Muammar Gaddafi akiwa Rais wa Libya na wakati huo nchi hiyo ikiwa imewaka moto kwa mapigano makali kati ya waasi na vikosi vya serikali, rafiki yake Rais Jacob Zuma alituma Jet yake hadi Tripoli, Libya kumfuata Gaddafi ambaye aligoma na miezi michache baadaye aliuawa na waasi.
Jonas Savimbi akiwa amezungukwa na walinzi wake enzi za uhai wake.Jonas Savimbi akiwahutubia wafuasi wake.
Ndivyo ilivyokuwa kwa Jonas Savimbi ambaye kitendo chake cha kugomea
kurudiwa kwa uchaguzi wa rais wa nchi hiyo na kuamua kuingia msituni
kulipelekea kuuawa kwake. Savimbi alifanya kosa moja kubwa alilazimisha
vikosi vyake kuingia msituni kupambana na serikali akiwa bado
hajajipanga vyema, ni bora angekubali kurudia uchaguzi dhidi ya Rais Dos
Santos huku akijipanga.Bahati mbaya hakulikumbuka hilo, aliwaza jambo moja tu kuingia msituni kuandaa kikosi chake tayari kuuondoa utawala wa Dos Santos.
Aliingia msituni kipindi ambacho tayari kikosi chake kilikuwa kimeingiliwa na vibaraka ‘spy’ kutoka ndani ya kabila lake, vibaraka hawa waliandaliwa kwa ustadi mkubwa na ndiyo walihusika kutoa siri zote za nini kilikuwa kinaendelea kwenye kikosi cha Savimbi.
TAARIFA YA KUUAWA KWAKE
Februari 22, 2002 vyombo vingi vya habari duniani kote vilitawaliwa na habari kubwa ya kuuawa kwa komando wa vita, mbabe wa wababe, mfalme wa pori na mwanaume aliyeisumbua serikali ya Angola kwa zaidi ya miaka 27 akiongoza vita vya msituni dhidi ya vikosi vya serikali.
HISTORIA YAKE
Jonas Malheiro Savimbi, alikuwa mtoto wa pekee kwa baba yake Lote, aliyekuwa mfanyakazi wa reli ya Benguela na mhubiri wa kanisa la Protestanti lililokuwa likifadhiliwa na Wamarekani.
Pamoja na baba yake kuwa muumini wa dini kamwe Jonas hakuwa muumini, tangu utoto wake alikuwa mtukutu.
Wazazi wake wote wawili walikuwa wanatoka kabila la Bieno ambalo baadaye ndiyo likawa msingi wa nguvu kubwa ya Jonas Savimbi kijeshi, kwani aliunda jeshi imara kwa kuwachukua ndugu zake na watu wa kabila lake hali iliyopelekea kuwa na jeshi imara na lenye umoja na mshikamano.
Waliwasiliana kwa kutumia lugha yao na ilikuwa ngumu kwa mtu asiye kabila la Bieno kuingia. Alifanya hivyo lengo likiwa kuwakwepa vibaraka ‘spy’ wa serikali.
Baada ya kumaliza elimu yake ya msingi alibahatika kwenda kusoma elimu ya sekondari nchini Ureno na akiwa huko alikutana na mwanaharakati Augustino Neto ambaye baadaye alikuja kuwa rais wa kwanza wa Angola.
HARAKATI ZAKE
Mwaka 1966 baada ya kurejea kutoka nchini China ambako alienda kupata mafunzo ya kijeshi alirudi na kuunda UNITA na kuanza kupambana na serikali ya kikoloni sambamba na vyama vingine ambavyo vyote vilikuwa vikipigana kumtoa mreno.
Hapa ndipo jina la Jonas Savimbi likaanza kusikika kote duniani kutokana na mbinu kubwa za kijeshi alizonazo huku akisapotiwa na wananchi kutoka kabila lake la Bieno.
Huku akipata sapoti kubwa kutoka China na baadaye Marekani, aliongoza vita vikali kwa muda wa miaka zaidi ya 20 huku akiwa ni tishio kubwa kwa Serikali ya Luanda. Kuna muda aliwahi karibia kuipindua serikali ya Rais Dos Santos.
Akiwa na uwezo wa kuzungumza lugha saba kiufasaha zikiwemo tatu za ndani ya bara la Afrika na nne nje ya bara aliweza kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali kuwaomba msaada wa zana za kivita na alifanikiwa kuwa na jeshi imara.
Aliwahi kunusurika kuuawa mara kadhaa likiwemo jaribio la Februari 1990 ambapo aliponea chupuchupu na kukimbilia nchini Marekani na kufanikiwa kuonana na Rais Bush ambaye alimuahidi kumuongezea zana zaidi za kijeshi na baada ya kupona alirejea nchini Angola kuendeleza mapambano.
Baada ya kunusurika kuuawa zaidi ya mara 20 na vikosi vya serikali ya Angola huku taarifa za kuuawa kwake zikiripotiwa zaidi ya mara 15 hatimaye 22 Februari 2002 Jonas Savimbi aliuawa.
Maauaji yake yalitokea kwenye mapigano baina ya vikosi vyake dhidi ya serikali kwenye mto uliopo jimbo la Moxico eneo ambalo alizaliwa. Mapigano hayo ya kushtukiza yalipangwa baada ya vibaraka kutoa siri za mahali alipo Savimbi na baadhi ya wasaidizi wake muhimu, haikuwa kazi rahisi kumuua.
Kwenye shambulio hilo kali kuwahi kufanywa na vikosi vya serikali dhidi ya kikosi cha Savimbi walifanikiwa kumpiga risasi 15 mwilini mwake, alipigwa kichwani, kifuani na sehemu za miguuni na aliweza kumudu na kuendeleza mapambano kwa zaidi ya saa nne kabla ya kuishiwa damu na kuanguka chini na kufariki.
Tukio la kuuawa kwake bado limeacha maswali
mengi mpaka leo inakuwaje na aliwezaje kuhimili kuendeleza mapambano
hata baada ya kupigwa risasi 15 mwilini mwake?
Alizikwa kwenye makaburi ya nyumbani kwao
ya Luena na kuhudhuriwa na wapiganaji mbalimbali wa UNITA. Mauaji yake
yalimaanisha mwisho wa mapigano ya msituni nchini Angola, Chuma kilikuwa
kimeangushwa, wasaidizi wake hawakuwa na mbinu na uwezo kama Savimbi.
Baada ya kifo chake serikali kuu ilitangaza ya kwamba hatimaye
wameangusha mbuyu wa chuma uliowasumbua miaka mingi.
Wapo wanaoamini mpaka kesho kwamba Jonas
Savimbi hakuwa binadamu wa kawaida, walimuona ni binadamu wa pekee
mwenye uwezo mkubwa kuliko binadamu wa kawaida. Wenye imani potofu
walimfananisha na jini au mzimu unaotembea popote na wakati wowote bila
kujali hatari iliyo mbele yake.
Hadi mauti yake yanamkuta ameacha watoto na wake wengi ambao idadi
yake haijawekwa wazi kulingana na sehemu kubwa ya maisha yake alikuwa
akiishi msituni.Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )