Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na
Walemavu), Jenista Mhagama amewataka wananchi kuvuta subira kuhusu
uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), kwa
sababu mamlaka za juu zitamteua wakati mwafaka ukifika.
“Niliteua
kaimu mkurugenzi wa NSSF, uteuzi ukatenguliwa kwa sababu baadhi ya
taratibu zilikuwa hazijakamilika, the business is over (biashara
imekwisha), tusubiri mamlaka za juu zitafanya uteuzi, mna haraka ya
nini?” alihoji Mhagama.
Alipoulizwa
nani anayesimamia uendeshaji wa shirika hilo kwa sasa, Mhagama alisema:
“Jamani, nimeshasema tusubiri mamlaka za juu, sina cha kuongeza.”
Waziri Mhagama alimteua Dk Carina Wangwe kukaimu nafasi hiyo lakini uteuzi huo, ulidumu kwa saa tano na kutenguliwa.
Nafasi
hiyo ipo wazi tangu Februari 15, baada ya Rais John Magufuli kumteua
aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk Ramadhani Dau kuwa balozi.
Ripoti NSSF yatia shaka
Awali,
Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria ilisema ripoti ya utendaji ya NSSF
iliyofikishwa mbele yake haina viwango kama ambavyo mfuko huo
unavyoonekana mbele ya jamii.
Mwenyekiti
wa Kamati hiyo, Mohamed Omar Mchengerwa alisema taarifa zilizomo kwenye
ripoti hiyo hazionyeshi miradi inayoendelezwa na mfuko huo.
“Tumeipokea
na kuijadili kwa sababu ya kuheshimu kazi zinazofanywa na mfuko na
uwapo wa Waziri Mhagama, vinginevyo tungewatoa nje mkaifanyie
marekebisho,” alisema.
Hata
hiyo, Mchengerwa aliagiza watendaji wa shirika hilo kupeleka ripoti
yenye taarifa kamili ifikapo Machi 31. “Tunataka tukiisoma taarifa
tunaijua vizuri NSSF, miradi yake yote na thamani yake, nyie mnatuletea
taarifa fupi ambayo haina majibu ya maswali tunayoyataka,” alisema.
Katika
taarifa hiyo, mfuko huo unalalamikia wanachama wengi kujitoa mara
wanapomaliza mikataba na waajiri wao na kuhitaji mafao kabla ya umri wa
kustaafu.
NSSF
inasema kumekuwa na ongezeko kubwa la mfuko kulipa mafao wanachama wa
aina hiyo na kwamba, miaka michache ijayo kutakuwa na wastaafu wengi
ambao hawana mafao ya uzeeni hivyo kuwapo wazee wengi wasio na kipato.
Akifafanua
hilo, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Crescentius Magori alisema kuna
haja ya Serikali kurudisha sheria ya kuzuia wanachama kujitoa kabla ya
kufikisha umri wa kustaafu.
Magori alisema wazee wengi ambao hawana mafao ya uzeeni wanakufa haraka, kuliko wanaolipwa mafao kila mwezi.
“Kuna
takwimu zinaonyesha ukubwa wa tatizo hilo, Serikali inatakiwa kurudisha
sheria na kuzuia wanachama kujitoa kwenye mifuko kwani wao wenyewe
ndiyo watakaoumia uzeeni,” alisema.
Naye Waziri Mhagama aliwaagiza watendaji wa mfuko huo kutayarisha ripoti ambayo itakusanya miradi yote inayoendelezwa.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )