TANZANIA imetajwa kuwa miongoni mwa nchi 20 bora duniani kwa kuwa na
sehemu kubwa ya mawaziri wanawake kwenye Baraza la Mawaziri, huku
ikishika nafasi ya tano Afrika.
Mtandao wa How Africa, The Rise of Africa, umeeleza hilo jana ukinukuu utafiti mpya ulioandaliwa na taasisi ya UN Women na Inter Parliamentary Union, ambazo zinaongoza duniani kwa kupigania ajenda ya kuongeza uwakilishi wa wanawake kwenye vyombo vya uamuzi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Cape Verde ndiyo nchi inayoongoza kwa kuwa na sehemu kubwa ya wanawake kwenye Baraza la Mawaziri, inayoundwa na wanawake ambalo kati ya mawaziri wote 17, tisa ni wanawake.
Mbali na kuwa ya kwanza Afrika, Cape Verde imetajwa kuwa ya pili duniani kwa kigezo hicho, ikitanguliwa na Finland, ambayo ndiyo ya kwanza duniani kwani kati ya mawaziri wake 16, mawaziri 10 ni wanawake.
Nchi ya pili Afrika kwa kuwa na sehemu kubwa ya wanawake kwenye Baraza la Mawaziri ni Afrika Kusini, ambayo kati ya mawaziri 36, mawaziri 15 ni wanawake.
Rwanda inashika nafasi ya tatu Afrika, kwani kati ya mawaziri wake 31, mawaziri 11 ni wanawake na inafuatiwa na Burundi na Tanzania katika nafasi ya tano.
Tanzania
Baraza la Mawaziri Tanzania likijumuisha na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, lina mawaziri 36 na kati yao, tisa ni wanawake.
Mawaziri hao ni Jenista Mhagama (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu); Ummy Mwalimu (Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto); Anjela Kairuki (Utumishi na Utawala Bora); Profesa Joyce Ndalichako (Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi).
Wengine ni Dk Ashantu Kijaji (Naibu Fedha na Mipango); Dk Susan Kolimba (Naibu Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afika Mashariki); Angelina Mabula (Naibu Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi); Stella Manyanya (Naibu Elimu, Sayansi Teknolojia na Ufundi) na Anastasia Wambura (Naibu Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo).
Nchi zingine
Afrika sasa ina nchi saba ambazo angalau asilimia 30 ya mawaziri wao ni wanawake na katika nchi 30 duniani zinazofikia wingi huo wa mawaziri wanawake na kuzidi, robo ya nchi hizo zinatoka Afrika na kufanya Bara hilo kuwa la pili kwa kufikia kigezo hicho baada ya Ulaya.
Nchi yenye uchumi mkubwa zaidi Afrika; Nigeria kati ya mawaziri 29, saba ni wanawake uwiano sawa na Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambayo kati ya mawaziri 22, watano ni wanawake.
Djibouti ndiyo ya mwisho, ambayo kati ya mawaziri wake 19, waziri mmoja tu ndiye mwanamke, wakati Sierra Leone ina mawaziri wanawake wawili tu kati ya mawaziri 29.
Bungeni
Rwanda inaongoza duniani katika uwakilishi wa wanawake bungeni ambapo kati ya viti 80 vya ubunge, viti 51 ni vya wanawake sawa na asilimia 63 ya wabunge wote.
Ushelisheli, Senegal na Afrika Kusini zinafuata na kuwa miongoni mwa nchi 10 bora duniani kwa kuwa na uwakilishi mkubwa wa wanawake bungeni.
Msumbiji, Angola, Tanzania, Algeria, Zimbabwe, Tunisia, Kameruni na Burundi, ni miongoni mwa nchi zingine za Afrika, zenye zaidi ya asilimia 30 ya wabunge wanawake kwenye mabunge yao.
Nchi zenye uwakilishi mbovu wa wanawake bungeni ni Swaziland, Nigeria, Congo zote mbili, Ivory Coast, Gambia, Mali na Botswana, ambazo uwakilishi wa wanawake kwenye mabunge yao ni chini ya asilimia 10.
Wastani wa uwakilishi wa wanawake kwenye mabunge ya nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, umetajwa kuwa asilimia 22.4 katika mataifa yenye mabunge yenye sehemu moja na asilimia 20 kwa mabunge yenye sehemu mbili; Bunge la Wawakilishi na Bunge la Seneti
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )