Waziri
wa Fedha na Mipango, Dk Mpango amewaeleza wabunge kuwa Serikali
itaendelea kukopa mpaka kieleweke kwa kuwa hakuna dhambi kukopa ikiwa
fedha hizo zinakwenda kukuza uchumi.
Dk Mpango amesema hayo jana Jumatatu jioni wakati akijibu hoja za wabunge kuhusu Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa 2018/19.
Kuhusu
hoja kuwa Deni la Taifa linakuwa kwa kasi kubwa wakati uchumi unakua
kwa kasi ndogo, Dk Mpango alisema deni hilo ni himilivu akisema baadhi
ya wabunge wanashindwa kukokotoa hesabu.
Alisema
Deni la Taifa liliongezeka kutoka dola 22.3 bilioni za Marekani mwaka
2016 na kufikia dola 26 bilioni ilipofika mwezi Juni 2017 ikiwa ni sawa
na ongezeko la asilimia 17.
“Deni
hilo ni sawa na asilimia 31.2 ya GDP (Pato la Taifa) ikilinganishwa na
ukomo wa uhimilivu wa asilimia 56. Uhimilivu wa Deni la Taifa hupimwa
kwa kuzingatia uwezo wa nchi kulipa deni”
Dk
Mpango alitoa takwimu za nchi za Afrika Mashariki za uhimilivu wa deni
la taifa kwa nchi hizo akisema Tanzania bado iko vizuri na iko katika
nafasi nzuri ya kukopesheka na wataendelea kukopa.
Alizitaja
nchi hizo na uhimilivu wa deni lao kuwa ni Uganda ambayo ni asilimia
35.4, Rwanda asilimia 36.6, Burundi asilimia 43.4 na Kenya asilimia 50.4
akisema hali ni nzuri kulinganisha na nchi nyingine.
Alilinganisha
nchi hizo na Zambia yenye uhimilivu wa asilimia 57.2, United Republic
of Emirates asilimia 60.3, Marekani asilimia 73.8, Morocco asilimia 77
na Uingereza asilimia 92.2.
“Misri
ni asilimia 92.6, Msumbiji asilimia100.3, Italia asilimia 132.5 na
Ugiriki asilimia 181.6. Kwa takwimu hizi sisi bado tuna nafasi kubwa ya
kukopa,”alisema Dk Mpango na kuongeza;
“Tutaendelea
kukopa kwa sababu moja tu kubwa. Kwamba ni kwa ajili ya ni kukuza uwezo
wetu wa baadaye wa kumudu uendeshaji wa nchi yetu na kulinda uhuru na
heshima ya nchi yetu,” alisema.
“Napenda
nisisitize hakuna dhambi ya nchi kukopa ilimradi nchi husika itumie
fedha hizo za mkopo kukuza uwezo wa kiuchumi na kuzalisha na kurejesha
hiyo mikopo,”
“Kama
Rais (John Magufuli) alivyosema alivyokuwa ziarani Kagera kwa kweli
tutaendelea kukopa mpaka kieleweke ilimradi Deni la Taifa tuhakikishe
linaendelea kuwa himilivu.”
Kuhusu
benki za biashara nchini kuporomoka kwa kiasi kikubwa kwa mikopo
binafsi, mikopo ya biashara na mikopo ya sekta za uzalishaji, alisema
hilo limetokea nchi kadhaa.
“Katika
miezi 12 iliyoishia Septemba 2017, wastani wa ongezeko la mikopo kwa
sekta binafsi nchini Kenya ilikuwa asilimia 3.8, Tanzania asilimia 5.0,
Uganda 5.2 na Rwanda asilimia 10.3.
Dk
Mpango alikuwa akijibu hoja za baadhi ya wabunge kuwa amekuwa na kiburi
na hana ushirikiano wa wabunge na wakati mwingine hapokei simu za
wabunge wanapomtafuta kumshauri.
Kuhusu
ushiriki wa sekta binafsi, Dk Mpango alikiri kuwa ndio injini ya uchumi
lakini akasema zipo changamoto kiuhalisia na kusema “akili za kuambiwa
tuchanganye na za kwetu”
“Akili
za kuambiwa mzee Kikwete alituambia lazima tuchanganye na za kwetu
kabla ya kuamua kufikia hatua ya kuwa na sekta binafsi yenye nguvu,”
“Kweli
natamani sana wawekezaji wa ndani na nje watatupunguzia huu mzigo.
Sekta binafsi tuliyonayo bado inahitaji kulelewa ili iweze kubeba jukumu
hili.”
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )