Rais
wa Jamuhuri ya Mungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli amekabidhi
gari la kubebea wagonjwa kwa hosipitali ya wilaya ya Chalinze, Ikiwa ni
utekelezaji wa ilani na ahadi ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi CCM
kwa wananchi ikiwa ni pamoja na wa jimbo la Chalinze.
Gari
hilo la kubebea wagonjwa limekabidhiwa kwa niaba ya Rais, na Katibu
Mkuu Ikulu Peter Ilomo kwa Mbunge wa Jimbo la Chalinze Mheshimiwa
Ridhiwani Kikwete Ikulu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
mara baada ya kukabidhi gari hilo, Katibu Mkuu Ikulu Ndugu Peter Ilomo
amesema gari hilo limetolewa na Mheshimiwa Rais kwa hosipitali hiyo
ikiwa ni kuitikia wito na utekelezaji wa ilani na ahadi ya uchaguzi ya
Chama Cha Mapinduzi CCM ya kuboresha huduma ya afya kwa wananchi wake
kote nchini.
Aidha,
Ndugu Ilomo amewaomba viongozi wa jimbo la Chalinze kulitumia gari hilo
kwa matumizi yaliyokusudiwa ya kuwahudumia wananchi wa eneo hilo.
Akipokea
gari hilo kwa niaba ya wananchi wa jimbo na Wilaya ya Chalinze, Mbunge
wa jimbo la Chalinze Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete amemshukuru
Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa msaada huo na kuahidi
kulitumia gari hilo kwa malengo yaliyokusudiwa, na kusema kuwa, utendaji
kazi wa Rais Magufuli umekuwa ukiungwa mkono na wananchi wa kada
mbalimbali na kuwaomba watanzania kuzidi kumuombea kwa Mungu.
Kwa
upande wake Dakta Nasoro Ally Matuzya, amesema gari hilo limekuja kwa
wakati muafaka kwa kuwa umezingatia utekelezaji wa malengo ya Milenia
hususan lengo namba nne linalosisitiza kupunguza vifo vya mama
wajawazito na watoto chini ya miaka mitano
Naye
Mwenyekiti wa Halmshauri ya Wilaya ya Chalinze Ndugu Saidi Omar
Zikatimu amesema gari hilo la kubebea wagonjwa litakuwa msaada mkubwa
kwa wananchi wa jimbo hilo la Chalinze hususan katika kusaidia kutoa
wagonjwa ambao wako katika maeneo ya vijijini wilayani humo na
kuwafikisha katika hospitali ya Chalinze na hivyo kunusuru maisha yao
kwa kupata huduma za afya kwa haraka.
Mbali
na Wilaya ya Chalinze kupata msaada wa gari hilo la kubebea wagonjwa,
tayari magari mengine mawili ya kubebea wagonjwa yameshakabidhiwa katika
vituo vya afya vya Kiroka na Kisemu mkoani Morogoro.
Hospitali
mpya ya Wilaya ya Chalinze imepanda hadhi kutoka kituo cha Msoga ambayo
ilikuwa haina gari la kubebea wagonjwa na hivyo kufanya usafirishaji wa
wagonjwa kutoka hospitali hiyo hadi hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Pwani
ya Tumbi au kutoka maeneo ya vijijini kuwa mgumu.
Imetolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )