Featured
Loading...

Familia ya Aliyeuawa kesi ya Zombe na wenzake Yamuomba Rais Magufuli Awasaidie


 


Aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Kinondoni, SP Christopher Bageni akisindikizwa kupanda gari la askari baada ya kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa.
***
 
Baada ya Mahakama ya Rufani kutoa hukumu dhidi ya vigogo wa polisi katika mauaji wafanyabiashara wa madini, familia ya mmoja wa marehemu amemuomba Rais John Magufuli kuwasaidia yatima walioachwa. 
Akizungumza jana, Martha Martine ambaye alikuwa mke wa marehemu Mathias Lunkombe alisema kwa kuwa mahakama imeshatoa hukumu hiyo, hawezi kupingana nayo, badala yake akaeleza namna kifo cha mumewe kilivyoiathiri familia, hususan watoto wawili alioachiwa. 
Katika hukumu hiyo iliyotolewa juzi, aliyekuwa mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai Wilaya ya Kinondoni, Christopher Bageni alihukumiwa kunyongwa hadi kufa huku Abdallah Zombe na wenzake wawili wakiachiwa huru. 
Hukumu hiyo ilitolewa baada ya rufani ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ambaye hakuridhishwa na hukumu ya Mahakama Kuu ambayo iliwaachia huru washtakiwa hao. 
Bageni alikuwa ni miongoni mwa washtakiwa kwenye kesi hiyo iliyokuwa inawakabili askari polisi tisa akiwamo Zombe ambaye alikuwa Mkuu wa upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam. 
Wafanyabiashara Sabinus Chigumbi, ndugu yake Eprahim Chigumbi na Mathias Lunkombe na dereva teksi, Juma Ndugu waliuawa Januari 14, 2006 kwenye Msitu wa Pande uliopo Mbezi Luis, Dar es Salaam. 
Kutokana na hukumu hiyo, Martha alisema kwa sasa anaishi maisha magumu kwa kuwa anatumia fedha nyingi kuwasomesha watoto wake Grace anayesoma kidato cha nne na Fulmes anayesoma kidato cha pili. 
Alisema Serikali ilimuahidi kumsaidia kutunza watoto lakini hakuna msaada wowote alioupata kutoka serikalini wala kwa kiongozi yeyote. 
Kutokana na hali hiyo, Martha alimwomba Rais Magufuli kuwasaidia watoto hao kupata elimu na mahitaji mengine muhimu ili waweze kuja kujitegemea kimaisha. 
Mdogo wa marehemu Protas, Mathias Lunkombe alisema tangu kaka yake alipofariki amekuwa akihudumia familia mbili, ya kwake na ya marehemu kaka yake. 
Kuhusu hukumu iliyotolewa, alisema haki imetendeka kwa kumhukumu Bageni kunyongwa hadi kufa japokuwa hakuna hukumu ambayo ingeweza kupoza au kuondoa machungu waliyonayo kwa ndugu yao aliyeuawa. 
“Pamoja na kumuua kaka yangu lakini kifo chake ni cha kumdhalilisha kwa sababu walimsingizia kuwa ni jambazi ilhali ni mfanyabiashara wa madini. "

Mke wa Bageni asita 
Wakati familia ya Lunkombe ikisema hayo, mke wa Bageni amekataa kuzungumzia hukumu kifo iliyotolewa kwa mumewe. 
“Mimi ni askari, nipo chini ya Kamishina (wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon) Sirro, siwezi kuongea na waandishi wa habari siruhusiwi kuongea chochote,” alisema mke wa Bageni, Stella Saria na kuongeza: 
“Kijeshi sisi tuna miiko ya kazi, kama mume wangu amepata matatizo hayo ni mambo ya kawaida, mimi nina viongozi wangu wa kazi, nilivyofundishwa kama ni kitu cha familia yangu, Christopher alikuwa ofisa wa polisi watajibu viongozi wake wapo. 

“Mimi nina amani ya kutosha, ni Mkristo nimempokea Yesu, tatizo haliwezi kunitokea nikadharau miiko ya kazi. Mimi ni kiongozi askari, naelewa miiko ya kazi lazima niiheshimu, samahani sana.” 

Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
© Copyright MZALENDO HURU
Back To Top