Ndugu Wanahabari,
Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaendelea kutoa
taarifa za ugonjwa wa Kipindupindu ambao umeendelea kuwepo katika mikoa
kadhaa hapa nchini ukiwa unaongezeka na kupungua kwa vipindi tofauti.
Ndugu Wanahabari,
Kwa
kipindi cha kuanzia tarehe 01 Septemba 2017 hadi 30 Septemba 2017,
jumla ya wagonjwa walioripotiwa walikuwa ni 532 na vifo 8. Mikoa na
wilaya zilizoripoti kipindupindu kwa mwezi Septemba ni Tanga-104 na
vifo-2(Tanga Jiji-2, Korogwe Mjini-45, Korogwe Vijijini-23 na kifo-1,
Handeni Vijijini-20, Handeni Mjini-8 na kifo-1, Muheza-6), Iringa-22 na
kifo-1(Iringa Vijijini1), Njombe-10(Wanging’ombe-10), Katavi(Katavi
Vijijini-6), Iringa-2(Mufindi-2), Songwe-82(Songwe Vijijini-82),
Mbeya-254 na vifo-3(Mbeya Vijijini-16, Mbeya Mjini-11, Chunya-68,
Mbarali-159 na vifo-3) na Kigoma-52 na vifo-2(Kigoma mjini-52 na
vifo-2).
Vile
vile katika kipindi cha kuanzia tarehe 1 hadi 31 Oktoba 2017 , jumla ya
wagonjwa walioripotiwa walikuwa ni 570 na vifo 10. Mikoa na wilaya
zilizoripoti kipindupindu kwa mwezi Oktoba ni Dodoma-14 na
kifo-1(Kongwa-1, Chamwino-9, Bahi-4 na kifo-1), Iringa-58 na
kifo-1(Iringa Vijijini-58 na kifo-1), Tanga-6 na kifo-1(Mkinga-6 na
kifo-1), Morogoro-7(Kilosa-7), Mbeya-109 na vifo-3(Chunya-53 na kifo-1,
Mbarali-25, Mbeya Mjini-18, Mbeya Vijijini-13 na vifo-2) na Songwe-376
na vifo 4(Songwe-376 na vifo-4).
Ndugu Wanahabari,
Bado
maambukizi mapya ni tishio kwani kuna ongezeko la idadi ya Mikoa na
Halmashauri zinazotoa taarifa za wagonjwa. Vile vile nchi yetu
inaelekea katika majira ya mvua ambazo zinaweza kuongeza kuenea kwa
maambukizi ya ugonjwa, hivyo tunahitaji kuzidisha juhudi za kuzuia
ugonjwa huu, kwa kusimamia kikamilifu maelekezo na miongozo stahiki
inayotolewa.
Ufuatiliaji
wa ugonjwa wa Kipindupindu umebaini kuwa wagonjwa wamekuwa wakiishi
mbali na jamii linganifu na mahali pale kituo cha afya kilipo. Hii
imechangia wagonjwa kutofika kituo cha kutolea huduma za afya kwa wakati
na hivyo kupelekea kupoteza maisha. Hivyo, Wizara inaagiza kuwa vituo
vya kutolea “Oral Rehydration Salt”, maarufu kama ORS, katika jamii
(Community ORS points) vianzishwe na halmashauri kwa kushirikiana na
jamii ili kuzuia vifo. Jamii zielekezwe namna ya kutumia ORS kwa
usahihi. Endapo ORS haitapatikana, jamii ielekezwe kuchanganya chumvi na
sukari kwa kutumia maji safi yaliyochemshwa kiasi cha lita moja na
vijiko viwili vya sukari na nusu kijiko ya chumvi. Njia hii ya kutumia
ORS au mchanganyiko wa chumvi na sukari ndio njia ya muhimu ya kuokoa
maisha ya mgonjwa wa Kipindupindu kwani inasaidia kupunguza kasi ya
kupungukiwa kwa maji mwilini inayosababisha kifo.
Ndugu Wanahabari,
Ni
dhahiri kuwa ushirikishwaji wa sekta zote kwa ngazi zote hadi katika
jamii ni muhimu sana katika kukabiliana na ugonjwa wa Kipindupindu.
Wizara inasisitiza kuwa wadau wote wapewe nafasi katika mapambano haya
kupitia vikao mbalimbali ili kujadili udhibiti wa ugonjwa wa
Kipindupindu kwenye halmashauri na mikoa. Viongozi wa dini, watu
mashuhuri na waganga wa tiba mbadala pia wasaidie kuhamasisha jamii zao
kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu.
Wizara
inaendelea kuwasihi wananchi kuungana na Halmashauri, Mikoa pamoja na
Wizara katika juhudi za kupambana na kuenea kwa ugonjwa wa
Kipindupindu. Jamii izingatie kanuni za usafi binafsi na usafi wa
mazingira, ikiwa ni pamoja na:
- Kujenga na kutumia vyoo bora katika maeneo tunamoishi.
- Kunawa mikono kwa maji yanayotiririka na sabuni kabla ya kula, baada ya kutumia choo, na baada ya kumsafisha mtoto aliyejisaidia.
- Kunywa maji safi na salama yaliyotakaswa kwa dawa (kama vile water guard) au yaliyochemshwa na kupoa.
- Kuzingatia ushauri na elimu sahihi kuhusu ugonjwa wa Kipindupindu, ili jamii iondokane na imani potofu kuhusu Kipindupindu.
- Kufikisha wagonjwa wa Kipindupindu mapema katika vituo vya kutolea huduma ili wawahi kupata matibabu.
Ndugu Wanahabari,
Changamoto
moja wapo katika kudhibiti ugonjwa wa Kipindupindu ni upatikanaji wa
maji safi na salama. Wizara inasisitiza yafuatayo yasimamiwe kwenye
halmashauri na mikoa yote nchini.
Kuimarisha
mifumo ya upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo yote mijini
na vijijini hasa wakati wa mlipuko wa Kipindupindu. Hii ni pamoja na:
- Mamlaka za maji katika ngazi zote ziweke mkazo wa kuwepo kwa vyanzo mbadala vya maji.
- Utakasaji wa maji ya bomba kwa njia ya kutumia klorini ufanyike kama miongozo inavyotaka na ufuatiliaji wa ubora wa maji ufanyike kulingana na miongozo.
- Utoaji wa taarifa sahihi na kwa wakati, za ugonjwa wa Kipindupindu kwa kufuata miongozo iliyopo.
- Kuongeza uwajibikaji wa viongozi na watendaji (Leadership and accountability): Usimamizi wa utekelezaji wa miongozo katika kuzuia na kudhibiti ugonjwa huu ni muhimu kwa viongozi na wanaowasimawa. Hii ni pamoja na;
- Usimamizi wa utekelezaji wa sheria ndogondodo za usafi wa mazingira ili kuimarisha matumizi ya vyoo.
- Usafi wa mazingira pamoja na udhibiti wa biashara za chakula na pombe za kienyeji katika mitaa.
- Kuzingatia agizo la Mheshimiwa Rais la kufanya usafi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi.
Ndugu Wanahabari,
Wizara yangu imekuwa karibu na mikoa na halmashauri katika kudhibiti ugonjwa huu kwa kufanya yafuatayo:
- Kutuma timu za wataalamu kwenda kwenye maeneo yaliyoathirika kushirikiana na mikoa na Halmashauri katika kudhibiti ugonjwa huu
- Kupima vipimo vya maabara na kubaini aina ya vimelea vinavyosababisha ugonjwa pamoja na kupima usikivu wa dawa inayofaa kutibu wagonjwa katika mlipuko huu
- Kupeleka Vifaa tiba na dawa katika Mkoa wa Mbeya, Wilaya ya Mabarali kupitia kanda ya bohari ya Dawa (MSD)
- Kusambaza dawa ya kutibu maji majumbani katika mikoa ya Iringa, Kigoma, Katavi na Tanga
HITIMISHO
Wizara
inaendelea kushukuru mchango wa wadau mbalimbali katika kudhibiti
ugonjwa huu ikiwemo Sekta ya Maji kwa kuendelea kuongeza kasi ya
upatikanaji wa maji, bila kuwasahu wanahabari kwa kuendelea kusaidiana
na Serikali katika kuwaelimisha wananchi juu ya ugonjwa huu. Wizara
inaendelea kutoa wito kwa wadau wote katika ngazi zote kushirikiana kwa
pamoja katika jitihada za kutokomeza ugonjwa huu.
Asanteni sana
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )