Mahakama
Kuu Kanda ya Moshi, imemfunga jela maisha mfanyabiashara, Silay Maulid
Jumanne (35) baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha kilo 21 za
majani ya mirungi.
Hukumu
hiyo iliyotolewa jana na Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo, Aishiel
Sumari, ni ya kihistoria katika vita dhidi ya dawa za kulevya nchini
kwani haijawahi kutolewa tangu Tanzania ipate Uhuru.
Wengi
wa wanaokamatwa na mirungi, hushtakiwa kwa kupatikana na mirungi,
shtaka ambalo husikilizwa na mahakama za chini tofauti na kusafirisha
ambalo husikilizwa na Mahakama Kuu.
Kutokana
na mazoea hayo, washtakiwa wengi wanaopatikana na hatia kwa kosa la
kupatikana na mirungi, huishia kupigwa faini hatua inayoelezwa kuchangia
kushamiri kwa matumizi ya mirungi.
Hata
hivyo, mshtakiwa huyo jana hakuamini masikio yake pale Jaji Sumari
alipomweleza kuwa adhabu ya kusafirisha mirungi kama ilivyo dawa
nyingine za kulevya ni kifungo cha maisha jela.
Akitoa
adhabu hiyo, Jaji Sumari alisema upande wa mashtaka ukiongozwa na
Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tamari Mndeme umejenga kesi hiyo na
kuishawishi Mahakama pasi na kuacha shaka.
Upande
wa mashtaka ukiongozwa na Wakili Mndeme akisaidiwa na mwenzake Kassim
Nassir, ulidai kuwa Septemba 7, 2013, mshtakiwa alikamatwa na vifurushi
21 vya Mirungi.
Kwa
mujibu wa mashtaka hayo, mshtakiwa alikamatwa kituo kikuu cha mabasi
mjini Moshi, akiwa kwenye harakati za kusafirisha mirungi hiyo kwenda
kuiuza jijini Arusha.
Jaji
Sumari alisema ushahidi wa mashahidi watano wa upande wa mashitaka,
umethibitisha kuwa mshtakiwa alikamatwa na begi la rangi ya kijani
likiwa na mirungi hiyo.
Alisema
licha ya mshtakiwa aliyekuwa akitetewa na Wakili Martin Kilasara,
kujitetea kuwa hakukamatwa stendi kuu bali eneo la Majengo mjini Moshi,
ushahidi umethibitisha alikamatwa stendi kuu.
“Baada
ya kusikiliza ushahidi, mashahidi wamethibitisha ulikamatwa Stendi Kuu
Moshi, ushahidi huo uliungwa mkono na kondakta wa basi na dereva teksi
aliyekuchukua,” alisema.
Jaji
Sumari alisema polisi hawakuwa na sababu yoyote ya msingi ya
kumbambikia shtaka mshtakiwa huyo, kama alivyojaribu kujitetea na
kusisitiza kuwa ushahidi ulikuwa madhubuti dhidi yake.
“Kulikuwa
na tofauti ndogondogo kama begi lilibebwa na nani kutoka stendi, au
kutoka kwenye basi kwenda kwenye teksi lakini zilikuwa ni tofauti ndogo
hazikuharibu mizizi mikuu ya ushahidi,” alisema.
Kwa
mujibu wa Jaji Sumari, ukiacha ushahidi huo, ungamo la mshtakiwa
linaongeza nguvu na kushabihiana na ushahidi uliotolewa na mashahidi.
Jaji
Sumari alisema mirungi ni dawa za kulevya zenye madhara, ushahidi wa
Mkemia Mkuu wa Serikali, ulibainisha matumizi yake humfanya mtumiaji
kuwa mtegemezi wa dawa hizo.
“Matumizi
ya dawa za kulevya yanaathiri jamii ulim wengu mzima hasa vijana, hivyo
sheria hii ilitungwa ikizingatia uhai wa binadamu ndiyo maana imeweka
adhabu kali,” alisema.
Jaji
Sumari alimweleza mshtakiwa huyo ambaye muda wote alikuwa akijifuta
jasho na kunywa maji, kuwa mtu yeyote anayepatikana akisafirisha mirungi
na dawa nyingine ni kufungwa jela maisha.
Hukumu
hiyo ilionekana kuwa gumzo katika viunga vya mahakama hiyo jana, huku
wanasheria wakisema inapeleka ujumbe kwa jamii kutodharau kosa
linalohusiana na mirungi.
Mwenyekiti
wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Tawi la Moshi, David Shilatu
alisema hukumu hiyo ni ya kwanza kutolewa na ya aina yake Tanzania.
“Kwa
sheria zetu hizi na marekebisho yake, mirungi nayo inaangukia daraja la
dawa za kulevya, kwa hiyo upande wa mashtaka ukithibitisha ulikuwa
unasafirisha adhabu ni kubwa,” alisema Wakili Shilatu.
Shilatu
alisema ingawa mshtakiwa anayo haki ya kukata rufaa, lakini hukumu hiyo
itoshe kupeleka ujumbe kwa jamii kwamba matumizi ya mirungi na
usafirishaji wake ni kosa la jinai nchini.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )