“Askari
lazima atishe. Popote anapokuwapo wahalifu wajue kuwa kuna mtu hatari
dhidi yao. Kama mhalifu atatiwa woga na uwepo wa polisi, uhalifu
utapungua tu na hivyo kubakiwa na kazi ndogo ya kuwakamata wachache
wanaoendelea na vitendo hivyo.” Omari Mahita
Inspekta
Jenerali wa Polisi (IGP) mstaafu, Omary Mahita amesema askari polisi
kwa sasa wamepoteza hadhi, hawaogopwi na wahalifu na ndiyo sababu kubwa
ya kuongezeka kwa vitendo vya kihalifu kila kukicha.
Mahita
aliyestaafu mwaka 2006, alisema mbali na kuongezeka kwa uhalifu,
inafikia hatua wahalifu wanawaingilia polisi kwa kuvamia vituo vya
polisi na kupora silaha ilhali zamani hakukuwa na matukio hayo.
Hata
hivyo, IGP, Ernest Mangu amejibu kauli hiyo akisema: “Siwezi kutumia
mbinu za Mahita kwa sababu alichokuwa anakabiliana nacho, kwa sasa
hakipo.”
Kauli ya Mahita
Kauli
ya Mahita imekuja miezi minane baada ya askari 10 kuuawa na bunduki
zaidi ya 20 kuporwa katika matukio mbalimbali ya uvamizi wa polisi na
vituo vya polisi.
Akizungumza
na mwandishi wetu baada ya kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa
Mkurugenzi wa zamani wa Mamlaka ya Hali ya Hewa, Dk Mohamed Mhita,
Oysterbay Dar es Salaam juzi, Mahita alisema: “Ili kupunguza vitendo vya
kihalifu vinavyozidi kuongezeka kila kukicha, ni lazima askari
warudishe hadhi yao ya kuogopwa na wahalifu popote walipo.
“Askari
lazima atishe. Popote anapokuwapo wahalifu wajue kuwa kuna mtu hatari
dhidi yao. Kama mhalifu atatiwa woga na uwepo wa polisi, uhalifu
utapungua tu na hivyo kubakiwa na kazi ndogo ya kuwakamata wachache
wanaoendelea na vitendo hivyo.”
Mahita
alikosoa kitendo cha askari polisi kuwa wapole na kueleza kuwa hilo ni
suala lisilotakiwa kabisa kufanywa ndani ya jeshi hilo na polisi...
“Unambembelezaje mhalifu? Hawa ni watu wanaostahili kubanwa kwa kila
namna ili kukomesha vitendo vyao katika jamii. Mhalifu yeyote akiachiwa,
madhara yake ni makubwa katika jamii.”
Licha
ya suala hilo, IGP huyo mstaafu alieleza umuhimu wa doria katika
kudhibiti uhalifu wa kila siku ambao hupunguza amani miongoni mwa jamii
na kuwafanya wananchi washindwe kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na
ratiba waliyojiwekea.
Alitolea
mfano wa vikundi vya uhalifu vilivyojitokea hivi karibuni kama ‘Panya
Road’, ‘Mbwamwitu’ na ‘Libya’ kwamba vimekuwapo kutokana na kupungua kwa
doria inayotakiwa ifanywe na jeshi hilo nchi nzima na hasa maeneo ya
mijini.
“Enzi
zangu doria ilipewa kipaumbele. Magari na pikipiki yalikuwa yanazunguka
kote katika jiji hili na kwingineko mikoani karibu kila siku na
walikuwa wanaogopeka… kwa sasa yapo lakini sidhani kama wanafanya kazi
kama ilivyokuwa enzi zile,” alisema Mahita.
“Wahalifu
walikuwa wanajua kuwa polisi wapo kazini muda wote. Lakini sasa hivi
mambo hayo hayapewi uzito unaotakiwa ndiyo maana unaona kikundi kama
Panya Road kinatingisha mji mkubwa kama huu (Dar es Salaam).
“Inawezekana vipi kikundi kama hicho kikatingisha amani ya jiji hili lenye viongozi wote wa jeshi?” alihoji Mahita.
Mahita
alikuwa maarufu kwa jina la ‘Ngunguri’ kutokana na kauli yake alipokuwa
akikabiliana na maandamano ya wafuasi wa CUF kwamba kama viongozi wake
wako ngangari basi polisi iko ngunguri kukabiliana nao.
Akizungumzia
uhalifu katika vituo vya polisi, Mahita alisema polisi imekosa kuungwa
mkono hivyo kupunguza ufanisi wake katika kutekeleza majukumu yake.
“Hata
jamii ipo mbali pia… Raia ndiyo wanavamia na kuua askari. Watu hawa
wanaishi katika jamii hiihii. Hivyo ni vyema ikajirudi na kuona kuwa hii
ni taasisi muhimu kwa maisha na mali ya kila mwananchi.”
Akizungumzia
vifo vya askari hao, Mahita alisema kuwa jamii imewasahau na kuwatenga
kwani hakuna anayeshtuka pindi wanapoteza maisha hata kama mauti hayo
huwakuta wakiwa kazini.
IGP Mangu
Akizungumzia hoja hizo, Mangu alisema mabadiliko ya jamii na maendeleo ya kiuchumi yamebadili mbinu za uhalifu.
“Mbinu
za kiuhalifu zimebadilika kiasi cha kulilazimu jeshi pia kubadilika ili
kuendana na mbinu hizo mpya. Haiwezekani jeshi likabaki kama ilivyokuwa
miaka 20 iliyopita.
“Jamii
ya wakati wa Mahita ni tofauti na ya sasa. Hata askari hawawezi
kuendelea kuwa wale waliokuwapo. Mazingira na kila kitu vimebadilika.
Enzi hizo kulikuwa na uhalifu wa ulipuaji wa mabomu na utakumbuka
ilishatokea huko Arusha na Zanzibar matukio ambayo hayapo kwa sasa,”
alisema Mangu. Alisema ni vigumu kulinganisha vipindi tofauti vya
viongozi na kwamba kufanya hivyo ni sawa na kutowatendea haki kwani
wanakuwa wanaongoza katika mazingira tofauti kwa kila kitu.
“Kubadilika
kwa mbinu na aina za uhalifu kunamlazimu kiongozi husika kuitikia
mabadiliko hayo pia. Mimi siwezi kutumia mbinu za Mahita kwa sababu
alichokuwa anakabiliana nacho hakipo sasa hivi.
Hapakuwa na mauaji ya albino wakati wake, hili peke yake linaonyesha jamii iliyopo ni tofauti na iliyokuwapo,” alisema.
“Hata
mimi nikistaafu baada ya Uchaguzi Mkuu Oktoba atakayekuja atapata
changamoto tofauti na hizi ninazokutana nazo au walizokutana nazo
watangulizi wangu,” alisema.
“Rais Kikwete alikemea mauaji ya polisi kila yanapofanywa... hivi ndivyo tunavyotakiwa kufanya,” alisema Mangu.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )