Featured
Loading...

Sakata la Mo Dewji Kutekwa laibuka bungeni

 
Mbunge wa Iringa mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), ameibua suala la kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji kiaina.

Akichangia mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa taifa wa mwaka 2019/20 bungeni leo Jumanne Novemba 6, 2018 , Mchungaji Msigwa alisema wafanyabiashara hawako huru kufanya biashara nchini.
“Wawekezaji wanajionaje kuwepo katika nchi hii, wapo salama? Takwimu zinaonyesha wawekezaji wa nje wanafunga virago.

“Je wawekezaji wa ndani wakoje? Wana raha? Kama bilionea mkubwa nchi hii anaweza akashikwa, akafichwa, akaachiwa halafu hadi leo hajaruhusiwa kusema alikuwa wapi unadhani nani atakuja kuweka biashara hapa ndani? Haya mambo hatuwezi kufumbia macho, lazima tuyajadili.”

Alisema hadi leo hakuna taarifa ni nani aliyemteka na pia alikuwa wapi na kuhoji  kwa sasa diplomasia ya nchi ikoje.

“Wakati wa Benjamin Mkapa (Rais wa Awamu ya Tatu) aliwahi kusema Tanzania inahitaji ulimwengu kuliko ulimwengu unavyotuhitaji sisi.”

“Kama leo Balozi wa Ulaya anaitwa nchini kwake kujadili mahusiano  kama taifa linahitaji kujiuliza wageni wanaionaje Tanzania. Wafanyabiashara wanafunga virago wanaondoka kwa sababu wanaona hawako sawa. Mheshimiwa Mpango, (Waziri wa Fedha na Mpango Dk Philip Mpango)  Serikali yako haieleweki inaendeshaje uchumi wa namna gani?” alihoji.

Aidha, alisema taifa linahitaji Katiba ambayo itawaunganisha Watanzania wote. Mwalimu Nyerere walipigana vita ya Uganda na wakashinda kwa sababu walikuwa wamoja,” alisema.

Alisema kinachowaunganisha Watanzania wote ni Katiba ili kuweza kupigana na kushinda vita ya uchumi.

Alisema wateule wa Rais wanamtii yeye tu na kwamba kila mtu ni kambale (samaki) na kwamba wakuu wa mikoa na wilaya hawawatii mawaziri.

“Mtu anatumia Instrument (vifaa) vya Serikali amekaa katika ofisi yenye bendera, polisi wanamlinda halafu mnasema hayo ni ya  kwake mwenyewe. Kama ni ya kwake mwenyewe kwa nini hamchukulii hatua?” alihoji.

Wakati akiendelea kuchangia, aliibuka Mbunge wa Siha (CCM), Dk Godwin Mollel na kutaka kufahamu Chadema ilizungumza nini katika kikao walichokifanya kati yao na mashoga 40.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bunge,  Mussa Zungu alimpotezea Dk Mollel na kumtaka Mchungaji Msigwa aendelee kuchangia mpango huo.


Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
© Copyright MZALENDO HURU
Back To Top