Akizungumza na MTANZANIA mjini hapa jana, baada ya kumalizika kikao cha kwanza cha Kamati Kuu, Mbowe alisema sifa za kiongozi anayepaswa kushika wadhifa huo zinafahamika.
Alisema wajumbe na wanachama wa Chadema watarajie kumpokea mtu makini ambaye jina lake atalipendekeza kisha kupigiwa kura na wajumbe wa Baraza Kuu kesho.
“Sifa za Katibu Mkuu zinajulikana, nawaomba wanachama na wajumbe kutulia, jina watakutana nalo ukumbuni muda ukifika… nina imani litakuwa jina la mtu makini,” alisema.
Mbowe alisema chama hicho kinakutana kwa mara ya kwanza tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa Rais mwaka jana, hivyo wana mambo mengi ya kujadili, ikiwa ni pamoja na kupanga mikakati mipya ya kuwafikia wafuasi wao.
Katika hatua nyingine, chama hicho kimesema kitamtambulisha Katibu Mkuu mpya rasmi Jumapili wakati wa mkutano wa hadhara utakaofanyika viwanja wa Furahisha jijini hapa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Ofisa Habari wa chama hicho, Tumaini Makene, alisema majina mawili yatawasilishwa katika Baraza Kuu litakalokaa usiku wa Jumamosi kwa ajili ya kupitisha jina moja.
Alisema majina yatakayowasilishwa hayatakuwa na uhusiano au urafiki wowote na Mwenyekiti Mbowe.
“Tayari viongozi wa kitaifa wamewasili Mwanza, Sekretarieti imekutana kwa ajili ya kuandaa ajenda ambazo zitajadiliwa na Kamati Kuu yenye wajumbe 36.
“Siku inayofuata Baraza Kuu litakaa usiku kwa ajili kumpata Katibu Mkuu, hii ni nafasi nyeti sana ndiyo maana hata wenzetu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanafuatilia kwa ukaribu kujua nani atapewa mikoba ya Dr Slaa.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )