Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 19 Septemba, 2016 amefanya
ziara ya kushitukiza katika Ofisi za Gazeti la Uhuru zilizopo Mtaa wa
Lumumba Jijini Dar es Salaam na kuzungumza na wafanyakazi.
Katika
Mazungumzo hayo, wafanyakazi wa Gazeti la Uhuru linalomilikiwa na CCM
wamelalamikia kutolipwa mishahara yao kwa miezi saba, kutotolewa kwa
michango ya wafanyakazi kwa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), kuuzwa
kwa mtambo wa kuchapisha magazeti katika hali ya kutatanisha,
kutotambuliwa katika ajira kwa baadhi ya wafanyakazi, kutolipwa kwa
madeni wanayozidai taasisi za Serikali na wanaostaafu kutolipwa mafao
yao.
Wafanyakazi
hao pia wamemueleza Rais Magufuli kuwa Bodi na Menejimenti ya kampuni
ya vyombo vya habari vya chama inayoendesha Gazeti la Uhuru na Redio
Uhuru zimeshindwa kuendesha vyombo hivyo na wamemuomba aingilie kati ili
kuvinusuru vyombo hivyo ambavyo kwa sasa vina hali mbaya kutokana na
kukabiliwa na madeni makubwa, na biashara yake imeshuka kwa kiasi
kikubwa.
Akijibu
malalamiko hayo Rais Magufuli aliyetembelea ofisi za Gazeti la Uhuru
akitokea Ofisini kwake katika jengo la Makao Makuu ya chama, Ofisi Ndogo
ya Lumumba Jijini Dar es Salaam amemuagiza Katibu Mkuu wa CCM
Abdulrahaman Kinana kuhakikisha mishahara yote wanayodai wafanyakazi
inayofikia Shilingi Milioni 609 inalipwa ndani ya Mwezi huu wa Tisa.
Aidha
ameagiza kupatiwa orodha ya taasisi za Serikali zinazodaiwa na Magazeti
ya Uhuru na Mzalendo, na pia ameagiza deni linalodaiwa na NSSF kutokana
na kutowasilishwa kwa makato ya wafanyakazi lilipwe.
Kuhusu
malalamiko dhidi ya Bodi na Menejimenti ya Kampuni hiyo, ajira za
wafanyakazi, mafao kwa wastaafu, kuuzwa kwa mtambo wa kuchapisha
magazeti na mazingira magumu ya kazi Dkt. Magufuli ameahidi kuyafanyia
kazi.
KK
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )