Mamlaka
ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali itakuwa na uwezo na mamlaka ya
kuchunguza watu waliozaliwa na jinsi mbili na kubaini jinsi tawala yenye
nguvu zaidi.
Muswada
wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa Mwaka
2016, uliopitishwa juzi usiku saa nne bungeni unampa Mkemia Mkuu mamlaka
ya kuchunguza na kubaini jinsi ya mtu na kutatua utata kwa mtu
atakayekuwa amezaliwa na jinsi mbili.
“Waheshimiwa
wabunge naona wengi wenu mnadhani mkemia mkuu kazi yake ni kuchunguza
vinasaba kubaini uhalali wa mzazi na mtoto, maana naona wabunge wengi
wamelishabikia hilo, lakini katika teknolojia ya vinasaba yanahusu pia
utambuzi wa jinsi, watu unakuta wanawake au wanaume wanazaliwa jinsi ya
kike na kiume, kwa hiyo tunaangalia jinsi tawala ni ipi ina nguvu,” alisema Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
Ummy
alikuwa akijibu michango ya wabunge waliochangia wakati wa kujadili
Muswada wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu 2016 kabla ya kuupitisha
juzi usiku, waliotaka mamlaka ya maabara ya mkemia mkuu kutoa elimu kwa
wananchi juu ya shughuli zake.
Alisema
kwa sheria hiyo, sasa mkemia mkuu kupitia maabara yake anaweza kusema
jinsi ya kike au ya kiume ndio yenye nguvu, lakini pia kuna suala la
kuhakikisha utambuzi wa mwanadamu hasa wakati yanapotokea majanga pamoja
na watu wanaosafiri kwa makundi.
Alikubaliana
na wabunge kuwa iko haja ya kuwaelimisha wananchi juu ya kazi za
maabara ya mkemia mkuu ambao wengi wao wanadhani inafanya kazi hiyo tu
ya kubaini vinasaba vya mzazi na mtoto, lakini sasa wafahamu hata
waliozaliwa na jinsi mbili wanaweza kutegua utata huo kwa kubaini jinsi
tawala au jinsi yenye nguvu zaidi kama ni ya kiume au ya kike.
Alisema
Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imekuwepo kihistoria tangu mwaka
1890 na imekuwa chombo cha kiserikali cha uchunguzi cha kikemia wa
kimaabara kwa bidhaa mbalimbali na kuongeza kuwa imekuwa ikifanya
uchunguzi wa kikemia wa vyakula, dawa na vipodozi hasa pale inapotokea
utata au kuhusisha masuala ya kesi za jinai.
Akifafanua
zaidi, alisema kwa upande wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) wao
wanafanya udhibiti wa ubora wa chakula, dawa na vipodozi na maabara hii
inafanya uchunguzi wa kikemia.
“Maabara
ya Mkemia Mkuu kazi yake ni kufanya uchunguzi wa kikemia, vinasaba,
kesi za jinai na sayansi jinai. Chombo hiki hakipimi kudhibiti ila
kufanya uchunguzi kwa ajili ya vitu vyenye maslahi ya taifa au masuala
yenye utatanishi na ushindanishi,” alisema waziri huyo.
Akitoa
mfano wa mahindi, alisema kulikuwa na tatizo la sumu kuvu, kwa hiyo
mkemia mkuu anafanya uchunguzi wa kimaabara na kusema wamekuta mahindi
yana sumu au la, au anaweza mfanyabiashara kuleta maziwa ya mtoto TFDA
ikapata mashaka, mkemia mkuu atayafanya uchunguzi wa maabara atasema
kama kuna sumu ama kuna kemikali isiyo salama kwa matumizi wa binadamu.
“Baada
ya uchunguzi wa kimaabara mwenye jukumu la kusema mahindi haya yasiuzwe
au maziwa haya yasiuzwe ni TFDA na sio maabara ya mkemia mkuu. Vile
mfanyabiashara anaweza kuleta bidhaa, TFDA ikaitilia mashaka, kwa hiyo
huyu mwenye bidhaa anaweza kukata rufaa kwa mkemia mkuu ili apimiwe
bidhaa yake kuithibitishia TFDA kuwa bidhaa yake ni salama,” alisema.
Waziri
Ummy alikuwa akijibu hoja za wabunge, ambao walikuwa wana hofu kuwa
Maabara ya Mkemia Mkuu inaweza kuingilia kazi za taasisi kama TFDA na
Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Alizungumzia
pia kuhusu kuipa mamlaka ya mwisho maabara hiyo, akisema katika nchi
zote duniani zenye maabara hizo, lazima serikali iwe na msemaji wa
mwisho wa uchunguzi wa masuala ya kimaabara na kikemia, vinasaba,
sayansi jinai na kesi za jinai, lakini pia haifuti sheria wala maabara
zingine za uchunguzi zilizoanzishwa kwa mujibu wa sheria mbalimbali.
Kuhusu
kutenga bajeti ya kutosha, Ummy alisema serikali imepokea maoni ya
wabunge na kuwa baada ya kupitisha muswada huo maabara hiyo imepewa
hadhi ya mamlaka na sasa imepewa hadhi na hivyo fungu lake lazima liwe
zuri kwa ajili kuendesha shughuli za maabara lakini pia kuajiri
watumishi 400 kwani waliopo sasa 192 hawatoshi.
Waziri
Ummy alisema wamepokea ushauri wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, kufanya
uchunguzi wa matumizi ya shisha na kuongeza kuwa tayari mkemia mkuu
alifanya uchunguzi na kubaini watumiaji wa shisha wanachanganya bangi,
heroine na kokeni na ndio maana serikali ilipiga marufuku kuitumia.
Hata
hivyo, alisema sasa itajikita zaidi kuchunguza ili kubaini viambata
kiasi gani vilivyopo katika shisha na kwa nini serikali iendelee kupiga
marufuku matumizi ya shisha nchini.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )