Featured
Loading...

Gavana BOT Afunguka Kuhusu Watoto wa Vigogo Walioajiriwa Bank Kuu...Adai Hakuna Jipya Kama Wanasifa Kwanini Wasiajiriwe?


Hatimaye Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Benno Ndulu amefunguka kuhusu hatma ya watoto 14 wa vigogo wanaodaiwa kuajiriwa kwa kubebwa katika taasisi hiyo nyeti kwa mustakabali wa taifa kiuchumi.

Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu jana, Prof. Ndulu alisema orodha hiyo, ambayo mwandishi alimsomea kuanzia mwanzo hadi mwisho, haina jipya.

Prof. Ndulu alisema hakuna ubaya wowote kwa mtu mwenye sifa kuajiriwa na BoT, bila kujali jina lake.
Kuanzia juzi na jana, orodha ya majina ya watu 14 wanaotajwa kuwa ni watoto wa vigogo waliopo BoT ilikuwa ikisambazwa kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii.

Mjadala katika mitandao hiyo ilikuwa huenda wapo watakaoguswa katika kutekeleza agizo la Rais John Magufuli aliyeitaka BOT kupunguza wafanyakazi wake wasiokuwa na shughuli muhimu za kufanya kutoka jumla ya wafanyakazi 1,391.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo juzi baada ya kufanya ziara ya ghafla kwenye benki hiyo na kutoa maelekezo kadhaa kwa uongozi wa juu, akiwamo Gavana Prof. Ndulu.

Majina ya watoto hao wa vigogo ambayo yamesambaa kwenye baadhi ya mitandao, yameendelea kuibua maswali mengi kuhusu hatma yao BoT.

Wengi wa wachangiaji wanadai kilichowapatia ajira ni ushawishi wa majina makubwa ya wazazi wao katika medani za uongozi nchini na siyo sifa za kuajiriwa kwenye taasisi hiyo.

Alipoulizwa suala hilo jana, Prof. Ndulu hakutaka kuzungumzia kwa kina, lakini alisema majina hayo siyo mapya na kwamba yalishaandikwa na kujadiliwa mara nyingi hapo kabla.

“Hayo majina kwani kwako wewe ni mapya? Mbona yameshaandikwa na kujadiliwa sana hayo… mimi nasema hakuna jipya hapo,” alisema Prof. Ndulu na kuongeza:

“Hivi ukiwa na jina kubwa halafu ukiwa na akili ama sifa za kufanya kazi fulani, unataka kuniambia usipewe hiyo kazi kwa sababu una jina kubwa?”

Kwa kauli, ni dhahiri tafsiri Prof. Ndulu ana maana kwamba watu hao wenye majina makubwa walipata kazi kwa sifa zao na siyo majina ya wazazi wao kama inavyovumishwa kwenye kurasa za mitandao mbalimbali ya kijamii.

ORODHA YENYEWE
Orodha ya watu wanaodaiwa kuwa ni ya watoto wa vigogo, na ambayo Prof. Ndulu alisema siyo mpya kwani ilishaandikwa na kujadiliwa sana hapo kabla ni pamoja na Pamela Lowasa, anayedaiwa kuwa ni mtoto wa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowasa.

Wegine ni Filbert Sumaye anayedaiwa kuwa ni mtoto wa Waziri Mkuu mstaafu katika serikali ya awamu ya tatu, Fredrick Sumaye na Zaria Kawawa, anayedaiwa ni mtoto wa aliyewahi kuwa Waziri Mkuu katika serikali ya awamu ya kwanza, Marehemu Rashid Mfaume Kawawa.

Mwingine ni Harriet Lumbanga anayedaiwa ni mtoto wa aliyewahi kuwa Katibu Mkuu Kiongozi wakati wa utawala wa serikali ya awamu ya tatu, Marten Lumbanga.

Aidha, orodha hiyo pia ina jina la Salama Ali Hassan Mwinyi anayedaiwa ni mtoto wa aliyekuwa Rais wa awamu ya pili, Alhaji Hassan Mwinyi; Rachel Muganda anayedaiwa ni mtoto wa aliyekuwa Balozi katika serikali ya awamu ya nne, Alexender Muganda.

Salma Omar Mahita, katika orodha hiyo anadaiwa kuwa ni mtoto wa aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi wakati wa utawala wa awamu ya tatu, IGP mstaafu Omar Mahita.

Wengine ni Justina Joseph Mungai anayedaiwa kuwa ni mtoto wa aliyewahi kuwa Waziri wa Elimu na Utamaduni katika serikali ya awamu ya tatu, Joseph Mungai.

Pia yumo Keneth Nchimbi anayehusishwa na kada wa CCM aliyewahi kuwa kigogo wa Jeshi la Polisi John Nchimbi.

Blasia William Mkapa, anadaiwa kuwa ni mtoto wa Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkpa katika orodha hiyo yenyep ia jina la Violet Phillemon Luhanjo, ambaye anadaiwa kuwa mtoto wa aliyewahi kuwa Katibu Mkuu kiongozi wakati wa serikali ya awamu ya tatu na nne, Phillemon Luhanjo.

Liku Kamba anadaiwa kuwa mtoto wa aliyekuwa kada wa CCM wa muda mrefu, Kate Kamba.

Wengine wanaotajwa katika orodha hiyo ni Thomas Mongela anayedaiwa kuwa mtoto wa kada mashuhuri ndani ya CCM; aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali zikiwamo za ubunge, Getrude Mongela.

Jina la Jabir Abdalah Kigoda linadaiwa kuwa ni mtoto wa aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara katika serikali ya awamu ya nne, marehemu Abdalah Kigoda.

KUPUNGUZA WAFANYAKAZI 
Juzi, miongoni mwa maagizo aliyoyatoa Rais Magufuli wakati wa ziara yake ya kushtukiza, ni pamoja na kumtaka Gavana Ndulu kupitia upya orodha ya wafanyakazi wa benki hiyo na kuwaondoa ambao hawana ulazima wa kuwapo.

Rais alielezea kushangazwa kwake na kitendo cha BoT kuwa na wafanyakazi wanaofikia 1,391.

Alipoulizwa kuhusu kupunguza wafanyakazi BoT kama ilivyoagizwa na Rais Magufuli, Prof. Ndulu alisema hayo yatafanyika baada ya vikao vya ndani na kwamba baada ya hapo, Benki Kuu itatolewa taarifa rasmi ya matokeo ya maagizo ya Rais.

Prof. Ndulu alisema si vyema, na wala haamini kuwa ni busara kuzungumzia masuala yanayowahusu wafanyakazi wa BoT kwa vyombo vya habari na badala yake, masuala hayo yatazungumzwa kwenye vikao vya ndani vya menejimenti ya benki hiyo.

“Haya ya kuwaondoa baadhi ya wafanyakazi tutayazungumza kwenye vikao vya ndani kisha tutaandaa na kutoa tamko," alisema Prof. Ndulu.

"Mambo haya si ya kuyazungumza kwenye vyombo vya habari, hata wewe masuala ya wafanyakazi wenu hamyaweki magazetini holela holela tu.

"Nomba niachieni nafasi jamani.”

Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
© Copyright MZALENDO HURU
Back To Top