Wakati amri ya Rais John Magufuli ya kufuta safari zote za nje ya nchi
kwa watumishi wa umma ikiendelea kushika kasi, imebainika kuwa hadi sasa
ni waziri mmoja tu ndiye walau amefanikiwa kwenda nje ya nchi baada ya
kukidhi vigezo vilivyopo.
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe, umebaini kuwa waziri huyo mwenye bahati
ya pekee hadi sasa ni Balozi Augustino Mahiga wa Wizara ya Mambo ya
Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa.
Katika agizo lake alilolitoa siku chache baada ya kuingia madarakani
Novemba 5, Rais Magufuli alisema ni marufuku kwa kiongozi au mtumishi
yeyote wa umma kwenda nje ya nchi bila ya kupata kibali kutoka kwake au
kwa Katibu Mkuu Kiongozi – Ikulu.
Taarifa zaidi zilieleza kuwa ili kiongozi au mtumishi yeyote wa umma
apate kibali cha kusafiri kwenda nje ya nchi, ni lazima aeleze wazi kuwa
safari hiyo anayotaka kwenda ina manufaa gani kwa taifa na kwamba, ni
athari zipi zitatokea kwa taifa iwapo safari hiyo haitafanyika.
Uchunguzi umebaini kuwa tangu kutolewa kwa agizo hilo, ni Balozi Mahiga
pekee ndiye aliyemudu kukidhi vigezo vya safari na hivyo kupata fursa ya
kufaidi posho zianzoambatana na safari za aina hiyo ambazo Rais
Magufuli anazipinga vikali kwa maelezo kuwa huligharimu taifa mabilioni
ya fedha ambayo yangeweza kutumika kwa shughuli nyingine za maendeleo.
Katika hotuba yake wakati akizindua Bunge Novemba 20, 2015, Rais
Magufuli alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2013/2014 na
2014/2015, taifa lilitumia zaidi ya Sh. bilioni 356.3 kwa ajili ya
kugharimia safari za nje; jambo ambalo kamwe yeye hatakubali litokee kwa
sababu fedha hizo zinaweza kukamilisha miradi mingi ya maendeleo
ikiwamo kujenga barabara ya lami ya urefu wa kilomita 400.
“Kwakweli hali ni mbaya. Safari za Ulaya, Marekani na kwingineko nje ya
nchi ndizo zilizokuwa zikitumiwa na mawaziri na vigogo wengine wa
taasisi za umma kuvuna utajiri kupitia manunuzi ya tiketi na posho… hivi
sasa anayenufaika ni Waziri Mahiga tu ambaye twaweza kusema ana bahati
sana kwa sababu wizara yake haiwezi kukwepa safari,” chanzo kimoja
kiliiambia Nipashe.
Wakati wa utawala wa awamu ya nne, mawaziri walikuwa wakisafiri mara kwa
mara, katika kile ambacho aliyekuwa waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, aliwahi kukaririwa akisema kuwa
‘walikuwa wakipishana angani utafikiri nyumbani kunawaka moto’.
Chanzo kingine kiliiambia Nipashe kuwa kabla ya kuingia Ikulu kwa
Magufuli, kuna mawaziri walikuwa wakivuna kati ya Sh. milioni saba na
milioni tisa kwa siku kupitia malipo mbalimbali wawapo nje ya nchi
lakini sasa hali iko tofauti kwani safari hizo zimebaki kuwa historia.
“Anayefaidi hapa ni Mahiga tu kwa sababu maelezo ya safari zake yako
wazi, yanajitosheleza kutokana na wizara anayoiongoza… hawa mawaziri
wengine mambo kwao ni magumu. Wapo waliojaribu kuomba safari wakaishia
kugonga mwamba kwa sababu ya kutokidhi vigezo vya kupata kibali,” chanzo
kingine kiliongeza.
MAHIGA ANAVYOFAIDI
Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa kutokana na asili ya wizara
anayoiongoza, walau Balozi Mahiga amesafiri kwenda nje ya nchi mara
nyingi kuliko hata Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Rais Magufuli
mwenyewe ambaye hadi sasa hajawahi kuvuka mipaka ya Tanzania.
Safari pekee ya Majaliwa kwenda nje ya nchi ilikuwa Januari 17 wakati
alipokwenda kumuwakilisha Rais Magufuli kwenye mkutano wa viongozi wa
Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), uliofanyika
GaboroNe, Botswana.
Baadhi ya safari za Balozi Mahiga ni pamoja na ile aliyokwenda Kigali,
Rwanda Februari 18 wakati alipokwenda kupeleka ujumbe wa Rais Magufuli
kwa Rais wa nchi hiyo, Paul Kagame na kisha akaenda Burundi kupeleka
ujumbe kama huo kwa Rais wa nchi hiyo, Pierre Nkurunzinza.
Januari 30, Mahiga alisafiri pia na Makamu wa Rais, Samia Suluhu, kwenda
Addis Ababa, Ethiopia kumuwakilisha Rais Magufuli kwenye mkutano wa 26
wa marais wa Afrika. Wakati wa Rais Kikwete, mikutano kama hiyo
ilihusisha msafara wa Rais pamoja na mawaziri wasiopungua wanne, achilia
mbali maafisa wengine mbalimbali.
Hata hivyo, licha ya unafuu wa safari za nje alio nao Mahiga, chanzo
kimedai kuwa hata yeye (Mahiga), kwa nafasi yake, ni kama hajasafiri
kitu kulinganisha na hali ilivyokuwa hapo kabla.
“Ingekuwa kipindi cha awamu ya nne, saa hizi Mahiga angesafiri mara
nyingi zaidi kuliko hivi sasa ambapo safari zake hazifiki sita… ila kwa
wengine hali ni mbaya zaidi kwa sababu hakuna aliyewahi kwenda nje ya
Tanzania,” chanzo kiliiambia Nipashe.
BILIONI 7/- KATIKA SIKU 100
Wakati akizungumzia siku 100 za Rais Magufuli tangu aingie Ikulu,
aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema Sh. Bilioni 7
zimeokolewa kwa kupiga marufuku safari holela za viongozi kwenda nje ya
nchi.
WAZIRI KITWANGA AKIRI KUTOSAFIRI
Alipoulizwa kuhusu safari za nje, Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles
Kitwanga, alisema yeye ni miongoni mwa wengi ambao hadi sasa hajawahi
kusafiri kwenda nje ya nchi tangu aapishwe na Rais John Magufuli kushika
wadhifa huo.
Alisema ameshindwa kufanya hivyo kwa sababu hajawahi kupata mwaliko au kutumwa na Rais Magufuli, kusafiri kwenda nje ya nchi.
“Mimi sijawahi kwenda kwa sababu sina shughuli za kufanya huko na wala
Rais hajawahi kunituma… sasa naendaje bila kutumwa wala kuwa na
mwaliko?” Alisema Kitwanga.
MWIJAGE, MWIGULU MBIONI KUSAFIRI
Baada ya kutokwenda nje ya nchi tangu waapishwe, hatimaye Waziri wa
Viwanda na Biashara, Charles Mwijage na Waziri wa Kilimo, Mifugo na
Uvuvi, Mwigulu Nchemba wanatarajiwa kusafiri kwa mara ya kwanza baada ya
Rais Magufuli kuwaruhusu juzi kwenda Vietnam kujifunza mbinu za kuinua
kilimo na kujenga viwanda.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )