Na. Immaculate Makilika – MAELEZO
Serikali
ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, imefanya jitihada kadhaa ikiwa ni
sambamba na kutekeleza sera mbalimbali ambazo zimeiwezesha nchi ya
Tanzania kupata mafaniko makubwa ndani na nje ya nchi katika kipindi
cha miaka mitatu
Akizungumza
jana jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na
Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi, ametaja mambo 10 muhimu
yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli katika kipindi
cha miaka mitatu na ambayo yameitangaza nchi ya Tanzania kimataifa.
Dkt.
Abbasi alitaja mambo hayo kuwa ni uchumi unaoendelea kukua kwa kasi
nzuri, ambapo katika mwaka 2017/18 uchumi wa Tanzania ulikua kwa
wastani wa asilimia 7.1 na kuongoza katika nchi zote za Afrika
Mashariki, huku ukiingia katika rekodi ya kuwa miongoni mwa nchi ambazo
uchumi wake unakua kwa kasi zaidi duniani kama ambavyo ripoti
mbalimbali za kimataifa zimeeleza.
“Uchumi
wetu ni wa tisa kwa ukuaji wa kasi duniani na katika Afrika, Kusini mwa
Sahara ni wanne, hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya World Economic Forum
ya mwezi Machi, 2018 na kwa nchi za Afrika Mashariki uchumi wa
Tanzania unaongoza kwa ukuaji” alisema Dkt. Abbasi
Kuongezeka
kwa mapato ya Serikali katika kipindi cha miaka mitatu, Rais Magufuli
amethubutu kuziba mianya ya upotevu wa mapato na kuongeza kasi ya
kukusanya kodi na hivyo kuongeza mapato ya kodi ya Serikali kutoka
wastani wa shilingi bilioni 850 kwa mwezi hadi kufikia wastani wa
shilingi trilioni 1.3 kwa mwezi.
Kufufuliwa
kwa mashirika ya umma, Dkt. Abbasi alisema kuwa kutokana na
ufuatiliaji, ubunifu, uwekezaji wa Serikali ya Rais Magufuli, mashirika
mengi mfano Shirika la Mawasiliano Tanzania(TTCL), Shirika la Reli
Tanzania (TRC) na Mamkala ya Maji Safi (DAWASA) na Bandari sasa
yameanza kuamka kuwa na ufanisi, kuongeza mapato na mengine kutengeneza
faida.
“Baadaa
ya Serikali kuchagiza mageuzi ya kiutendaji sasa kwa mwaka TTCL
inakusanya shilingi bilioni 212 kutoka shilingi bilioni 102, Bandari
imekusanya kutoka shilingi bilioni 703 hadi kufikia shilingi bilioni 838
kwa mwaka, TRC kutoka shilingi bilioni 23 hadi 36 kwa mwaka na DAWASA
shilingi bilioni 32.4 hadi shilingi bilioni 122.4 kwa mwaka “ alisema
Dkt. Abbasi
Aidha,
Dkt. Abbasi alisema kuwa katika kipindi hiki cha miaka mitatu Serikali
ya Rais Magufuli imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika sekta ya viwanda
ambapo jumla ya viwanda 3,306 viliandikishwa, na vingine vinaendelea
kujengwa na baadhi vimekamilika. Halikadhalika viwanda hivyo vimeanza
kutengeneza bidhaa mbalimbali ambapo kati ya hivyo viwanda 251 ni
vikubwa na vya kati ni 173.
Ambapo
mchango wa ekta ya viwanda katika pato la Taifa umeongezeka kutoka
asilimia 5.2 mwaka 2015 hadi 5.5 mwaka 2017. Kasi ya ukuaji wa Sekta ya
Viwanda ilikua kutoka asilimia 6.5 mwaka 2015 hadi asilimia 7.1 mwaka
2017/18.
Akiendelea
kufafanua mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano Dkt. Abbasi alisema
kuwa Rais Magufuli amepambana na rushwa na ufisadi kwa pamoja na mambo
mengine, sambamba na kutimiza ahadi yake ya kuunda Makosa ya Uhujumu
Uchumi maarufu kama Mahakama ya Mafisadi
“Mpaka
sasa kesi mpya 41 zimefunguliwa, na kuna maombi ya dhamana 346
yamewasilishwa katika Mahakama hii kati ya mwaka 2017 na 2018” alisema
Msemaji huyo wa Serikali.
Katika
sekta ya usafirishaji nako, Serikali ya Rais Magufuli imefanya mageuzi
kadhaa, yaliyopelekea sekta hiyo kupata mafaniko ya kuwa na ndege nne
mpya zinazoendelea kuleta mageuzi katika usafiri wa anga nchini, abiria
wanaotumia ndege za ATCL wameongezeka kutoka takribani abiria 4,000 kwa
mwezi hadi abiria 30,000 kwa mwezi.
Aliongeza
kuwa ndege mbili aina ya Air Bus zenye uwezo wa kubeba abiria watu
132 zitawasili nchini Disemba mwaka huu, na ndege aina ya Boeing
dreamliner ya pili inatarajiwa kuwasili nchini Oktoba mwaka mwakani.
Aidha,
mradi wa umeme wa Stigler’s gorge utakapokamiika unatarajiwa kuzalisha
megawati 2,100, sambamba na mradi wa ujenzi wa reli kwa kiwango cha
standarg gauge kutoka Dar es salaam hadi Morogoro na baade Dodoma,
ambapo umefikia 33% ya ujenzi.
Mafaniko
mengine ya Serikali hii yanaonekana katika katika sekta ya afya,
ikiwemo kujenga vituo vya Afya vya Kata 210 na kukarabati vingine vingi
kufikisha idadi ya vituo vinavyotoa huduma hadi mwaka huu kuwa 7,746
kutoka vituo 7,014 mwaka 2014/15 sawa na ongezeko la asilimia 10.4.
Dkt.
Abbasi alifafanua kuwa vituo hivi pia vina wodi za kina mama na vifaa
vya kisasa. Aidha, ajira zaidi ya 6,000 za kada ya afya zimetolewa.
Katika miaka mitatu Zahanati zimeongezeka kutoka 6,143 mwaka 2015 hadi
6,646 mwaka huu ikiwa ni sawa na ongezeko la zahanati 503 ambapo
baadhi zilijengwa na zingine kukarabatiwa sawa na ongezeko la asilimia
8.1.
Vilevile,
Serikali ya Awamu ya Tano imefanya mageuzi ya kiutendaji ikiwemo
kuongeza Bajeti ya Dawa na Vifaa Tiba kutoka shilingi bilioni 31 mwaka
2015 hadi kufikia shilingi bilioni 270 kwa mwaka huu wa fedha.
Ongezeko
hilo limewezesha upatikanaji wa dawa muhimu katika vituo vya kutolea
huduma za afya nchini kufikia asilimia 89.6 kutoka asilimia 36 mwaka
2015/16. Aidha upatikanaji wa dawa muhimu umepanda kutoka wastani wa
asilimia 35 tu hadi asilimia 93.
Sekta
ya madini nayo, Dkt. Abbasi alisema kuwa “Serikali iliweka lengo la
kukusanya shilingi bilioni 1.5 kwa mwaka kutoka kwa wachimbaji wadogo wa
Tanzanite pale Mirerani. Hata hivyo kabla hata ya nusu ya mwaka huu wa
bajeti kufika, tayari mapato eneo la Tanzanite yamefikia shilingi
milioni 788.5 sawa na asilimia 52 ya lengo la mwaka 2018/19, hii
inashadidisha kuwa uamuzi wa Mhe. Rais kujenga ukuta ulikuwa makini”
alisema Dkt. Abbasi
Katika
miaka hii mitatu licha ya matukio ya hapa na pale, Tanzania imeendelea,
kusimama kama moja ya visiwa vya amani duniani na Taifa limeendelee
kushikamana kawa kuishi kwa amani na upendo.
Aidha,
Dkt, Abbasi alisema kuwa Rais Magufuli anasimamia misingi na
Watanzania leo wako huru kuamua mambo yao kama Taifa, huku akisisitiza
kuwa safari ya kujitegemea imeanza na mataifa mbalimbali duniani
yanafahamu azma ya Rais Magufuli kwa Taifa lake.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )