Bilionea Trump amemshinda mpinzani wake wa karibu, Seneta Ted Cruz, ukiwa ni ushindi wake wa 13 kwenye kura za mchujo za chama chake cha Republican.
Kabla ya ushindi huo, Trump alikuwa mbele kwa kura za wajumbe 384 dhidi ya 300 za Cruz.
Wadadisi wanasema ushindi huo umezima uvumi wa mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa kampeni ya Trump ilikuwa imepoteza kasi.
Baada ya kupata ushindi huo, Trump alisema anakiongezea umaarufu Republican.
Mshindani wake mkuu, Seneta Ted Cruz naye alipata ushindi katika jimbo dogo la Idaho.
Naye Hillary ameshinda kwa urahisi kwenye jimbo hilo la Missisipi linalokaliwa na Wamarekani wengi wenye asili ya Afrika, dhidi ya mshindani wake wa karibu ndani ya chama chake, Bernie Sanders.
Kati ya wajumbe 36 wa jimbo hilo, Hillary amejinyakulia kura za wajumbe 21. Kwa ujumla, mke huyo wa rais wa zamani, anaongoza kwa wajumbe 1,155 mbele ya Sanders mwenye kura za wajumbe 502.
Ili mtu kuweza kuteuliwa kuwa mgombea, anahitaji kupata kura za wajumbe 2,383.
Trump ambaye hata hivyo, aliangushwa na Cruz kwenye jimbo la Idaho, aliwaambia wafuasi wake mjini Michigan kuwa kwa sasa ana uhakika wa kuwa Rais wa Marekani.
“Tupo mbele kwa kiasi cha asilimia 50 au zaidi. Hapo unazungumzia mamilioni ya watu.
Naamini kabisa kuwa hii ni habari kubwa kabisa kwenye siasa, na ninatarajia Warepublican wataipokea. Tuna Democrat wanakuja, tuna wagombea huru wanakuja, lakini hawana idadi hiyo na pengine kamwe hawatakuwa nayo,” alisema Trump.
Hillary Clinton ambaye ni waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani, alilichukua kwa urahisi jimbo la ghuba ya kaskazini la Missisipi, ambalo lina wafuasi wengi wa Democratic.
Tayari mke huyo wa rais wa 42 wa Marekani, amejikingia zaidi ya nusu ya kura wa wajumbe 2,382 zinazohitajika kuteuliwa kupeperusha bendera ya kuwania kiti hicho, akiwekeza zaidi kampeni zake kwenye uwezo wa Wamarekani kujiamini katika kuleta mabadiliko, mfano wa ilivyokuwa kampeni ya Rais Barack Obama.
“Usimruhusu mtu kukwambia kuwa hatuwezi tena kufanikiwa Marekani. Tunaweza, tunafanikiwa na tutafanikiwa. Lakini ili hilo liwe, hatuwezi kujenga kwenye kuta kongwe au kurejesha majira ya saa nyuma. Tunapaswa kujenga juu ya kile kinachoifanya Marekani kuwa taifa kubwa, nishati, matumaini, uwazi na ubunifu wetu,” aliwaambia wafuasi wake.
Sanders bado aonyesha dhamira
Licha ya kuwa hesabu za kura zinamuweka Hillary mahala pazuri zaidi mpinzani wake, Sanders ameibuka kuwa mwanasiasa mwenye dhamira ya dhati ya kusonga mbele.
Katika jimbo la Michigan, mzee huyo wa miaka 74 ambaye ana uzoefu wa harakati za kisiasa kwa zaidi ya miaka 50, amemuangusha Hillary kwa asilimia 2.
Anatajwa kuwavutia zaidi wapiga kura vijana kwa kampeni yake ya mapinduzi ya umma, usawa wa kiuchumi na mapambano dhidi ya kile anachokiita “mfumo wa kifisadi wa kisiasa”
“Watu wa Marekani wanasema kuwa wamechoka na mfumo wa kifisadi wa kampeni na ufadhili wa matajiri wakubwa, Wall Street na tabaka la mabilionea.
Wamechoka na uchumi unaoibiwa ambapo watu wa Michigan, Illinois, Ohio, wafanya kazi kwa masaa mengi kwa mshahara wa kiwango cha chini, wakiwa na wasiwasi na mustakabali wa watoto wao,” alisema mjini Michigan.
Wachambuzi wanasema iwapo Sanders hatafanikiwa kuitwaa tiketi ya Democratic kuwania urais, kama ambavyo amewahi kuikosa huko nyuma, athari yake kwenye siasa za sasa za Marekani ni kuweza kudharaulika.
Uchaguzi huo umefanyika siku chache baada ya wagombea wakuu wa Republican kushinda majimbo mawili kila mmoja katika kura ya mchujo.
Cruz ameshinda majimbo ya Kansas na Maine huku Trump, akitwaa majimbo ya Louisiana na Kentucky.
Trump ameshinda majimbo mengine kadhaa ya awali na anaongoza wapinzani wake katika Republican, jambo linalowatia wasiwasi vigogo wa chama hicho wakisema sera na kauli zake zinakwenda kinyume na maadili ya Marekani.
Cruz anasema yeye ndiye anaweza kuwa mgombea mbadala wa bilionea huyo wa New York.
Wagombea wengine 12 wa Republican walijotoa kwenye mbio hizo baada ya kufanya vibaya katika hatua za awali na hivyo kufanya uwanja kusaliwa na wanasiasa wanne.
Kwa upande wa Democratic, Hillary Clinton amemshinda Louisiana huku mpinzani wake seneta Bernie Sanders akishinda Kansas na Nebraska.
Akihutubia wapinzani wake amesema demokrasia ya Marekani haipaswi kuharibiwa na mabilionea.
Awali wagombea hao wa Democratic walichuana vikali katika mdahalo uliofanyika juzi huku kila mmoja akitamba kuwa katika nafasi nzuri ya kukabiliana na mgombea yoyote kutoka Republican.
Wagombea hao wanaotafuta tiketi ya kugombea urais wa Marekani wamesema wapo tayari kupambana na Trump.
Hillary na Sanders, walisema kwamba wako tayari kupambana na Trump kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Wakizungumza wakati wa mdahalo uliofanyika mjini Flint katika jimbo la Michigan, walisema midahalo yao ni tofauti na ile ya Warepublican.
Wamedai hivi karibuni wamekuwa wakishambuliana na kurushiana matusi.
Sanders aliibua kicheko aliposema Warepublican wamedhihirisha waziwazi kwa nini utawala wake utalipa kipau mbele suala la kuwekeza kwa taasisi za kushughulikia afya ya akili.
Wakazi wa mji wa Flint, wengi wao wakiwa ni watu weusi maskini, wamekuwa wakikabiliana na mzozo wa maji yaliyo na kemikali za chuma.
Suala hilo limezua mtafaruku baina ya viongozi wa Serikali kwa miezi kadhaa.
Wanasiasa hao wawili, walimtaka Gavana wa Jimbo la Michigan, Rick Snyder kujiuzulu kufuatia kashfa hiyo.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )