Bodi
ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza orodha
nyingine yenye wanafunzi 1,775 wa Mwaka wa Kwanza waliofanikiwa kupata
mikopo na hivyo kufanya jumla ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza
waliopangiwa mikopo hadi sasa kufikia 31,353.
Katika Awamu ya Kwanza, wanafunzi 10,196 wa mwaka wa kwanza walipangiwa mikopo, Awamu ya Pili (11,481), Awamu ya Tatu (7,901).
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa jana (Jumapili, Novemba 12, 2017) na
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru, orodha kamili ya
wanafunzi hao inapatikana katika tovuti ya Bodi (www.heslb.go.tz) na pia imetumwa kwa vyuo husika jana ili kuwawezesha wanafunzi kufanya usajili na kuendelea na masomo.
“Tumekua
tukifanyia kazi orodha za udahili ambazo tumekuwa tukipokea, na kila
tunapokamilisha, tunatoa orodha za wanafunzi waliopangiwa mikopo ambao
wana sifa – leo tumetoa hao 1,775,” alisema Bw. Badru.
Bw.
Badru, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari pia alikumbusha kuwa
kiasi cha shilingi 427.54 bilioni zimetengwa kwa ajili ya mikopo ya
wanafunzi kwa mwaka 2017/2018 na tayari Serikali imeshatoa shilingi
147.06 bilioni kwa ajili ya robo ya kwanza ya mwaka huu wa 2017/2018.
Fedha hizo, shilingi 427.54, ni kwa ajili ya jumla ya wanafunzi 122,623 wa mwaka wa kwanza na wale wanaoendelea na masomo.
Wakati
huohuo, HESLB imetangaza kufungua dirisha la rufaa kuanzia kesho,
Jumatatu, Novemba 13, 2017 hadi Novemba 19, 2017 ili kuwapa fursa
waombaji wote ambao hawajaridhika na upangaji wa mikopo kuwasilisha
rufaa kupitia vyuo walivyopata udahili.
Kwa
mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji huyo wa HESLB, lengo la HESLB ni
kuhakikisha wanatangaza orodha ya majina ya waombaji mikopo
waliofanikiwa katika rufaa zao ifikapo au kabla ya tarehe 30 Novemba
mwaka huu.
“Tunatoa
wito kwa uongozi wa vyuo vyote kupokea maombi ya rufaa za wanafuzi na
kuwasilisha kwa Bodi ya Mikopo kabla ya Novemba 22, 2017 ili kuiwezesha
Bodi kutoa orodha ya waombaji waliofanikiwa katika rufaa zao ifikapo
Novemba 30, 2017,” alisema Bw. Badru katika taarifa yake.
Maelezo ya kina kuhusu utaratibu wa kuwasilisha rufaa yatatolewa kupitia tovuti ya Bodi (www.heslb.go.tz).
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )