DONALD Trump ameapishwa kuwa Rais wa 45 wa Marekani, na kurudia ahadi yake ya kuifanya nchi yake kuwa taifa lenye nguvu zaidi kuliko ilivyokuwa awali.
Hata
hivyo, Trump ameapishwa wakati ambao nchi hiyo imegawanyika, ambapo
jana maelfu ya wananchi waliandamana kupinga kuapishwa kwake. Kwa mujibu
wa uchunguzi wa maoni, ni asilimia 40 ya Wamarekani ndio wanamuunga
mkono.
Trump
aliapishwa huku idadi ya wageni walioalikwa kuhudhuria sherehe hizo
ikiwa ni nusu ya wale waliohudhuria wakati Rais aliyemaliza muda wake
jana, Barack Obama alipoapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2009.
Takribani
watu milioni 1.8 walihudhuria sherehe za kuapishwa kwa Obama wakiwamo
watu maarufu na wanamuziki, lakini mambo yashindwa kwenda sawa kwa Trump
kutokana na sherehe zake kuhudhuriwa na wageni takribani 800,000.
Jana
Polisi walipambana na kundi kubwa la wananchi waliokuwa wakiandamana na
kuziba mitaa na barabara za majimbo mbalimbali nchini humo wakipinga
kuapishwa kwa Trump kuwa rais wa nchi hiyo.
Trump
ambaye alimshinda mpinzani wake wa Chama cha Democratic, Hillary
Clinton katika uchaguzi mkuu uliofanyika Novemba 8 mwaka jana, amekuwa
akipingwa na kundi kubwa la raia wa nchi hiyo ambao wanasema hakuwa
chaguo lao bali alishinda kutokana na mfumo mbovu wa upigaji kura
unaotumiwa na Taifa hilo.
“Tutaandamana tu wala hatutaogopa kama Polisi watatupiga au kutukamata, lengo ni kumwonesha Trump kwamba hakubaliki miongoni mwa raia wengi wa Marekani, haijalishi ameshinda na anaapishwa, katu hatopata nafasi nyoyoni mwetu.
“Hajawahi kuwa na sera zinazoonesha kama ni kiongozi wa kutazamwa, kauli zake za kibaguzi kuanzia rangi na wanawake vinamfanya kuwa Rais wa ajabu kuwahi kutokea Marekani,” alisema mmoja wa waandamanaji katika eneo la San Diego, California.
Democrats
Sherehe hiyo iligubikwa na mabadiliko mengi mahsusi tofauti na ilivyozoeleka kwa watangulizi wake.
Jambo
kubwa mbali na maandamano hayo yaliyoendeshwa na wafuasi wa chama cha
Democrats, ni uchaguzi wa Trump wa Biblia ambayo alitumia kuapia, kwani
alichagua aliyotumia utotoni, lakini pia kiutaratibu alitumia Biblia ya
Lincoln ambayo ilitumiwa katika viapo vitatu vilivyotangulia.
Biblia hiyo ilitumiwa na Abraham Lincoln mwaka 1861 na Barack Obama mwaka 2009 na mwaka 2013.
Tofauti
na viapo vya nyuma, idadi ya waburudishaji haikuwekwa wazi kutokana na
wengi waliokuwa wamejulishwa kushiriki walijijitoa kutokana na upinzani
wa kisiasa uliogubika sherehe hizo.
Mmoja
wa waburudishaji waliothibitishwa tangu awali ni Jackie Evanco (16)
ambaye ni maarufu kwa albamu yake ya ‘America’s Got Talent’ na ndiye
aliyeimba Wimbo wa Taifa.
Jambo
lingine lisilo la kawaida ni idadi kubwa ya wajumbe wa Baraza la
Congress wa Democrats ambao walitangaza kususa hafla hiyo, huku idadi
ikionesha kuwa theluthi tatu ya wajumbe wote wa Baraza hilo kutoka
Democrats hawakushiriki.
Hata
hivyo ratiba ya matukio ya jana haikutofautiana sana na ilivyozoeleka
katika viapo vilivyotangulia vya marais, hata hivyo, Trump ambaye
alilala na familia yake kwenye jengo la Blair House mkabala na Ikulu ya
White House, alianzia kanisani asubuhi.
Baadaye
akifuatana na mkewe, Melania, walikwenda White House kufungua kinywa
pamoja na familia ya Rais Barack Obama kabla ya kwenda Capitol.
Baada
ya kiapo, Obama aliondoka na kumwacha Trump akipata chakula cha mchana
kabla ya matukio mengine kama vile gwaride na shamrashamra zingine ili
kuhitimisha siku hiyo.
Wapinzani
Wapinzani wa Trump usiku wa kuamkia jana walipambana na polisi na kunyunyiziwa pilipili jijini hapa.
Kundi
kubwa la waandamanaji wanaompinga Rais Trump lilikusanyika mapema nje
ya Klabu ya Taifa ya Waandishi wa Habari, ambako kulikuwa na sherehe
zijulikanazo kama ‘DeploraBall’ – tukio ambalo liliandaliwa na wafuasi
wa Trump juzi usiku.
Mamia ya waandamanaji hao waliingia mitaani nje ya klabu hiyo, wengi wakiimba huku wakibeba mabango ya kumkataa Trump.
Mmoja
wa wafuasi wa Trump ambaye alikuwa eneo hilo lakini hakuhudhuria hafla
hiyo, alidai kuwa waandamanaji hao walifanya vurugu – wakimshutumu mmoja
wao kwa kumshambulia kwa mlingoti wa bendera.
“Nilikuwa nimevalia kofia yangu yenye maandishi ya ‘Ifanye Marekani Taifa Kubwa tena’, na mwanamume mweupe akanifuata kwa nyuma na kunisukasuka kwa mlingoti wa bendera – nikapoteza fahamu kama dakika moja hivi,” Jones Allsup (21) aliiambia Fox News.
Wafuasi
Kambi
ya Trump kwenye ghasia hizo nayo iliwakilishwa na waendesha mapikipiki
waliotoka sehemu mbalimbali za nchi kuja hapa siku kadhaa kabla ya jana
ambao walijiandaa kukabiliana na waandamanaji hao.
Kundi
hilo linalojiita Bikers For Trump liliomba kibali cha watu 5,000 kukaa
kwenye bustani ya John Marshall, huku wakipanga kufanya mkutano usio
rasmi kati ya tukio la kula kiapo na kuanza kwa gwaride.
Muasisi wa kundi hilo, Chris Cox (48), aliiambia Fox & Friends: “Kwenye tukio hili ambalo tunahitajika, tutajenga ukuta wa nyama. Tutakuwa bega kwa bega na ndugu zetu na tutakuwa kidole kwa kidole na yeyote atakayethubutu kuvuka vizuizi vya Polisi,” alionya Cox.
Kabla
ya kuapishwa Trump na Makamu wake, Mike Pence na familia zao
walihudhuria ibada kwenye Kanisa la Mt John baadaye wakaenda Ikulu ya
White House kufungua kinywa na familia ya Rais Barack
Obama
kabla ya kuelekea jengo la Capitol, kuapishwa na Jaji Mkuu, John
Roberts Jr na kuhudhuriwa na wabunge wa Baraza la Congress.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )