Spika
wa Bunge, Job Ndugai amewaonya mawaziri kuacha kupiga stori wanapokuwa
bungeni, badala yake wawe makini kusikiliza mijadala na maswali kutoka
kwa wabunge.
Ndugai
alitoa onyo hilo jana katika kipindi cha maswali na majibu baada ya
kuwataja baadhi ya manaibu ili wajibu maswali lakini walishindwa
kusimama kwa kuonyesha hawakusikiliza kilichokuwa kimeulizwa na wabunge.
“Waheshimiwa
mawaziri acheni kupiga stori ndani ya Bunge, ndiyo maana mnashindwa
kusikiliza kinachoendelea humu, hebu punguzeni na mjikite katika
kusikiliza,” alisema Ndugai.
Kiongozi
huyo alianza na naibu waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso ambaye
alimtaka ajibu swali la nyongeza la Mwantumu Dau Haji (viti maalum -
CCM) ambalo lililenga katika suala zima la upatikanaji wa maji kwa ajili
ya kilimo cha umwagiliaji.
Kabla
ya swali hilo, tayari mbunge huyo alishauliza swali la msingi ambalo
lilielekezwa ofisi ya Makamu wa Rais na lilijibiwa na naibu waziri wa
wizara hiyo, Kangi Lugola likihusu masuala la mabadiliko ya tabia nchi.
Aweso
alisimama asijue nini cha kujibu huku akiendelea kutazamana na Spika
Ndugai kwa sekunde kadhaa ndipo akaamuliwa kuketi kwa kuwa alikuwa hajui
swali gani liliulizwa.
“Tatizo
lenu mawaziri hamsikilizi kinachoendelea ndani ya Bunge, mnapiga stori
tu. Haya naibu waziri Ofisi ya Makamu wa Rais okoa jahazi hilo,” alisema Ndugai.
Baada
ya maswali kadhaa kupita aliwataka naibu mawaziri ofisi ya Rais
(Tamisemi), Joseph Kakunda na Joseph Kandege kujibu swali la nyongeza
kuhusu umaliziaji wa majengo ambayo yanaanzishwa na wananchi.
“Haya
naibu mawaziri Tamisemi, Josephat Kandege naomba ujibu swali hilo. Kama
hujajipanga naomba mwenzako Joseph Kakunda ajibu, jamani ndiyo haya
niliyosema wapo hapa tu lakini wanapiga stori na hawasikilizi
kinachoendelea,” alisema spika.
Ndugai
aliwaonya pia wabunge kutozungumza na waziri mkuu na kumtaka kiongozi
huyo wa shughuli za Serikali kuzungusha macho ili kuona namna ambavyo
wabunge walikuwa wamesimama na kutaka kuuliza maswali kuhusu maji.
“Mheshimiwa
waziri mkuu, naomba hao wanaozungumza na wewe wakuache kwanza, hebu
geuka nyuma na uangalie pande zote uone namna ambavyo wabunge wamesimama
kutaka kuuliza maswali kuhusu maji majimboni kwao, Serikali iangalie
jambo hili,” alisema.
Wakati
huo spika aliitaka Serikali kutafakari namna ambavyo imekuwa ikitoa
maagizo na amri kila wakati kupitia mabaraza ya madiwani akisema siyo
afya na haijengi.
Alikuwa
akitolea majibu mwongozo ulioulizwa na mbunge wa Babati Mjini
(Chadema), Pauline Gekul kuhusu mpango wa Serikali kuagiza wananchi
kuendelea kumalizia majengo ya zahanati, maabara na madarasa
waliyoyaanzisha.
“Ndugu
zangu Serikali, anachokisema mbunge ni sahihi maana sasa imekuwa ni
kero kubwa, hebu angalieni jambo hilo kwani kila mahali ni maagizo
maagizo na hata tukienda kwenye baraza la madiwani utasikia kuna ajenda
ya kudumu ambayo ni maagizo, hii inakera jamani,” alisisiza Ndugai.
Pia,
aliwataka viongozi kuangalia namna bora ya kufanya ili kufikisha ujumbe
kuliko kuagiza kila mara ambako kunaondoa imani ya wananchi kwa
Serikali yao.
Hata
hivyo, alisema kumekuwapo na tabia ya baadhi ya viongozi kujiona kama
miungu watu na wanaamini kuagiza kila wakati kwa kutumia amri ndiyo
itakuwa maendeleo wakati si kweli.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )