Serikali
iko katika mchakato wa maandalizi ya muswada wa sheria ambayo
itasimamia sekta ya nyumba, hivyo kuondoa changamoto ya wamiliki kudai
kodi ya pango ya zaidi ya mwezi mmoja.
Naibu
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula amesema
hayo bungeni leo Ijumaa Novemba 17,2017 akijibu swali la nyongeza la
mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Halima Bulembo.
Halima
katika swali lake amesema vijana ambao ni kati ya asilimia 56 na 60
nchini, wanashindwa kutimiza ndoto zao kutokana na gharama kubwa ya kodi
ambayo hutakiwa kulipa kwa kipindi cha mwaka mmoja au miezi sita.
"Serikali
inasemaje kuhusu kuleta sheria itakayofuta tabia ya wenye nyumba
kulazimisha kulipwa kodi ya mwaka?" amehoji mbunge huyo.
Akijibu
swali hilo, Mabula amesema Serikali imeliona tatizo hilo na ipo katika
mchakato wa kuandaa muswada wa sheria utakaosimamia sekta hiyo.
Mabula
amesema baada ya kukamilika kwa sheria ambayo itaunda chombo cha
kusimamia sekta hiyo, wapangaji hawatalipa kodi ya mwaka wala miezi sita
tena bali watalipa kwa mwezi na kuweka amana ya miezi mitatu.
Katika
swali la msingi, Halima amesema kumekuwa na upandaji holela wa gharama
za pango kwa nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
"Je Serikali haioni kuna haja ya kudhibiti upandaji holela ambao unaathiri wananchi wengi kutokana na kipato chao?" amehoji.
Akijibu,
Mabula amesema utaratibu wa urekebishaji wa viwango vya kodi za shirika
hilo husimamiwa na bodi ya wakurugenzi ambayo imepewa mamlaka ya
kisheria ya kusimamia kodi ya pango na kuidhinisha viwango vya kodi
vinavyotozwa kwa wapangaji wa nyumba za shirika.
"Kwa
mara ya mwisho bodi ya wakurugenzi ya Shirika la Nyumba la Taifa
iliidhinisha viwango vipya vya kutoza kodi kwenye nyumba za shirika
mwaka 2011 ambavyo ndivyo vinavyotumika mpaka sasa," amesema.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )