Featured
Loading...

Jeshi la Zimbabwe: Tunawalenga Wahalifu Si Mugabe

 
Jeshi  la Zimbabwe limesoma taarifa kwenye kituo cha runinga cha serikali ZBC, likisema kuwa linachukua hatua ya kuwalenga wahalifu nchini humo.  Hata hivyo, limesema kuwa hayo si mapinduzi ya kijeshi na Rais Mugabe yuko salama.

Milio mikubwa ya risasi ilisikika katika maeneo ya kaskazini mwa mji mkuu Harare mapema jana.  Taarifa hiyo ya jeshi ilikuja saa kadhaa baada ya jeshi kudhibiti kituo cha utangazaji cha  ZBC. Grace Mugabe anaonekana kukaribia kukirithi kiti cha mumewe

Mwanamume mmoja ambaye alikuwa amevaa sare za jeshi alisema kuwa jeshi linataka kukabiliana na watu ambao wanatenda uhalifu unaoleta madhara ya kijamii na kiuchumi nchini Zimbabwe.

“Wakati tutakapomalizia wajibu wetu, tunatarajia kuwa hali itarudi kuwa kama kawaida.”

Taarifa hiyo ilisema kuwa Mugabe,  93, na familia yake wako salama.  Haijulikani ni nani anaongoza hatua hiyo ya kijeshi.  Magari ya wanajeshi waliojihami kwa silaha yalionekana maeneo ya mjini Harare.

Hali hiyo ya wasiwasi wa lolote kuweza kutokea, ilianza  jana jioni, ambapo wanajeshi wakiwa na silaha walionekana wakijipanga katika maeneo kadhaa  na kuzingira ofisi za shirika la utangazaji la Zimbabwe (ZBC).

Hata hivyo, taarifa zinasema kuwa wafanyakazi wa shirika hilo la utangazaji la ZBC, waliambiwa na wanajeshi hao kwamba hawapaswi kuwa na wasiwasi na kwamba uwepo wa vikosi hivyo ni kwa lengo la kulinda eneo hilo.

Chama tawala nchini Zimbabwe kimemtuhumu mkuu wa majeshi Constantino Chiwenga, kwa hatua yake ya madai kuwa jeshi lipo tayari kuingilia mzozo huo wa kisiasa kwa lengo la kulinda wapigania uhuru wa taifa hilo.

Hakuna kauli yoyote iliyotolewa na Rais Robert Mugabe kutokana na hali ya sasa nchini mwake.

Marekani imesema kuwa inafuatilia kwa karibu hali ya Zimbabwe na kutoa rai pande zote kutatua mzozo huo kwa njia ya amani.

Naye Balozi wa Marekani nchini Zimbabwe kupitia ukurasa wake wa Tiwtter amesema kuwa leo watasitisha shughuli za kiofisi ubalozini hapo kutokana na hali ya sasa mjini Harare.

Balozi wa Zimbabwe nchini Afrika Kusini, Isack Moyo, ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa serikali ipo imara katika jambo hilo na kuzuia uwezekano wowote wa kufanyika kwa mapinduzi.

Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
© Copyright MZALENDO HURU
Back To Top