Wakati
sakata la kumpata Meya wa Jiji la Dar es Salaam likiendelea kupamba
moto baada ya mchakato huo kuwekewa zuio la mahakama juzi, serikali
imetishia kuivunja Halmashauri ya Jiji la Tanga iwapo haitamaliza
mgogoro wake wa kisiasa.
Akizungumza
na viongozi serikali na kisiasa jijini Tanga jana, Makamu wa Rais,
Samia Suluhu Hassan, alisema serikali italazimika kuivunja halmashauri
hiyo endapo mgogoro huo hautamalizwa haraka, kutokana na ukweli kwamba
tangu kuanza kwa uongozi wa awamu ya tano baada ya uchaguzi mkuu wa
mwaka jana imeshindwa kufanya vikao vyake halali kwa mujibu wa katiba
kutokana na mgogoro wa kisisa bina ya Chama Chama cha Mapinduzi (CCM) na
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa, huku wananchi wakishindwa
kutatuliwa kero zao kwa wakati hivyo kuzorotesha maendeleo yao.
“Mpaka
sasa jiji la Tanga hakuna uongozi uliosimama, sasa hatuwezi kwenda kwa
mwendo huu, wananchi wanahitaji maendeleo na kurudia uchaguzi hatuwezi
ni gharama kubwa, kilichobaki ni kuivunja halmashauri mpaka hapo muda wa
kufanya uchaguzi kwa mujibu wa katiba ya nchi utakapotimia, hivyo kwa
maana nyingine kama itavunjwa serikali kuu ndiyo itasimamia shughuli za
jiji hili,” alisema Suluhu.
Alisema
mkoa huo una mipango mbalimbali ya maendeleo lakini haiwezi
kutekelezeka kutokana na mgogoro uliopo na kuwataka viongozi wa mkoa kwa
kushirikiana na wazee kukaa chini kutafuta namna ya kuumaliza haraka.
“Jiji
ni kioo cha mkoa mzima, sasa kama wazee hawatakaa kitako na viongozi
kutafuta suluhu, basi hii mipango yenu yote ya kufufua viwanda itakuwa
ni ndoto tu kwa sababu hapa mjini hakupo shwari na tunalitambua hilo,” alisema.
Mgogoro
wa umeya Tanga umeibuka baada ya CCM yenye madiwani wachache kushinda
nafasi hiyo dhidi ya Ukawa yenye madiwani wengi jambo ambalo linapingwa
na umoja huo unaondwa na vyama vya CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na NLD.
Hatua
kama hiyo ya kuvunja halmashauri si mara ya kwanza kutokea nchini,
kwani mwaka 1996, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ilivunjwa na
serikali na badala yake ikaundwa Tume ya Jiji iliyokuwa chini ya Charles
Keenja.
Makamu
wa Rais pia alisema mkoa wa Tanga unakabiliwa na changamoto kubwa ya
biashara ya magendo, hali ambayo inarudisha nyuma mkoa huo kiuchumi na
kimaendeleo.
Kufuatia
hatua hiyo aliiagiza kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo kutumia
kila mbinu kuzuia biashara hiyo ili mkoa uweze kuimarika kiuchumi na
kimapato.
Kuhusiana
na suala la chakula, Makamu wa Rais alisema serikali ya awamu ya tano
haitamvumilia mkuu wa mmoa yeyote wala wilaya ambaye atatoa malalamiko
ya kukosekana kwa chakula kwenye eneo lake na badala yake atakuwa
amejifukuzisha kazi mwenyewe.
Alisema
kukosekana kwa chakula wakati viongozi wa eneo husika wana uwezo wa
kujenga malambo ili kukinga maji ya mvua kipindi cha masika na
kuwaelekeza wananchi kulima mazao yanayostahimili ukame, itakuwa ni
kipimo chao cha uongozi na wale ambao watashindwa kupata madawati kwa
ajili ya shule kwenye maeneo yao.
Awali
akisoma taarifa ya mkoa wa Tanga kwa Makamu wa Rais, Mkuu wa Mkoa wa
Tanga, Mwantumu Mahiza, alisema hali ya chakula mkoani humo hadi kufikia
mwezi huu si ya kuridhisha kutokana na kuchelewa kunyesha kwa mvua
msimu wa mwaka 2014/2015 na hata ziliponyesha hazikuwa na mtawanyiko
mzuri.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )