Wakati
maswali mengi yakijitokeza kuhusiana na Dk. Louis Shika, ambaye
aliibuka mshindi katika mnada wa nyumba za kifahari za Said Lugumi
zilizoko Mbweni JKT na Upanga jijini Dar es Salaam kwa thamani ya jumla
ya Sh. bilioni 3.3, imebainika kuwa anaishi katika chumba kimoja cha
kupanga.
Imebainika
kuwa Dk. Shika anakaa kwenye nyumba hiyo iliyopo Mtaa wa Amani kwa
kipindi cha takribani mwaka mmoja sasa na kodi anayolipa kwa mwezi ni
takribani Sh. 50,000.
Aidha,
baadhi ya majirani zake wamemuelezea kuwa ni mtu asiye na makeke, huku
baadhi wakidai kuwa aliwahi kuwaahidi wauza mihogo ya kukaanga walio
jirani na mahala anapoishi kuwa atawaunganishia kupata mikopo nafuu ili
wakuze biashara zao, lakini bila ya kuwatajia taasisi atakayowaunganisha
nao. Inadaiwa kuwa vilevile, kwa baadhi ya watu hufahamika kwa jina la
‘profesa’.
Dk.
Shika alijipatia umaarufu katikati ya wiki baada ya kuibuka mshindi
katika mnada wa nyumba za kifahari za Lugumi, kwa kununua nyumba moja ya
Mbweni kwa Sh. bilioni 1.2, nyumba ya pili iliyoko pia Mbweni Sh.
milioni 900 na nyumba ya tatu iliyoko Upanga alishinda na kutaka kununua
kwa Sh. bilioni 1.2.
Hata
hivyo, alishindwa kutumiza masharti ya kulipa asilimia 25 ya fedha kwa
kila nyumba baada ya kushinda, hivyo kujikuta akitiwa mikononi mwa
vyombo vya dola kwa kuharibu mnada.
Katikati
ya wiki hii, jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, lilimtia
nguvuni Dk. Shika kutokana na tuhuma za kuharibu mnada huku likidai kuwa
linafanya uchunguzi zaidi ili kubaini kwa nini alifanya hivyo.
Mbali
na kuchunguza juu ya hatua ya kuharibu mnada, kamanda wa kanda Maalum
ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema walikwenda nyumbani kwake
kufanya upekuzi sambamba na kuchunguza udaktari wake. Shika aliwahi
kukaririwa kuwa ni msomi wa shahada ya uzamivu (Ph.D).
Hata
hivyo, Mambosasa alisema udaktari wake huo unatia shaka kwa kuwa
ameshindwa kuonyesha vielelezo kuthibitisha kama anastahili hadhi hiyo.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )