Aliyekuwa
mwanachama CCM, ambaye baadaye alihamia Chadema, Lawrance Masha
amejivua uanachama katika chama hicho akidai upinzani wa sasa
umeridhika na hali ya kuendelea kuwa wakosoaji ili kukisaidia chama
tawala kujirekebisha.
Pia
amesema, “Nimejiridhisha pasipo shaka kuwa upinzani wa sasa nchini
hauna nia wala sababu ya kutafuta fursa ya kuunda Serikali kupitia
falsafa, sera na uongozi mbadala.”
Masha ameeleza hayo katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa leo Jumanne Novemba 14.
Masha
ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, katika Serikali
ya awamu nne, amesema upinzani hauwezi kutegemea kushika dola kwa
kutegemea madhaifu ya CCM badala uwezo wake kama mbadala.
Amesema
kazi kubwa ya chama chochote cha siasa ni kujiandaa na hatimaye
kushinda uchaguzi ili uweze kuunda na kuendesha Serikali na dola kama
njia ya maono yaliyo kwenye ilani ya uchaguzi kwa lengo la kuleta
maendeleo na ustawi katika nchi.
“Nilijivua
uanachama CCM mwaka 2015 na kujiunga Chadema nikiamini nitashiriki
kukifanya chama hiki kikomae na kufikia hatua ya kuwa mbadala kifalsafa,
kisera na uongozi. Hata hivyo uzoefu wangu wa miaka miwili ndani ya
Chadema umenionyesha chama hiki kina safari ndefu kisiasa na kuwa chama
mbadala cha kuunda Serikali.
“Mpaka
sasa chama hiki kimendelee kujikita katika kukosoa na kuonyesha
madhaifu ya Serikali hasa Rais John Magufuli binafsi. Natambua kwamba
kukosoa ni kazi muhimu ya chama cha upinzani, kazi hii haikifanyi chama
kuwa mbadala cha kuunda Serikali,”amesema Masha katika taarifa hiyo.
Masha
ambaye aliwani kuwa Mbunge wa Nyamagama mwaka 2005-10, amesema siyo
sahihi kwa vyama vya upinzani kuwekeza katika kumpinga Rais Magufuli
ambaye ni mkuu wa nchi pekee anayetekeleza kwa vitendo mambo ambayo
upinzani ilikuwa ikiyapigia kelele kwa miaka mingi, na kuwashinda
viongozi wa CCM waliomtangulia.
“Nimejivua
uanachama kuanzia leo, nina imani uamuzi huu utanipa fursa ya
kutafakari kwa kina safari yangu ya kisiasa ndani ya nchi hii.
Nawashukuru viongozi wa Chadema kwa miaka miwili ya kufanya kazi pamoja
nao nawatakiwa kila la kheri,” amesema Masha ambaye alikuwa ni miongoni
mwa watu walioshirikia kampeni za uchaguzi za mwaka 2015 kupitia Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )