VIGOGO
wawili raia wa Kichina, Huang Gin na Yu Fujie waliokamatwa mwaka 2013
wakituhumiwa kukutwa na meno ya tembo wamehukumiwa kwendea jela miaka 30
au kulipa shilingi Bilioni 54 kila mmoja.
Raia hao wamehukumiwa leo katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam chini ya Hakimu
Mkazi, Cyprian Mkeha ambapo kesi hiyo ilichukua muda wa zaidi ya saa 5
kusomwa huku upande wa serikali kupitia kwa Wakili wa Serikali
ukiongozwa na Faraja Nchimbi ambaye alikuwa na mawakili wengine ambao ni
Paul Kadushi,Wankyo Simon pamoja na Salim Msemo ambapo kwa upande wa
washitakiwa waliwakilishwa na Wakili Nehemiah Nkoko ambaye alijaribu
kutoa hoja zake ikiwemo kuiomba mahakama iwapunguzie adhabu.
Watuhumiwa wote walisomewa mashtaka
matatu ambayo ni kwanza, kukamatwa na nyara za serikali ambazo ni meno
ya tembo, shitaka la pili, kutumia pesa walizokutwa nazo katika upekuzi
kuwashawishi maofisa wa serikali ili wawaachie na shitaka la tatu,
kukutwa na ganda la risasi katika nyumba waliyokuwa wakiishi ambapo
shitaka hilo la tatu lilitupiwa mbali na kubaki mawili yaliyowatia
hatiani.
Akisoma vifungu vya sheria, Hakimu Mkeha
alisema kuwa watuhumiwa walikamatwa Novemba 2013 katika nyumba
waliyokuwa wamepanga iliyopo Mikocheni jijini Dar, wakiwa na vipande vya
meno ya tembo 728 ambapo ni sawa na tembo waliouawa 226 na kusema kuwa
waliisababishia serikali kupoteza fedha nyingi na kuingizwa katika kesi
ya uhujumu uchumi. Pia mahakama iliamuru magari yao matatu waliyokutwa
nayo kutaifishwa.
Mshitakiwa wa pili,Yu Fujie (kushoto) na Huang Gin wakiwa katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Wakiingizwa katika chumba cha mahakama na askari magereza.
Wakijuta baada ya kuhukumiwa.
Na Denis Mtima/Gpl
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )