Jeshi la polisi Mkoani Manyara linamshikilia mkazi wa Kijiji cha Dongobesh Wilayani Mbulu, Mussa Selemani (28) akidaiwa kumpiga jiwe kwenye paji la uso askari polisi wa kituo cha polisi Dongobesh na kusababisha akapoteza fahamu.
Hadi hivi sasa askari polisi huyo ambaye alipigwa jiwe hilo wakati akiwa kituoni amelazwa kwenye hospitali ya rufaa ya Haydom, amepoteza fahamu na anaendelea kupatiwa matibabu huku akiwa na jeraha katika paji la uso wake.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Francis Massawe alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa kwenye kijiji hicho baada ya kumpiga jiwe askari huyo akiwa kituoni na kisha kukimbilia kusipojulikana.
Kamanda Massawe alimtaja askari polisi huyo kuwa ni PC Boniface mwenye G 8404 na tukio hilo lilitokea Aprili 15 mwaka huu saa 3 usiku wakati akiwa kwenye kituo cha polisi cha Dongobesh.
Alisema siku ya tukio hilo PC Boniface alikuwa anaandika maelezo ili awapatie fomu namba 3 (PF3) ya matibabu wazazi wawili waliofika na mtoto wao mwenye miaka 7 kituoni hapo kwa ajili ya kutibiwa wakidai kuwa alipigwa.
Alisema wakati akiandika maelezo hayo ndipo Selemani akatokea akiwa amelewa na kuingilia kati mahojiano hayo hivyo kusababisha usumbufu ndipo PC Boniface akamtoa nje kwa nguvu ili aweze kuendelea na kazi yake ipasavyo.
“Wakati PC Boniface anaendelea kuandika maelezo ya watu hao, ghafla Selemani alimpiga jiwe na kupoteza fahamu kisha akakimbizwa kwenye hospitali ya rufaa Haydom kwa matibabu,” alisema Kamanda Massawe.
Alisema baada ya tukio hilo Selemani alikimbia na wale watu wawili na mtoto wao nao wakakimbia ila polisi walifanikiwa kumkamata mhalifu huyo na askari huyo amelazwa hospitali ya rufaa ya Haydom na hali yake siyo nzuri bado hajitambui.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )