Hussein Makame-NEC
Mwenyekiti
wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Semistolces Kaijage amevitaka
vyama vya siasa kufanya kampeni kwa kuzingatia maadili ya Uchaguzi.
Jaji
Kaijage ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa NEC na vyama vya
siasa uliofanyika jijini Dar es Salaam jana Novemba 13 kuelekea Uchaguzi
mdogo wa madiwani.
Alisema
iwapo ukiukwaji au uvunjaji wa Maadili hayo utatokea, Chama au Mgombea
awasilishe malalamiko hayo mbele ya Kamati husika ili ishughulikiwe
kisheria.
Aliwakumbusha
kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 53 cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za
Mitaa, Sura ya 292 Tume inayo mamlaka ya kuruhusu kuwepo kwa Kampeni za
Uchaguzi katika maeneo ya Uchaguzi na siyo Mikutano ya Vyama vya Siasa.
Hivyo,
kampeni hizo zifanyike kwenye Kata husika na inategemewa kuwa Mikutano
ya Kampeni italenga kuwashawishi, kwa namna ya kistaarabu, wananchi wa
Kata husika ili wamchague Mgombea anayefanyiwa kampeni.
”Kwa
mujibu wa kipengele cha 2.1. (c) cha Maadili ya Uchaguzi wa Rais,
Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015 tunategemea kila Chama cha Siasa
kiendelee kufanya Kampeni kwa mujibu wa ratiba. Kampeni zote zinatakiwa
kuanza saa 2:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni,” alisema Jaji Kaijage.
Aliongeza
kuwa kwa kuzingatia Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya
mwaka 2015, Tume imekwisha kutoa ushauri kwa Viongozi wa Mikoa na
Wilaya ili katika kipindi hiki cha Uchaguzi wahakikishe wanazingatia
wajibu wao na ukomo wa madaraka yao katika shughuli za Uchaguzi kuanzia
kipindi cha Kampeni hadi kutangazwa kwa Matokeo.
Naye
Mkurugenzi wa Uchaguzi kailima Ramadhani aliaviomba Vyama vya Siasa
kuwahimiza wanachama na wapenzi wao walioandikishwa kuwa Wapiga Kura
wajitokeze Siku ya Uchaguzi kwenda Kupiga Kura zao bila hofu yoyote
kuhusu usalama wao.
“Ni
imani ya Tume kuwa Viongozi wa Vyama vya Siasa mtakuwa chachu ya
kuwaongoza na kuwaelekeza wanachama, wafuasi na mashabiki wenu katika
kushiriki uchaguzi kwa amani na utulivu,” alisema Kailima.
Uchaguzi
Mdogo wa madiwani katika kata 43 za Tanzania Bara, unatarajiwa
kufanyika tarehe 26 Novemba, 2017 ambapo wapiga kura 333,309
wanategemewa kupiga kura siku ya uchaguzi huo.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )