Rais
wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni ametoa tamko la kulaani uamuzi
uliotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) ambayo
imemuagiza mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo kuanzisha uchunguzi dhidi
ya mgogoro wa Burundi.
Rais
Museveni ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
amesema ICC inaingilia mambo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki bila
kuwahusisha viongozi wa Jumuiya hiyo jambo ambalo sio sahihi na
linarudisha nyuma juhudi za kutafuta amani ya Burundi.
Rais
Museven amezungumza hayo kabla ya kuagana na Rais Magufuli ambaye jana
amemaliza ziara rasmi ya kiserikali ya siku 3 nchini Uganda na kurejea
nchini Tanzania.
Akizungumzia
uamuzi huo wa ICC Mh. Magufuli amesema hatua hiyo inarudisha nyuma
hatua zilizochukuliwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo iliunda
Kamati ya usuluhishi wa mgogoro wa Burundi inayoongozwa na Mhe. Rais
Museveni na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Tanzania Mhe. Benjamin
William Mkapa.
Rais
Magufuli aliagana na Rais Museveni katika Mji wa Masaka na baadaye
kusindikizwa na Makamu wa Rais wa Uganda Mhe. Edward Kiwanuka Sekandi
hadi Mutukula, mpakani mwa Tanzania na Uganda.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )