WAZIRI
wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Bw. Mwigulu Nchemba amesema hakuna chama
cha siasa ambacho kinaweza kuthaminishwa na maisha ya mwanadamu na
kwamba wananchi hawana sababu ya kupigana na kutoana uhai kwa sababu ya
ushabiki wa vyama.
Ametoa
kauli hiyo jana mchana (Alhamisi, Machi 17, 2016) wakati akizungumza
na mamia ya wakazi wa mji mdogo wa Katoro, wilayani Geita alipopewa
nafasi kuwasalimia wananchi kwenye mkutano wa Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa.
“Duniani
kote hakuna chama cha siasa kinaweza kuwa na thamani sawa na maisha ya
mwanadamu au damu ya mwanadamu. Ninazungumza hili nikihusisha na matukio
ya hivi karibuni hapa Geita na kule Tunduma ambako raia wetu walipoteza
maisha kwa sababu ya tofauti za kisiasa, “alisema.
Aliwauliza wananchi hao ni kwa nini wanapigana hadi kutoana uhai wakati wao (wananchi) hawaendi bungeni. “Ninyi
mnaopigana hakuna hata mmoja wenu anayeingia bungeni lakini sisi
tukikutana kule bungeni tunasalimiana na kugongeshana glasi. "
Akitolea
mfano kauli hiyo, Waziri Mwigulu alisema wakati waneenda kwenye msiba
wa wana CCM waliouawa huku Tunduma, baada ya mazishi yeye na Mwenyekiti
wa CHADEMA, Bw. Freeman Mbowe pamoja na wanasiasa wengine walikaa na
kula nyama za kuchoma hadi saa usiku.
“Nini kinachowafanya muwe maadui wa siasa kiasi hicho?” alihoji na kuongeza:
“Mnasababisha
watoto wasio na hatia tena wasiojua siasa wawe yatima. Duniani siasa
hazina tofauti kama zilivyo mechi za mpira. Leo unavaa jezi hii na kesho
jezi ile. Acheni kufanya uadui katika siasa”,alionya.
Wakati
huohuo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema atamtuma Waziri wa Nishati
na Madini, Prof. Sospeter Muhongo aende Geita keshokutwa (Jumamosi,
Machi 19, 2016) ili akasikilize malalamiko ya wananchi hao juu ya suala
la magwangala.
Magwangala
ni mchanga uliochimbwa mgodini na kuchujwa na sasa unatakiwa kuchujwa
tena ili utolewe mabaki ya madini na wachimbajiwadogo wadogo.
“Nimemuita
Profesa Muhongo aje na timiu yake ya wakurugenzi pamoja na wataalamu wa
STAMICO ili waje wakamilishe suala hili. Najua lilikwishaanza
kughughulikiwa tangu Makamu wa rais alipopita hapa mwezi uliopita na
sasa nimeambiwa kuwa limefikia asilimia 75 ya utekelezaji,” alisema.
Waziri Mkuu amemaliza ziara ya mkoa huo na alirejea jijini Dar es salaam jana jioni
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )