WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amekutana na kufanya
mazungumzo na Balozi wa Japan nchini, Mheshimiwa Masaharu Yoshinda
ambaye amemueleza kwamba Serikali yake ipo tayari kukarabati shule
zilizoharibiwa na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera.
Pia imeomba kupatiwa orodha ya mahitaji ya dharura yakiwemo mahema, mablanketi, dawa na vifaa tiba kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa tetemeko hilo.
Balozi Yoshinda ameyasema hayo leo (Jumatatu,
Septemba 19, 2016) wakati alipokutana na Waziri Mkuu ofisini kwake
Magogoni Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuzungumzia masuala ya maafa
yalitokea Kagera.
Kwa upande wake Waziri Mkuu ameishukuru Serikali
ya Japan kwa hatua hiyo na kukiagiza Kitengo cha Maafa kilicho chini ya
Ofisi yake kuwasiliana na Ubalozi wa Japan nchini na kuwasilisha orodha
ya shule zilizoharibika pamoja na mahitaji ya dharura.
Wakati huo
huo Waziri Mkuu amepokea msaada wa tani 2.5 za mchele, magodoro 200,
mablanketi 100 na fedha taslimu sh. milioni 10 ili kusaidia wananchi
waliothirika na tetemeko hilo.
Msaada huo umetolewa na wadau
mbalimbali akiwemo Ofisa Utumishi wa Kampuni ya Chang Qing Inernational
Investiment Limited ya nchini, Bi. Anna Jiang aliyetoa magodoro 200
yenye thamani ya sh. milioni sita.
Wengine ni Mkuu wa Kitengo cha
Fedha wa Benki ya Exim, George Shumbusho aliyetooa sh. milioni 10 pamoja
na Katibu Mkuu wa Chama cha Urafiki kati ya Serikali ya Tanzania na
China, Bw. Joseph Kahama aliyetoa mchele tani 2.5 pamoja na mabllanketi
100 vyote vikiwa na thamani y ash. milioni 10.
Waziri Mkuu
amewashukuru kwa misaada hiyo na kuwaomba wananchi wengine wajitokeze
kwa wingi ili kuwasaidia watu walioathirika na tetemeko hilo ambalo ni
kubwa na halijawahi kutokea nchini.
Tetemeko hilo lilitokea
Jumamosi, Septemba 10, 2016 na kusababisha vifo vya watu 17 na wengine
440 walijeruhiwa kati yao watu 253 walifikishwa Hospitali ya Mkoa, 153
walilazwa, 113 wametibiwa na kuruhusiwa na wengine 38 wanaendelea na
matibabu ambapo kati yao watu 23 wamefanyiwa upasuaji mkubwa na
wanaendelea vizuri.
Pia tetemeko hilo limesababisha nyumba 2,063
kuanguka huku nyingine 14,081 zikiwa katika hali hatarishi baada ya
kupata nyufa na 9,471 zimepata uharibifu mdogo huku wananchi 126,315
wakiiitaji misaada mbalimbali.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Balozi wa Japan nchini, Masaharu
Yoshida kuhusu namna ambavyo Japan inaweza kusaidia waathika wa tetemeko
la ardhi mkoani Kagera. Mazungumzo yao yalifanyika Ofisini kwa Waziri
Mkuu jijini Dares salaam Septemba 19, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu).
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM.
JUMATATU, SEPTEMBA 19, 2016
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )