Balozi
wa China nchini Tanzania Dkt. LU Youqing amefanya mazungumzo na Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira Mh. January
Makamba Ofisini kwa Waziri huyo Mtaa wa Luthuli jijini Dar es Salaam.
Katika
mazungumzo yao Balozi wa China amesema kuwa Serikali ya China inaamini
kwamba uchaguzi wa Zanzibar uliofanyika mwishoni wa wiki iliyopita
ulikuwa huru na haki.
Balozi
Youqing amesema kuwa Makamu wa Rais wa China ametuma salamu za pongezi
kwa Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kuchaguliwa kwake na kwa
watu wa Zanzibar kwa kuendesha uchaguzi huo katika misingi ya haki na
uhuru.
“Alikuwepo shuhuda wetu katika kushuhudia uchaguzi huo na alituambia kuwa ulikuwa wa haki na uhuru,” alisema Balozi huyo.
Katika
mazungumzo hayo Balozi Youqing alisema Serikali ya China itaendelea
kutoa misaada na kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwani huo ni wajibu wa
mataifa makubwa kwa nchi zinazoendelea.
Alimhakikishia
Mheshimiwa Makamba kwamba China ina mipango mingi ya ushirikiano na
Tanzania, ikiwemo kwenye sekta ya umeme na itaendelea kutoa ushirikiano
kwa Tanzania, ikiwemo kupitia makampuni ya China, ili kuhakikisha
malengo ya Tanzania kwenye sekta ya umeme yanatimia.
Kwa
upande wake, Mheshimiwa Makamba alimshukuru Balozi Youqing pamoja na
Serikali ya China kwa ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo mbili.
“Ujumbe
na salamu ulizotoa leo umetupa faraja Watanzania. Urafiki baina ya nchi
zetu, na baina ya vyama vyetu vya CCM na CCP, ni wa muda mrefu, ni wa
majira yote, na umejengwa kwenye misingi ya kuheshimiana na hauna budi
kuendelezwa”, alisema Mheshimiwa Makamba.
Pia
Waziri Makamba na Balozi Youqing walikubaliana kutembelea Pemba na
Unguja kwa pamoja mwezi Aprili ili kukagua na kutengeneza miradi ya
maendeleo kati ya China na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Vilevile,
walikubaliana kuhusu kutengeneza mradi mkubwa wa ushirikiano kati ya
Serikali ya Jamhuri ya Muugano wa Tanzania na China kwenye teknolojia
zitakazosaidia kupunguza matumizi ya mkaa, hivyo kuhifadhi mazingira.
Waziri
Makamba pia amemueleza Balozi Youqing kuhusu hitaji na umuhimu wa
ushirikiano katika kuiwezesha Tanzania kumiliki teknolojia ya uzalishaji
wa nishati kwa kutumia taka ngumu zinazozagaa katika miji ya Tanzania
ambapo Balozi Youqing aliahidi kulifuatilia suala hilo.
IMETOLEWA NA:
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI,
OFISI YA MAKAMU WA RAIS.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )