Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) amemuondolea kosa la mauaji aliyekuwa mkuu wa upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Zombe na sasa inataka ajibu mashtaka ya kuficha wahalifu.
DPP amefanya mabadiliko hayo kwenye rufaa aliyoikata Mahakama ya Rufani dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu wa kumuachia huru Zombe, ambaye alikuwa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) katika mashtaka ya mauaji.
Awali, DPP alikata rufaa akipinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyomwachia huru Zombe na wenzake tisa, katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara wa madini kutoka Mahenge mkoani Morogoro na dereva mmoja wa teksi wa Manzese jijini Dar es Salaam.
Katika rufaa hiyo, DPP alikuwa anaiomba Mahakama ya Rufani iwatie hatiani washtakiwa hao kwa kosa la mauaji ya kukusudia, kama ilivyokuwa kwenye kesi ya msingi, kosa ambalo adhabu zake ni pamoja na kunyongwa hadi kufa.
Hata hivyo, DPP amebadili msimamo huo dhidi ya Zombe na badala yake anaiomba Mahakama hiyo imtie hatiani kwa kosa la kuwalinda wahalifu ambao walitenda kosa la mauaji ya wafanyabiashara hao na dereva wa teksi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Timoth Vitalis, ambaye ni Wakili Mkuu wa Serikali (PSA) na Richard Rweyongeza, ambaye ni wakili wa kujitegemea anayemtetea Zombe katika rufaa hiyo, walisema mtu anayepatikana na hatia kwa kosa hilo adhabu yake ni kifungo jela kisichozidi miaka saba.
Kwa maana hiyo, hata kama Mahakama ya Rufani itakubaliana na hoja za rufaa za DPP na kumtia hatiani Zombe kwa kosa hilo jipya ambalo hata hivyo, hakuwa ameshtakiwa nalo kwenye kesi ya msingi, atakuwa ameepuka adhabu ya kitanzi.
DPP alibadili msimamo wake huo dhidi ya Zombe siku ya usikilizwaji wa rufaa hiyo Mahakama ya Rufani mbele ya jopo la majaji watatu, Bernard Luanda, Sauda Mjasiri na Semistocles Kaijage, hivi karibuni.
Mkurugenzi huyo wa mashtaka alifikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha kuwa hakuna ushahidi wa kumtia hatiani Zombe kwa kosa hilo la mauaji. Akizungumzia uamuzi huo wa DPP kumuondoa kwenye shtaka la mauaji kama alivyokuwa akidaiwa tangu awali na sasa kupewa shtaka la kuwalinda wahalifu, Zombe alisema kwanza alikuwa ameonewa kwa kuhusishwa na hatimaye kushtakiwa kwa kosa la mauaji.
Alisisitiza kuwa hakutendewa haki wakati wa kumfungulia shtaka hilo la mauaji kwa kuwa sheria hazikufuatwa.
"Kwanza ni mambo ya ajabu sana. Nimedhalilishwa sana kwa muda wote huo na kuonekana kuwa mimi ni muuaji kila ninakopita, kwa kufunguliwa shtaka ambalo sikuhusika nalo," alisema Zombe.
"Mimi sikuwapo eneo la tukio na wala nilikuwa siwafahamu watu hao na hata Tume (iliyoundwa na Rais kuchunguza mauaji hayo iliyoongozwa na Jaji Mussa) Kipenka ililiridhika kuwa sikuwepo eneo la tukio. Sasa nilihusikaje na mauaji hayo?"
Zombe aliongeza kuwa washtakiwa wote walihojiwa na kuandika maelezo yao na kwamba huo ndiyo utarartibu wa kisheria. Zombe alisisitiza kuwa yeye alikuwa mwendesha mashtaka kwa muda mrefu na mkuu wa upelelezi wa mkoa, hivyo anajua taratibu kwa kuwa alikuwa akiandika majalada mengi kwenda kwa Mwanasheria wa Serikali na mengine yalikuwa yakienda mahakamani kama alivyoyaandika.
Kuhusu kosa alilobadilishiwa na DPP wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo, Zombe hakuwa tayari kulizungumzia kwa kuwa bado Mahakama haijatoa hukumu. Kabla ya kumbadilishia shtaka hilo, wakati wa usikilizwaji wa rufaa, DPP alitaka kumuongezea Zombe shtaka hilo kama shtaka mbadala, wakati wa usikilizwaji wa kesi ya msingi.
Hata hivyo, DPP aligonga mwamba baada ya Jaji Massati kumkatalia kwa maelezo kuwa alitakiwa ashtakiwe tangu mwanzo kwa kosa hilo. Kabla ya kumuondoa Zombe katika kosa la adhabu hiyo ya kunyongwa, kwanza DPP, aliwaondolea washtakiwa wengine watano, baada ya kubaini kuwa ushahidi aliokuwa nao hauwagusi katika rufaa hiyo. Walioondolewa ni Jane Andrew, Emmanuel Mabula, Michael Shonza, Abineth Salo na Festus Gwabisabi. Lakini ameendelea kuwang'ang'ania Zombe na wenzake watatu ambao ni Christopher Bageni, Ahmed Makelle na Rajabu Bakari.
Source: Mwananchi
SIGNATURE
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )