Mwanafunzi
wa kidato cha sita wa Shule ya Sekondari Thaqaafa ya jijini hapa, Amos
Kitala (26) ameuawa kwa kuchinjwa kwa kipande cha chupa shingoni kwenye
kilabu cha pombe za kienyeji.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Justus Kamugisha alisema tukio hilo lilitokea
Machi 19, mwaka huu saa 10 jioni wakati mwanafunzi huyo akigombana na
watu wawili kwenye kilabu hicho.
Kamugisha
alisema inadaiwa kabla ya kuuawa Kitala alionekana kuwazidi nguvu
wagomvi wake na ndipo walipoamua kuchukua chupa, kuivunja na kumkata
nayo shingoni na kusababisha atokwe damu nyingi.
Kamgisha alisema wanamshikilia Ramadhan Sima (27) na Omary Philipo (35) kwa tuhuma za mauaji hayo.
Wakati
huohuo; kibarua amekufa kwa kudondoka kutoka kwenye lori alilokuwa
akining’inia wakati akidai ujira wa Sh10,000 kwa kupakia kokoto.
Kamugisha
alimtaja kibarua aliyepoteza maisha baada ya kudondoka kwa kile
kilichodaiwa ni kusukumwa na dereva wa lori hilo aina ya Scania kuwa ni
Mashaka Mathias (34), mkazi wa Isamilo.
Dereva huyo, Haji Juma (38) anashikiliwa na polisi kwa mahojiano kuhusiana na kifo cha kibarua huyo.
Katika
tukio jingine; Christopher Starabu (34), amefariki dunia baada ya
kugongwa na gari wakati akivuka barabara katika eneo la Mabatini.
Kwa mujibu wa Kamugisha, dereva wa gari hilo, Rajabu Mika (30, Mkazi wa Bwiru anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za mauaji hayo.
Mwalimu wa Shule ya Msingi Ilula, John Sinega (29), amefariki dunia baada ya kugongwa gari wakati akiendesha pikipiki.
Kamanda
huyo alisema, dereva wa gari hilo, Ismail Jamal (36), anashikiliwa na
polisi kwa tuhuma za kusababisha kifo cha mwalimu huyo.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )