
walifuatia nyuma na kuongozwa kwenye pori zito ambalo wakati mwingine
walilazimika kutembea kwa magoti kwani haikuwezekana kutembea huku
umesimama.
“Tulipotembea
kama kilometa 13 ikabidi nimwambie mwenzangu (Athuman Fadhil) kwamba
tutafute njia ya kujiokoa. Hata hivyo alinijibu kwamba kuwa yeye hawezi
kwa kuwa amevaa nguo inayomtambulisha zaidi endapo akitoroka itajulikana
na wenzetu watapata shida,” alisema.
Alisema
walitembea mbele kidogo ndipo alipobaini umbali kidogo kati yake na
askari ambapo pembeni yake kulikuwa na kinjia cha kujipenyeza ndipo
alipoamua kutambaa kwa magoti na kujipenyeza kwenye kinjia hicho na
kufanikiwa kujificha bila kuonekana.
Alisema
mara baada ya wenzake kupita alianza safari kwenye pori hilo bila kujua
anakokwenda mpaka alipofanikiwa kukutana na kikosi cha Polisi ambacho
kilimchukua na kumpeleka sehemu salama.
Athuman
Fadhili ambaye alitekwa hadi kuokolewa na majeshi ya DRC, alisema baada
ya mwenzake kutoroka alipata matumaini kuwa atasaidia kuwaletea msaada
hivyo waliendelea na safari kama kilometa 30 zaidi kwenye msitu huo
mnene.
Alisema
katika safari hiyo ya mateso ya siku mbili walitembea usiku na mchana
huku wakichanwachanwa na miba, walifika kwenye eneo la kijiji ambacho
hata hivyo kilikuwa na nyumba chache, wakaamriwa watembee kwa kutambaa
ili wasionekane na wanakijiji hao.
Baada
ya kilometa tano kutoka kwenye hicho kijiji walifika kwenye makazi ya
muda ya watekaji hao na kukutana na mkubwa wao aliyejitambulisha kama
Shehe Hassan aliyeamuru wapewe maji na kuanza kuwahoji majina yao
kupitia hati zao za kusafiria na kutaka kujua kuhusu familia zao.
Walibeba mizigo ya waasi
Alisema
wakiwa katika eneo hilo, mmoja wa viongozi wa watekaji hao aliyekuwa
akizungumza kwa simu na bosi wao mwingine alitoa taarifa kuwa majeshi ya
DRC yanawafuatilia hivyo wanatakiwa kujihadhari.
Baada
ya mahojiano hayo walipewa chakula na maji na kisha giza lilipoingia
walitafutiwa eneo la kulala ambalo ni hema lililowekewa turubai. Alisema
majira ya saa sita au saa saba usiku huku mvua kubwa ikiwa inanyesha,
waliamshwa na kutakiwa kuendelea na safari kwa kuwa hali ya usalama
katika eneo hilo ni tata kutokana na majeshi ya DRC kuzidi kuwakaribia.
“Tulikuwa
tumechoka sana kutokana na kubeba mizigo yetu na yao safari nzima
lakini tulilazimika kutembea tu. Ilifikia mahali tulitamani kupigwa hata
risasi ili tupumzike na kuondokana na mateso tuliyokuwa tunayapata,” alisema Fadhili.
Walitaka dola 4,000 kutoka kwa Dewji
Alisema
wakati wakiendelea kutembea, viongozi wa watekaji hao waliendelea
kuwasiliana njia nzima na bosi wa Simba Logistics, Azim Dewji na kumpa
saa 24 awe ametoa dola za Marekani 4,000 kwa kila dereva ili waachiwe
huru.
“Lakini
baadaye wao wenyewe wakaanza kubishana juu ya namna ya kuzipata fedha
hizo kutokana na hali halisi ya msitu huo. Wakaambizana fedha hizo
zipelekwe kupitia helikopta ya kampuni walikoshushia mzigo wa saruji na
madereva hao wapepee bendera kuonesha wako salama na fedha hizo
zidondoshwe,” alifafanua.
Alisema
walitembea tena umbali kidogo ndipo waliposimama na kupewa chakula aina
ya ugali wa mhogo uliokuwa umejaa michanga pamoja na mboga za majani
wasiyoyajua na kulazimika kula tu kwa kuwa walikuwa na njaa.
Fadhil
alisema waliendelea kubaki katika eneo hilo kwa muda, ndipo watekaji
hao walipomtuma kijana wao akanunua unga mjini, baada ya muda alirejea
akiwa anatweta na kuwataarifu kwa taharuki kuwa majeshi ya DRC
yamekaribia eneo hilo.
Madereva wagawanywa kwa waasi
Kutokana
na taharuki ya viongozi hao, kila mtekaji alipewa madereva wawili mpaka
watatu awaongoze na kuanza kukimbia huku watekaji hao wakiwa
wametangulia mbele.
“Walionesha
kuchanganyikiwa kwa kweli wakaanza kutufokea huku wametushikia mitutu
ya bunduki na kila kundi likaenda upande wake. Kwa kuwa wao ndio
waliotangulia, tukaanza kutoroka mmoja mmoja mpaka kwenye kundi letu
tukabaki wawili mimi na Issa,” alisema.
Alisema
baada ya kubakia wawili wakaamua pia na wao watoroke kwani hali ilikuwa
tete hivyo wakajitosa msituni na kuanza kukimbia hadi waliposikia sauti
za maaskari wa DRC zikiwaita.
“Tulisikia
wakituita kwa lafudhi yao ya kikongo, watanzania kuya (kuja) watanzania
kuya (kuja) jitokezeni sisi ni jeshi la DRC tumewaokoa. Sikuamini
masikio yangu tulijitokeza na kupewa msaada haraka,” alisema.
Dewji, Serikali ya Tanzania na Congo wazungumza
Kwa
upande wake, Dewji alilishukuru jeshi la DRC na Serikali ya Tanzania
kwa kuwa naye bega kwa bega katika harakati za kuwaokoa madereva hao na
kubainisha kuwa katika tukio hilo, magari ya kampuni yake ya Simba manne
yalichomwa moto na hivyo kupata hasara ya Sh milioni 600.
Alisema
alikuwa akiwasiliana na waasi hao kila mara wakimtaka atoe fedha hizo
ambazo alikuwa tayari kuzitoa lakini alionywa na jeshi la DRC kuwa
endapo atazitoa atawajengea tabia ya utekaji zaidi wanajeshi hao.
Aidha,
Dewji alisema Serikali ya DRC imemuahidi kuwa itaendelea kuweka usalama
kwa wafanyabiashara wa malori nchini humo na kumhakikishia ulinzi wa
doria kila kampuni hiyo itakaposafirisha mizigo yake nchini.
“Hiki
kilichotokea ni bahati mbaya, tutaendelea na biashara lakini kwa
tahadhari. Biashara yangu inagusa watu wengi si kampuni yangu pekee
endapo nitasitisha wengi wataathirika,” alisisitiza.
Balozi
wa DRC nchini, Jean Piorre Mutamba, alisema tukio hilo limemshtua na
kumpa wakati mgumu, hasa ikizingatiwa kuwa ni balozi mpya aliyewasili
nchini hivi karibuni, hivyo alitumia fikra zake zote ili kuhakikisha
madereva hao wanaokolewa.
Aliwataka
madereva hao kuhakikisha wanawasiliana na ubalozi wa DRC kabla ya
kuanza safari ili kuwawekea mazingira ya usalama zaidi na kuwafuatilia.
Kwa
upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Susan Kolimba, aliwahakikishia madereva hao kwamba tukio hilo
ni la bahati mbaya na kwamba Serikali ya Tanzania itaendelea kuwalinda
wananchi wake wanaofanya kazi nje ya nchi.
“DRC
ni nchi rafiki na tumekuwa tukifanya nao kazi nyingi. Nina imani tukio
hili haliwezi kuvunja uhusiano wetu kwani serikali zote mbili zimefanya
jitihada kubwa za kuwaokoa madereva hao,” alisisitiza.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )