Serikali
imemjia juu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kutokana na
kauli yake kuwa Rais John Magufuli amekuwa akipendelea baadhi ya kanda
katika uteuzi wake.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Watu wenye
Ulemavu, Jenister Mhagama jana Jumatatu jioni alisema Mbowe anapotosha
na kumtaka aache kuingilia madaraka ya Rais.
Wakati
akichangia Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa 2018/2019, Ijumaa iliyopita
Mbowe alienda mbali na kudai anaweza kuleta uthibitisho kama Bunge
litamkata kufanya hivyo.
“Mumwambie
bwana mkubwa unapoamua mambo mengine tenda haki pande zote. Lakini
unapokuwa haki hiyo unaipeleka mahali fulani na unakandamiza upande
mmoja unawanyima haki”
Mbowe
alitolea mfano wa teuzi mbalimbali alizozifanya Rais Magufuli tangu
aingie madarakani mwaka 2015, akisema hazikugawanywa kwa usawa wa mikoa
kama utamaduni uliokuwepo awamu zilizopita.
Hata
hivyo, jana Jumatatu jioni Jenister amesema Ibara ya 36 (1) (2)(3)(4)
imempa Rais madaraka ya kuanzisha na kufuta ya nafasi za mbalimbali kwa
utumishi na haijasema atazingatiwa usawa wa kanda.
“Ibara
hiyo haisemi kuwa Rais wakati atakapokuwa anafanya uteuzi eti aangalie
ukanda. Haisemi hivyo Ibara hiyo haisemi anavyoandaa uteuzi aaangalie
makabila mbalimbali,”alisema Mhagama.
“Unasimamaje
ndani ya Bunge kuhoji madaraka ambayo Rais amepewa kwa mujibu wa
Katiba? Alihoji Mhagama na kutoa mifano ya teuzi tatu zilizofanywa na
Rais kutoka mikoa ya Kaskazini.
“Ameteuliwa
Aggrey Mwandry kutoka Siha kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora na anafanya kazi
vizuri sana. Ameteuliwa Alexander Mnyeti kuwa Mkuu wa Mkoa wa
Manyara,”alisema na kuongeza
“Ameteuliwa
Anna Kilango kutoka Same. Nina orodha ndefu lakini uteuzi huo unafuata
madaraka ya kikatiba. Niwaombe sana wabunge tusiingile madaraka ya Rais
aliyopewa kwa mujibu wa Katiba.”
Alisema
Rais amekuwa akifanya teuzi mbalimbali kwa utashi wa hali ya juu na
anateua watu wa kubeba dhamana ya kumsaidia kuongoza kwa niaba yake
pasipo upendeleo.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )