Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe
27 Septemba, 2016 amepokea msaada wa Shilingi Milioni 545 kutoka kwa
Waziri Mkuu wa India Mhe. Narendra Modi kwa ajili ya kusaidia wananchi
wa Mkoa wa Kagera waliopatwa na maafa ya tetemeko la ardhi lililotokea
tarehe 10 Septemba, 2016.
Hundi ya fedha hizo imekabidhiwa leo Ikulu Jijini Dar es Salaam na Balozi wa India hapa nchini Mhe. Sandeep Arya na baadaye Rais Magufuli akaikabidhi kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.
Katika
barua yake kwa Rais Magufuli iliyosomwa na Balozi Sandeep Arya, Waziri
Mkuu wa India Mhe. Narendra Modi amesema Serikali na Wananchi wa India
wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kutokea kwa maafa hayo
yaliyosababisha vifo vya watu na uharibifu wa mali.
"Tunaziombea
amani na uvumilivu familia zote zilizopatwa na madhara na pia tunapenda
kuwahakikishia kuwa tupo pamoja na marafiki zetu Serikali ya Tanzania
katika kipindi hiki kigumu" amesema Waziri Mkuu Modi.
Kwa
Upande wake Rais Magufuli amemshukuru Waziri Mkuu wa India Mhe.
Narendra Modi na Serikali yake kwa kutoa mchango huo na kutuma salamu za
rambirambi, na amesema Serikali yake imeguswa na moyo wa upendo
waliounesha.
"Mhe.
Balozi Sandeep Arya naomba unifikishie shukrani zangu za dhati kwa
Waziri Mkuu Mhe. Narendra Modi, mwambie kwa niaba ya Serikali yangu
tunamshukuru sana kwa kutoa msaada huu muhimu kwa ajili ya Watanzania
wenzetu waliopatwa na maafa kule Kagera.
"Mwambie
ameonesha moyo wa upendo na ushirikiano kwetu na tumefarijika kwamba
marafiki zetu mmeguswa kwa namna ya kipekee na tatizo lililoipata nchi
yetu" amesema Rais Magufuli.
Wakati
huo huo, Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa
Kagera Bw. Amantius Msole na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya
Bukoba Bw. Steven Makonda baada ya kubaini kuwa wamefungua akaunti
nyingine ya benki kwa kutumia jina linalofanana na akaunti rasmi ya
kuchangia maafa iitwayo "Kamati Maafa Kagera" kwa lengo la kujipatia
fedha.
Taarifa
iliyotolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Kassim Majaliwa muda mfupi baada ya kupokea hundi ya msaada kutoka kwa
Waziri Mkuu wa India imeeleza kuwa pamoja na kutengua uteuzi huo Rais
Magufuli ameagiza vyombo vya dola vichukue hatua dhidi ya wote
waliohusika katika njama za kufungua akaunti hiyo.
Aidha,
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mhasibu Mkuu wa
Mkoa wa Kagera Bw. Simbaufoo Swai kutokana na kuhusika katika njama
hizo.
Hata
hivyo Mhe. Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wananchi na taasisi
mbalimbali kuendelea kuchangia misaada kwa ajili ya walioathirika kwa
kutumia akaunti rasmi ya "Kamati Maafa Kagera" ambayo imetangazwa na
Serikali.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
27 Septemba, 2016
Rais
Dkt. John Pombe Magufuli akimshukuru Balozi wa India hapa nchini
Sandeep Arya mara baada ya kupokea mfano wa hundi yenye thamani ya
Shilingi za Kitanzania milioni 545 Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais
Dkt. John Pombe Magufuli akijadiliana jambo kwa furaha na Balozi wa
India hapa nchini Sandeep Arya mara baada ya kupokea mfano wa hundi
yenye thamani ya Shilingi za Kitanzania milioni 545 Ikulu jijini Dar es
Salaam. Kushoto ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na kulia ni Katibu Mkuu
wa Mambo ya Nje Balozi Dkt. Aziz Mlima. .
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )