Aliyekuwa
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk.
Willibrod Slaa, ameajiriwa katika duka kubwa la bidhaa za majumbani
(Supermarket) la Costco lililopo Oakville, Toronto nchini Canada,
imebainika.
Dk. Slaa, kwa sasa anaishi nchini Canada alikokwenda kwa masomo, tangu alipotangaza kuachana na siasa Septemba 1, mwaka 2015.
Kwa
muda wa wiki kadhaa, ziliibuka taarifa katika mitandao ya kijamii kuwa
mbunge huyo wa zamani wa Karatu, amemaliza masomo yake na sasa anafanya
kazi katika moja ya maduka makubwa ya bidhaa mbalimbali nchini humo –
Supermarket.
Supermarket
ya Costco anayofanya kazi Dk. Slaa akihudumu kama Mshauri wa Mauzo
(Sales Advisor), akilipwa Dola za Marekani 10 (zaidi ya Sh 20,000) kwa
saa, ina hadhi kama Nakumat, Shopers, Imalaseko, Game na maduka mengine
makubwa nchini.
Akizungumza
na Gazeti la Mtanzania jana kwa simu , Dk. Slaa alisema kuwa kwa sasa
anaishi kwa kazi ya mikono yake kwani ili aweze kuishi anahitaji
kufanya kazi zaidi ya mbili hadi nne kwa siku.
“Niko,
ninafuatilia matukio Mutukula (ziara ya Rais Dk. John Magufuli jana).
Siku zote nimesema ninaishi kwa jasho na kazi ya mikono yangu. Canada
ili uishi vizuri, unahitaji kazi zaidi ya mbili au tatu mpaka nne. Hayo
nimeweka wazi, sijui jambo jipya kama mtu alikuwa hafuatilii.
“Mimi
ninafanya kazi PWD/CDS/COSTCO kama Sales Advisor, baada ya kumaliza
masomo yangu hasa Interpersonal Communication. Costco ninakofanya kazi
ina members (wanachama) 10,000. Kwa siku wanaofika Warehouse ni kati ya
5,000 hadi 7,000,” alisema Dk. Slaa.
Mbali na hilo, alisema kuwa pia anafanya kazi nyingine ikiwa ni pamoja na ushauri (Consultancy).
Alisema
kila mara amekuwa akiwataka Watanzania na vijana wafanye kazi kwani
fedha haziji kwa kukesha kwenye mtandao wala propaganda.
“Canada
ni kazi, Profesa wa Chuo Kikuu anafanya kazi ya Uber. Sijui kama Uber
inafahamika Tanzania, ni dereva Taxi kwa kutumia gari lake binafsi.
Ofisa wa Serikali usiku anaosha vyombo hotelini.
“Ndiyo
maana familia ina magari mawili au zaidi, TV, nyumba ya kisasa, chakula
cha kisasa. Wanatekeleza sera ya ‘Hapa Kazi Tu’ kwa matendo. Nadhani
nimekupa taarifa za kutosha ikiwa ni pamoja na kujibu propaganda kuwa
nilihongwa mabilioni.
“Niwahakikishie
tena, wakati wa kusoma nilikuwa na scholarship, tangu nianze kazi
ninaishi kwa jasho la mikono yangu. Mke wangu yeye ameingia Chuo Kikuu
cha York baada ya Diploma yake na bado anapata scholarship.
“Ndiyo
maana tuna uwezo wa kuwa na magari mawili aina ya Jeep na Dodge,
ukifanya kazi utaishi vizuri. Hii ni pamoja na kugharamiwa bima ya afya
(Health Insurance), watoto kusomeshwa na Serikali ya Canada,” alisema
Dk. Slaa.
Mei
mwaka huu, Dk. Slaa, alisema hana mpango wa kurudi nchini kwa sasa na
kwamba taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii hazina ukweli
wowote.
Hata
hivyo, Dk. Slaa ambaye alipata kuwa Mbunge wa Karatu kwa vipindi vitatu
mfululizo, hakuweza kuainisha mazingira yaliyomfanya aondoke nchini na
kwenda kuishi ughaibuni.
Septemba,
2015 wakati wa Uchaguzi Mkuu, Dk. Slaa alijiweka kando na siasa, kwa
kile alichokieleza kutofautiana na viongozi wenzake ndani ya chama chake
juu ya masharti ya kumpokea aliyekuwa mgombea urais wa Umoja wa Katiba
ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa.
“Sina
tabia ya kuyumbishwaa, sina chuki na mtu yeyote, sipendi siasa za
udanganyifu na propaganda. Nimeachana na siasa tangu Julai 28, 2015,
baada ya kuona misingi ya chama nilichoshiriki kukijenga imepotoshwa,”
alisema Dk. Slaa siku alipotangaza kuachana na siasa.
Alisema
sharti la kwanza ambalo alitaka Chadema izingatie, ni kiongozi huyo wa
zamani ndani ya Serikali ya CCM, kujisafisha dhidi ya tuhuma ya kashfa
ya sakata la Kampuni ya Kufua Umeme ya Richmond aliyohusishwa nayo akiwa
Waziri Mkuu.
Credit: Mtanzania
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )