Mahakama
ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro imetupilia mbali hati ya kiapo cha
kupinga dhamana ya wabunge Suzan Kiwanga(Mlimba), Peter Lijualikali
(Kilombero) na washtakiwa wengine 37 waliofikishwa mahakamani hapo kwa
makosa nane.
Mbele
ya Hakimu, Ivan Msaki mahakama ilitupilia mbali kiapo hicho na kueleza
kuwa washtakiwa wote dhamana yao iko wazi kwa masharti ya kuwa na
wadhamini wawili kila mmoja watakaosaini dhamana ya Sh 5 milioni na pia
barua za dhamana lazima zisainiwe na wenyeviti wa vijiji ama maofisa
watendaji.
Katika
kiapo kilichowasilishwa awali mahakamani hapo na upande wa mashtaka
kupitia wanasheria wa Serikali, Sunday Hyera na Edga Bantulaki ulieleza
sababu walizodai kuwa ni za msingi za kupinga dhamana na kwamba kuwepo
nje kwa washtakiwa kunaweza kuharibu upelelezi wa kesi hiyo.
Kufuatia
hoja hiyo upande wa utetezi unaowakilishwa na mawakili wanne
wakiongozwa na wakili Peter Kibatala uliamua kuwasilisha hati ya kupinga
kiapo hicho kwa madai kuwa kiliandikwa bila ya kuzingatia misingi na
matakwa ya kisheria.
Wakili
Kibatala alidai kuwa miongoni mwa mapungufu yaliyokuwemo kwenye kiapo
hicho ni pamoja na kutokuonyesha majina ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya
Malinyi (OCD) ambaye alitajwa kwenye kiapo hicho kama chanzo kilichotoa
taarifa zilizotengeneza mashtaka yanayowakabili wabunge hao na wenzao.
Alidai
kuwa mapungufu mengine yaliyokuwepo kwenye kiapo hicho ni utofauti wa
tarehe ya kuandika kiapo hicho na kusainiwa na hivyo waliiomba mahakama
kuzingatia mapungufu hayo.
Kutokana
na mvutano huo wa kisheria baina ya pande hizo mbili Hakimu Msaki
aliamua kupitia hoja za msingi za kisheria na hivyo kubaini mapungufu
yaliyopo kwenye kiapo hicho na kueleza kuwa mapungufu hayo hayawezi
kurekebishwa na kwamba kazi ya mahakama ni kutafsiri sheria na si
kufundisha namna ya kuandika kiapo.
Kwa
msingi huo Hakimu Msaki alitupilia mbali hati hiyo ya kiapo cha kupinga
dhamana na kueleza kuwa washtakiwa hao watakuwa nje kwa dhamana wakati
kesi yao ikiendelea.
Kabla
ya kupewa dhamana washtakiwa hao walikaa rumande kwa siku 12 hali
iliyosababisha kesi hiyo kuvuta hisia za watu hususani viongozi na
wanachama Chadema waliokuwa wakifulika mahakamani hapo.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )