Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na
Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni wamewaagiza
Mawaziri wa nchi hizi mbili kujadiliana juu ya namna ya kuongeza
biashara kati ya nchi hizi ili kupata manufaa makubwa zaidi ya uhusiano
na ushirikiano wa kidugu uliopo.
Viongozi
hao wametoa kauli hiyo jana tarehe 10 Novemba, 2017 baada ya kufanya
mazungumzo rasmi na kisha kuzungumza na waandishi wa habari katika Ikulu
ndogo ya Masaka nchini Uganda ambako Mhe. Rais Magufuli ameendelea na
ziara yake rasmi ya kiserikali ya siku 3.
Akisisitiza
juu ya agizo hilo Mhe. Rais Magufuli amesema kwa muda mrefu biashara
kati ya Tanzania na Uganda imekuwa ni takribani shilingi Bilioni 200 kwa
mwaka kiasi ambacho ni kidogo mno ikilinganishwa na fursa zilizopo,
uhusiano na ushirikiano wa kidugu uliojengwa tangu enzi za Baba wa Taifa
Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere.
“Tumewaagiza
Mawaziri na wataalamu wakae na waangalie vikwazo vyote vinavyosababisha
tufanye biashara kwa kiasi kidogo, wakishajadili watatuambia tufanye
nini, tunataka kuona biashara ya Tanzania na Uganda inakua, hivi sasa
Uganda imewekeza Dola za Marekani Milioni 47 tu nchini Tanzania na
kuzalisha ajira 146,000, kiasi hiki ni kidogo sana, ni lazima tuongeze”
amesema Mhe. Rais Magufuli.
Kuhusu
hatua ambazo Tanzania imeanza kuchukua Mhe. Rais Magufuli amesema
pamoja kuanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard
Gauge) kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma umbali wa kilometa 726, Serikali
imekarabati reli iliyopo, pamoja na kivuko cha mabehewa ya treni cha
Umoja katika ziwa Victoria ili kuwezesha mizigo ya kutoka bandari ya Dar
es Salaam kufika Kampala kwa gharama nafuu na pia inaendelea kujenga na
kuimarisha barabara za mpakani.
“Napenda
pia kukushukuru Mhe. Rais Museveni kwamba Serikali yako sasa itajenga
kipande cha kilometa 11 za reli kutoka Portbell hadi Kampala, na sisi
tumeamua kuweka bandari kavu pale Mwanza ili wafanyabiashara wa Uganda
wasisumbuke kwenda hadi Dar es Salaam, mizigo yao wataipata Mwanza, hii
ni njia ya uhakika na nafuu ya kusafirisha mizigo” ameongeza Mhe. Rais
Magufuli.
Akijibu
maswali ya waandishi wa habari Mhe. Rais Magufuli ameeleza kuwa
Tanzania imejipanga kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wake na
Uganda kwa kuhakikisha miradi mbalimbali inakwenda vizuri ikiwemo kituo
cha pamoja cha huduma za mpakani (One Stop Border Post – OSBP) na mradi
wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya
Tanga nchini Tanzania.
Kwa
upande wake Mhe. Rais Museveni amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa
juhudi kubwa anazozifanya kupambana na rushwa na kuimarisha uchumi, na
amemuagiza Waziri wake wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Monica Azuba Ntege
kuharakisha mchakato wa ujenzi wa kipande cha reli cha kilometa 11
kutoka bandari ya Portbell hadi Kampala ili usafirishaji wa mizigo kwa
njia ya reli kutoka bandari Dar es Salaam uanze mara moja.
Mhe.
Rais Museveni amesisitiza kukuzwa kwa biashara katika ya Tanzania na
Uganda hasa wakati huu ambapo Uganda inahitaji kununua gesi ya Tanzania
kwa ajili ya viwanda vyake vya mbolea na chuma na pia kurudisha historia
ambapo Uganda ilikuwa mnunuzi mkubwa wa bidhaa za Tanzania.
Kabla
ya kuzungumza na waandishi wa habari Marais wote wawili wameshuhudua
utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya Shirika la Utangazaji
Tanzania (TBC) na Shirika la Utangazaji wa Uganda (UBC) na makubaliano
kati ya Jeshi la Polisi la Tanzania na Jeshi la Polisi la Uganda.
Mhe. Rais Magufuli atamaliza ziara yake rasmi ya siku 3 kesho na kurejea nchini Tanzania.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Masaka, Uganda
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )