Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa akikagua bandari ya Mtwara na kunusa harufu ya
ufisadi katika utoaji wa zabuni ya ujenzi wa gati mpya tatu.
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amekagua bandari ya Mtwara na kunusa ufisadi katika utoaji wa zabuni ya ujenzi wa gati mpya tatu.
Amekinyooshea kitengo cha manunuzi bandarini hapo, akisema kimekuwa
chanzo cha upotevu wa fedha za serikali kutokana na ujanja wa watu
wachache.
Waziri Mkuu aliigusa pia Bodi ya Korosho akisema yako majipu
yanayohitaji kutumbuliwa kutokana na kukwamisha mizigo kupitia bandari
ya Mtwara, badala yake inapitishwa kupitia bandari ya Dar es Salaam.
Utata wa zabuni
Majaliwa ambaye juzi alitembelea eneo la ujenzi wa gati hizo, alisema
mzabuni ameshashinda, lakini yapo madai kwamba watu wa manunuzi kupitia
Mamlaka ya Manunuzi ya Umma Tanzania (PPRA) ndiyo wanakwamisha zabuni
hiyo.
Alisisitiza, “Natambua kwamba kuna mpango wa kujenga gati nne ambapo
moja kati ya hizo itajengwa na TPA (Mamlaka ya Bandari) lakini hizi tatu
zilitangazwa na kupata mzabuni ambaye ni kampuni ya Hyundai kutoka
Japan. Lakini hii kampuni imekuwa ikizungushwa bila sababu. Tutafuatilia
kubaini tatizo liko wapi.”
“Sasa hivi tuna uwezo wa kupaki meli moja tu, lakini gati zikikamilika
tutaweza kuwa na meli tatu kwa mpigo, cha msingi tusimamie maamuzi yetu
kwamba lazima wafanyabiashara wa korosho watumie bandari hii kusafirisha
mizigo yao na si kuipeleka kwingine,” alisema.
Kitengo cha manunuzi
Waziri Mkuu alimtaka Mkuu wa Bandari ya Mtwara, Prosper Kimaro kuwa
makini na watu wa kitengo cha manunuzi katika bandari hiyo, akisema
kimekuwa chanzo cha upotevu wa fedha za Serikali kutokana na ujanja wa
watu wachache.
“Hapa si kuna mtu alitaka kuiba Sh milioni 300 kwa kufoji (kughushi)
saini za wakubwa wake?” Alihoji Waziri Mkuu, swali ambalo lilijibiwa na
Kimaro akikiri juu ya hilo na kusema, uongozi uliingilia kati kabla wizi
huo haujakamilishwa.
Bodi ya Korosho
“Kwenye Bodi ya Korosho nako kuna majipu yanahitaji kutumbuliwa. RCC
(Baraza la Ushauri la Mkoa) ilishakaa na kupitisha uamuzi kuwa mizigo
yote ipitie bandari ya Mtwara lakini kuna watu ndani ya Bodi hiyo
wanatoa vibali vya kusafirisha mizigo kupitia bandari ya Dar es Salaam,”
alisema Waziri Mkuu.
Aliomba wabunge wa Mkoa wa Mtwara washirikiane kusimamia ujenzi wa gati
uanze mara moja, ili ajira kwa wananchi mkoani humo zipatikane.
“Ujenzi ukikamilika siyo tu ajira zitaongezeka bali hata meli nyingi
zitaleta mizigo katika bandari hii na mapato ya mkoa yataongezeka”,
alisema.
Fidia kisiwa cha Mgao Kuhusu fidia kwa wakazi wa vijiji vya Kisiwa na
Mgao ambao wamekubali kuhama ili kupisha upanuzi wa bandari hiyo, Waziri
Mkuu aliwahakikishia wabunge hao pamoja na uongozi wa bandari kwamba Sh
bilioni 13.8 zimekwishatengwa na Wizara na zitatolewa mapema mwezi
ujao.
Alitumia fursa hiyo kusisitiza udhibiti wa bandari bubu ambazo
zinatumiwa kuingiza sukari na mchele na kuikosesha Serikali mapato.
“Mkuu wa Mkoa, nilikwishatoa agizo kama hilo wakati nimeenda kukagua
bandari ya Tanga. Kaa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa nanyi pia
muweke mbinu za kudhibiti upenyo huu wa kuingiza bidhaa za magendo kwa
sababu hawa ndiyo wanaokwepa kulipa kodi ya Serikali,” alisisitiza.
Awali, Mkuu wa bandari ya Mtwara, Kimaro wakati akitoa taarifa ya
utendaji wa bandari mbele ya Waziri Mkuu, alisema ilianzishwa mwaka 1950
na imekuwa ikikabiliwa na ufinyu wa gati ya kuegesha meli, vifaa vya
kupakulia na kupakia mizigo.
Alisema hivi sasa wamekwishapata winchi ya bandarini yenye uwezo wa kubeba tani 100 na wako kwenye mpango wa kujenga gati moja.
Majipu bandarini
Waziri Mkuu, Majaliwa ameshafanya ziara kwenye Bandari za Dar es Salaam,
Tanga na sasa Mtwara ambako amebaini mambo mengi hayaendi vizuri hali
ambayo amekuwa akilazimika kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwajibisha
watendaji.
Chini ya mkakati wa Serikali ya awamu ya tano ya kutumbua majipu, Rais
John Magufuli alivunja bodi simamizi ya bandari siku chache baada ya
kupatikana kwa kontena ambazo hayakuwa yamelipiwa ushuru Bandari ya Dar
es Salaam.
Kampuni 43 ziligunduliwa kuhusika katika makontena hayo. Mwenyekiti wa
Bodi, Profesa Joseph Msambichaka sanjari na Mkurugenzi Mkuu wa Bandari,
Awadhi Massawe walivuliwa nyadhifa zao .
Pia Katibu mkuu wa wizara ya uchukuzi, Dk Shaban Mwinjaka aliondolewa
kwenye wadhifa huo. Waziri Mkuu, Majaliwa alipofanya ziara ya
kushitukiza katika bandari ya Dar es Salaam, aligundua kontena 329
zilipitishwa bila kulipiwa kodi kinyume na utaratibu wa bandarini.
Aidha, Waziri Mkuu, hivi karibuni alifanya ziara ya kushitukiza katika
Bandari ya Tanga ambako pamoja na masuala mengine, alikuta tishali tatu
zikiwa chakavu bila ya injini wakati serikali ilitoa fedha za ununuzi wa
matishali ya kisasa.
Baada ya kubaini jipu hilo, alimwagiza Meneja wa Bandari ya Tanga, Henry
Arika kutoa maelezo kwa maandishi ya nani alihusika na ununuzi wa
matishali hayo badala ya zile mbili zilizopaswa kuwapo ambazo Serikali
ilitoa dola za Marekani milioni 10.
Arika alijitetea kwamba tishari hizo ziliwasili nchini miaka minne
iliyopita iliyopita lakini zilianza kufanya kazi rasmi mwaka jana na
kwamba yeye hana muda mrefu katika bandari hiyo.
CHANZO: HABARI LEO
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )