Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, DODOMA
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Mhe. Seleman Jafo amezindua kampeni ya
“Mkoa wetu, Viwanda vyetu” yenye lengo la kuanzisha viwanda 100 katika
kila Mkoa nchini, jana Mjini Dodoma.
Akizungumza
katika uzinduzi huo Mhe. Jafo alisema kuwa ni jambo lililowazi kuwa ili
nchi iweze kuendelea inahitaji kufanya mapinduzi makubwa katika
viwanda.
“Historia
ya Viwanda siyo ngeni katika nchi yetu, tangu tupate Uhuru mwaka 1961
Serikali imekuwa ikilenga katika kujenga Uchumi kupitia Viwanda ambapo
tokea wakati huo viwanda vingi vidogo vya kati na vikubwa vilianzishwa
na kusimamiwa huku sehemu kubwa ya viwanda hivyo vikisimamiwa na
Serikali” alieleza Mhe. Jafo.
Aidha
alisema kuwa ili azma hiyo iweze kufikiwa TAMISEMI itashirikiana na
Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji katika kuweka mazingira wezeshi
pamoja na kutoa mwongozo wa namna ya kushirikisha Tasisi za Serikali na
Sekta Binafsi na wadau wa maendeleo katika kuanzisha, kuendesha na
kusimamia Viwanda ili kuikuza sekta hiyo nchini.
“TAMISEMI
kupitia Mikoa na Halmashauri imedhamiria kutekeleza kwa vitendo azma ya
Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga Uchumi wa Viwanda, hivyo kila Mkoa
uanishe Viwanda vya vipaumbele kwa kuzingatia Malighafi muhimu za
Viwanda zinazopatikana kwenye maeneo yao pamoja na mahitaji muhimu ya
soko” alifafanua Mhe. Jafo.
Hata
hivyo, Mhe. Jafo aliwataka Wakuu wa Mikoa, wakuu wa Wilaya na
Halmashauri kuwatumia ipasavyo Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa
Ugani ili kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa
uchumi wa viwanda nchini.
Kwa
upande wake, Naibu Waziri Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhandisi
Stella Manyanya alisema kuwa Wizara yake itaendelea kuweka mazingira
wezeshi ikiwa ni pamoja na kuanza kujenga majengo maalumu kwa ajili ya
uendelezaji viwanda katika Ofisi zote za SIDO Mikoani.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )