Mkuu
wa Wilaya ya Butiama, Annarose Nyamubi ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Mkoa
wa Mara, juzi alimzuia Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mwigulu
Nchemba kwenda kijiji cha Mikomario wilayani Bunda kutatua mgogoro wa
ardhi kati ya wananchi na mwekezaji kwa madai ya wasiwasi wa usalama
kuwa mdogo.
Baada
ya jitihada zake za kumzuia kugonga mwamba, Nyamubi ambaye pia ni Kaimu
Mkuu wa Wilaya ya Bunda aliamua kujitenga na ziara hiyo kwani licha ya
kufika eneo la mkutano, hakujihusisha na lolote kwa kuamua kukaa
pembeni.
“Mheshimiwa
waziri nakushauri usiende Kijiji cha Mikomario kwa muda huu ambao
unakaribia usiku kwa sababu usalama utakuwa ni mdogo kutokana na ukorofi
wa wananchi wa eneo lile,” alishauri Nyamubi wakati akizungumza na Nchemba ofisini kwake.
Hata
hivyo, waziri Nchemba alisisitiza kuwa lazima aende kuzungumza na
wananchi hata kama atalazimika kuhutubia kwa kutumia taa za gari kwa
sababu aliwaahidi kuwa angefika na kuzungumza nao na walikuwa
wakimsubiri tangu mchana.
“Mheshimiwa
kaimu mkuu wa mkoa, bado sijashawishika kutotimiza ahadi ya kwenda
kuzungumza na wananchi wale, wamenisubiri tangu asubuhi na nimepata
taarifa wako uwanjani hadi jioni hii wakinusubiri. Kutokwenda ni
kutowatendea haki,” alisisitiza Nchemba.
Baada
ya msimamo huo, ndipo Nyamubi alipotangaza kujitoa kwa lolote ambalo
lingetokea, licha ya kuwamo kwenye msafara wa viongozi uliofika kijijini
hapo saa 12.40 jioni, hakukaa meza kuu wala kujishughulisha na lolote
hadi mkutano ulipomalizika kwa amani saa 1.10 usiku.
Akizungumza
na wakazi wa kijiji hicho ambacho kimekuwa na mgogoro wa ardhi kwa
miaka 30 sasa bila ufumbuzi, Waziri Nchemba aliahidi kuutafutia
ufumbuzi, lakini akawasihi kuwa na subira kwa sababu lazima awasiliane
na wizara nyingine zinazoguswa nao.
“Suala
hili ni la kisheria, hivyo linatakiwa kutatuliwa kisheria badala ya
mapigano, nipeni fursa ili wizara yangu iwasiliane na Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Tamisemi ili kwa pamoja
tuutafutia ufumbuzi.
“Wenye
mamlaka ya kupanga na hata kubadili matumizi ya ardhi ya kijiji ni
ninyi wananchi kupitia mikutano na Serikali yenu ya kijiji, viongozi na
wataalamu kazi yetu ni kutoa ushauri kuhakikisha uamuzi wenu unakuwa
halali,” alisema.
Wakiwa
na mabango yenye ujumbe, wakazi hao walimpongeza waziri kwa kutimiza
ahadi ya kuzungumza nao ili kutafutia ufumbuzi mgogoro huo unaohusu
hekta 2, 500 zinazodaiwa kutolewa kwa mwekezaji bila ridhaa ya Serikali
ya Kijiji.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )