Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
amekutana na kufanya mkutano wa kazi na watendaji wa ofisi yake ya Idara
ya Mazingira kujadili kwa kina namna ya kukabiliana na hali tete ya
uharibifu wa mazingira unaoendelea nchini.
Katika
mkutano huo uliofanyika leo, Ikulu, Dar es salaam ambao ulihudhuriwa
pia na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na
Mazingira January Makamba, Makamu wa Rais ameawaagiza watendaji wa idara
hiyo waache kukaa ofisini na badala yake waende kutoa elimu kwa
wananchi kuhusu namna ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira katika
maeneo mbalimbali nchini.
Alisema
hali ya uharibifu wa mazingira ikiachwa iendelee kama ilivyo inaweza
ikasababisha madhara makubwa kwa jamii na Taifa kwa ujumla, hivyo ni
muhimu kwa makundi yote wakiwamo wataalam wa mazingira na wadau wa
maendeleo kuelekeza nguvu zao katika kukabiliana na tatizo hilo.
Alisema
baadhi ya watendaji wamekuwa ni sehemu ya uharibifu wa mazingira na
kuonya wataobainika kufanya vitendo hivyo watachukuliwa hatua kali ili
kukomesha tabia hiyo.
Baadhi
ya watendaji waliotoa taarifa kuhusu hali ya mazingira nchini wamekiri
kuwa hali ya uharibifu wa mazingira siyo nzuri hasa kwenye mikoa ya
Dodoma, Shinyanga, Manyara, Geita, Singida na Kilimanjaro.
Inakadiriwa kuwa takribani hekta 400,000 za misitu zinaharibiwa kila mwaka hali ambayo inapelekea baadhi ya wanyama kutoweka.
Watendaji
hao wameiomba serikali iongeze bajeti ya kutosha ili waweze kukabiliana
na tatizo la uharibifu wa mazingira ikiwemo utoaji wa elimu kwa
wananchi.
Makamu
wa Rais ametumia siku ya mapumziko ili kujadiliana na kuweka mipango na
mikakati ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira nchini. Mkutano huo
wa kazi unaendelea tena hapo kesho.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es salaam
20/8/2016
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )