Wadau
wa sanaa ya filamu nchini masikio yao leo yatakuwa katika Mahakama Kuu
ambako kutakuwa na tukio kubwa katika tasnia hiyo wakati itakapotolewa
hukumu ya kesi inayomkabili mwigizaji maarufu nchini, Elizabeth Michael
maarufu kama Lulu.
Lulu
anakabiliwa na kesi ya kumuua mpenzi wake Steven Kanumba bila
kukusudia, kinyume cha kifungu cha 195 cha kanuni za adhabu (PC), Aprili
7, 2012, Sinza Vatican jijini Dar es Salaam kufuatia ugomvi wa
kimapenzi ulioibuka baina yao.
Hapana
shaka kuwa hii ni hukumu ambayo inasubiriwa kwa hamu na wadau wa
sheria, sanaa ya uigizaji, wapenzi wa filamu, ndugu, jamaa na marafiki
wa mshtakiwa huyo na wa marehemu Kanumba na hata jamii kwa jumla.
Hii
inatokana na ukweli kwamba ni moja ya kesi zilizovuta hisia za makundi
yote katika jamii tangu kutokea kwa tukio hilo, kushtakiwa kwa msanii
huyo, jinsi jamii ilivyokuwa ikifuatilia mwenendo wa kesi pamoja na
kuibua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya jamii na hata vijiweni.
Wakati
upande wa mashtaka ukidai kuwa Lulu alimuua Kanumba bila kukusudia,
Lulu mwenyewe mara zote amekuwa akikana mashtaka hayo akidai kuwa
hahusiki kwa vyovyote na kifo cha mpenzi wake huyo.
Hata
hivyo, mvutano huo baina ya mshtakiwa huyo na upande wa mashtaka
unatarajiwa kuhitimishwa leo na Jaji Sam Rumanyika aliyekuwa anasikiliza
kesi hiyo.
Kama
ilivyo ada kwa kesi yoyote, kila upande yaani upande wa mashtaka na wa
utetezi (mshtakiwa) utakuwa unatarajiwa moja kati ya mambo mawili;
mshakiwa kutiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu au kuachiwa huru.
Hivyo
ndivyo inavyotarajiwa kutokea pia kwa hukumu ya msanii huyo
itakaposomwa na Jaji Rumanyika na kama mshtakiwa atatiwa hatiani na
kuhukumiwa kifungo au atabaki uraiani kuendelea na maisha kama kawaida,
iwapo mahakama haitamtia hatiani.
Kwa
vyovyote itakavyokuwa matokeo ya hukumu hiyo yatakuwa na uzito wa pekee
kwa msanii huyo kwani ndiyo itakayotoa mustakabali wa maisha yake.
Hii
ina maana kwamba iwapo apatikana na hatia, basi atakabiliwa na adhabu,
jambo ambalo litabadili historia na mustakabali wa maisha yake kwa
jumla, ingawa inategemeana na adhabu atakayopewa.
Lakini
iwapo atashinda kesi hiyo, basi yeye ndiye atakayekuwa na furaha kubwa
kwa kuwa atakuwa ameepuka adhabu, na hivyo kuendelea na maisha akiwa
huru.
Kwa hiyo, wakati wa hukumu hiyo Jaji Rumanyika anatarajiwa ama kumtia hatiani na kumhukumu adhabu au kumwachia huru.
Katika
kufanya hivyo, jaji huyo atazingatia ushahidi uliotolewa mahakamani
hapo na mashahidi wa pande zote, yaani upande wa mashtaka na upande wa
utetezi pamoja na vielelezo mbalimbali.
Mbali
na ushahidi huo na vielelezo vyake, pia Jaji Rumanyika atazingatia
sheria zinazoongoza kesi za namna hiyo pamoja na uamuzi wa kesi
mbalimbali zilizowahi kuamuliwa zenye mashtaka na hata mazingira
yanayofafana nayo.
Katika
kesi hasa za mauaji ama ya kukusudia au ya bila kukusudia huwa kuna
ushahidi wa aina mbili. Mosi ni ushahidi wa moja kwa moja, yaani
ushahidi wa kushuhudia tukio.
Pili,
ni ushahidi wa kimazingira. Huu ni ushahidi ambao hakuna shahidi
aliyeshuhudia moja kwa moja tukio likitokea, bali mshtakiwa huhusishwa
na tukio kulingana na mazingira yaliyokuwapo kabla au wakati wa tukio
husika.
Katika
kesi ya Lulu, kwa mujibu wa Jaji Rumanyika, upande wa mashtaka
umeegemea kwenye aina hii ya pili ya ushahidi wa mazingira, kwani kati
ya mashahidi wanne wa upande huo hakuna hata mmoja aliyeshuhudia tukio
hilo.
Ushahidi
wa upande wa mashtaka unasema Kanumba alifariki dunia kutokana na
tatizo la mtikisiko wa ubongo lijulikanalo kwa kitaalamu kama brain
concussion, lililosababisha mfumo wa upumuaji kushindwa kufanya kazi
baada ya kujibamiza ukutani upande wa kisogoni.
Hivyo
upande wa mashtaka unadai kuwa mshtakiwa ndiye aliyesababisha Kanumba
kujibamiza ukutani (ukimaanisha kuwa alimsukuma) na hivyo kupata tatizo
lililosababisha kifo chake.
Hata
hivyo, hakuna shahidi hata mmoja aliyeieleza mahakama kuwa alishudia
mshtakiwa akifanya jambo ambalo lilisababisha kifo cha Kanumba, badala
yake kuna ushahidi wa kusikia sauti za ugomvi baina ya Lulu na Kanumba
chumbani mwa Kanumba.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )