Viongozi
wa Taasisi ya Kusaidia Jamii ( TSSF) ambayo ilitangaza kuwa inatoa
mikopo ya elimu ya juu wamekamatwa na polisi baada ya kugundulika kuwa
ni matapeli.
Wakurugenzi
hao wamekamatwa jana Jumatatu jioni mara tu baada ya mkutano wa
waandishi wa habari na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,
William Ole Nasha wa kuelezea kuhusu uchunguzi uliofanyika baada ya
Mbunge wa Mafinga Mjini (CCM), Cosato Chumi kuomba mwongozo bungeni.
Chumi
alitaka ufafanuzi kuhusu uhalali wa taasisi hiyo baada ya kutangaza
kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa kulipa Sh 30 000 kama ada
ya maombi ya kusajiliwa kuomba mkopo.
Hata
hivyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako
amesema Serikali haitambui taasisi hiyo na kuahidi kufanya uchunguzi.
Akizungumza
leo Jumanne, Ole Nasha amesema baada ya uchunguzi huo wamebaini kuwa
taasisi hiyo haina uwezo wa kutoa mikopo kwa wanafunzi 50,000 ambao
ilitangaza kutoa.
Amesema
katika mahojiano na taasisi hiyo viongozi hao walisema kuwa fedha za
kuwakopesha wanafunzi hao watazipata kutoka nje ya nchi baada ya
kupeleka kiasi cha fedha.
Hata
hivyo, amesema mkataba wa taasisi hiyo na wafadhili hao unaonyesha kuwa
wamefikia makubaliano ya kufanya utafiti wa jinsi wanavyoweza kukusanya
fedha na si kuwapa fedha kwa ajili ya kutoa mikopo.
Amesema
tayari taasisi hiyo imekusanya fedha kwa wanafunzi 600 na imepeleka
wanafunzi 198 katika vyuo mbalimbali nchini kwa makubaliano ada zao
wangelipa Desemba mwaka huu.
Hata
hivyo, amesema hakuna uthibitisho kama wana fedha kweli za kuwalipia
wanafunzi hao ada ingawa wanadai kuwa katika akaunti zao za benki wana
fedha kati ya Sh 600 milioni na 700 milioni.
Amesema
kufuatia hilo wanaagiza vyombo vya dola kuchunguza jambo hilo na wakati
wakifanya hivyo ni marufuku kwa vyuo kuwapokea wanafunzi wanaopewa
mikopo na taasisi hiyo.
Pia
ameagiza akaunti zao zote kufungiwa hadi hapo watakapomaliza uchunguzi
sambamba na taasisi hiyo kutojihusisha na shughuli yoyote.
Baada
ya kumaliza mkutano huo polisi kutoka makao makuu ya polisi waliingia
ndani ya ukumbi wa mkutano na kuwaeleza wako chini ya ulinzi.
Polisi hao mmoja akiwa na sare na mwingine akiwa na nguo za kiraia waliwakamata na kuondoka nao.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )