IDADI ya Watanzania wanaosubiri kunyongwa imekuwa ikiongezeka na hadi sasa imefikia 465 kutokana na hukumu ya kifo kutotekelezwa tangu mwaka 1994.
Ripoti iliyotolewa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora katika mafunzo kwa waandishi wa habari mjini Morogoro juzi, imebainisha kuwa hakuna hukumu yoyote ya kifo iliyosainiwa na Rais ili kutekelezwa hadi Oktoba 2015 kulipofanyika Uchaguzi Mkuu ambao Rais Magufuli aliibuka mshindi.
Ripoti hiyo ya Mpango wa Kujitathmini Kuhusu Hali ya Utekelezaji wa Haki za Binadamu (UPR), unaotekelezwa kwa mara ya pili nchini, imeonesha kuwa kuna mahabusu 465 wanaosubiri adhabu ya kifo, kati yao wanaume ni 445 na wanawake ni 20.
Wanaharakati
Akiwasilisha ripoti hiyo, Ofisa Uchunguzi Mkuu wa Tume hiyo, Philemon Mponezya, alisema Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, inaitaka Serikali kufuta adhabu hiyo kwa kuwa haitekelezeki lakini baadhi ya asasi hasa zinazohusika na haki za walemavu wa ngozi, zinapinga kufutwa kwa adhabu hiyo.
Baadhi ya asasi zinazopinga kufutwa kwa hukumu ya kifo ni taasisi ya Under The Same Sun (UTSS), ambayo inasema katika utafiti waliofanya, wahusika wanataka hukumu hiyo hasa inayohusu watu walioua albino, itekelezwe mpaka hapo mauaji hayo yatakapokoma.
Hata hivyo, Mponezya alisema watetezi wengi wa haki za binadamu wanataka adhabu hiyo ifutwe kwa kuwa ni kinyume cha haki za binadamu na kwa Tanzania, imekuwa mbaya zaidi kwa kuwa baadhi ya wahukumiwa wamesubiri zaidi miaka 20 bila hukumu dhidi yao kutekelezwa, jambo linalowaathiri kisaikolojia.
“Tume inasisitiza Serikali iangalie upya hukumu hii na kuiondoa kwa sababu ya utekelezaji wake. Tangu mwaka 1994 hadi leo watu 465 wanasubiri adhabu hiyo, hakuna aliyenyongwa. Kila mlango unapogongwa unahisi ni wewe kumbe la, tunadhani iondolewe maana haitekelezwi,” alisema Mponezya.
Wananchi wagawanyika
Tume hiyo ilikiri kwamba, Tanzania imeshindwa kutekeleza adhabu hiyo kwa miaka mingi kutokana na Serikali kueleza kuwa jamii imegawanyika kuhusu hukumu hiyo.
Wapo wanaotaka ifutwe lakini wengi wanataka iendelee kutekelezwa kutokana na ongezeko la mauaji ya vikongwe kwa imani za kishirikina na albino.
Wakili wa Serikali Mkuu kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mark Mulumbo, alipotakiwa kufafanua kuhusu mtazamo wa kisheria na kiserikali kuhusu utekelezaji wa adhabu hiyo katika mafunzo hayo, alikiri kwamba tafiti zilizofanywa nchini zimeonesha kuwa, kuna mgawanyiko kwa wananchi kuhusu adhabu hiyo.
“Tume kadhaa zilizoundwa kupata maoni ya wananchi, zilitoa matokeo kuwa wananchi wengi bado hawataki adhabu iondolewe, wanataka iendelee kuwapo, sasa Serikali inafanya kazi kwa matakwa ya wananchi, si vinginevyo,” alisema Mulumbo.
Akifafanua zaidi, alisema hata katika mchakato wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, hali hiyo ilijitokeza kwamba Watanzania wengi hawaoni kama muda ni mwafaka kufuta adhabu hiyo.
Marais
Kuhusu marais kushindwa kusaini hukumu hiyo, Mulumbo alisema upo mtazamo wa aina mbili kuhusu jambo hilo; wa kiimani na kisheria.
Alisema pamoja na kwamba nchi haina dini, marais wote waliowahi kuchaguliwa mpaka wa Awamu ya Tano, wana imani za kidini.
“Siwasemei kwamba imani zao ni sababu, lakini huenda ni sababu.Ila kisheria rais hahukumiwi akisaini hukumu hiyo, sasa hilo mimi siwezi kulisemea ila sheria zinaweza kuangaliwa zaidi, ili zimpe rais nafasi ya kumpa mhusika kifungo cha maisha.
“Lakini hapo napo kuna mtazamo mwingine, maana kuna hoja kwamba kwa nini aliyeua na kupatikana na hatia afungwe maisha. Je, iko wapi haki ya aliyeuawa?” Alifafanua Mulumbo kwa mtazamo wake.
Wanaoipenda
Mwanasheria wa UTSS aliyewasilisha mada katika mafunzo hayo, Perpetua Senkoro, ambaye pia ana ulemavu wa ngozi, alisema kwamba, utafiti uliofanywa na taasisi hiyo kwa walemavu wa ngozi (albino) kuhusu hukumu hiyo, umeonesha jamii inataka iendelee kuwapo, na itekelezwe.
Senkoro alisema wana imani sawa na wanaharakati wenzao wa haki za binadamu kuwa dhana ya hukumu ni kumfanya mkosaji abadilike na hukumu ya kifo haitoi nafasi ya kubadilika, lakini kwao kutokana na namna wanavyouliwa kwa imani za kishirikina, hilo si suala la tabia bali ni imani na hivyo muuaji hawezi kubadilika, wanaona heri iendelee kuwapo na itekelezwe.
“Wengi wa jamii yetu wanataka hukumu iendelee kuwapo mpaka hapo mauaji kwa albino yatakapokoma na itekelezwe. Wauaji wa albino wanaua kwa imani si tabia, wanatumwa na watu wenye fedha, kiungo kinauzwa Dola za Marekani 2,000, tena tunaona wanaokamatwa ni vidagaa, bado mapapa hatuyaoni, tunaomba Serikali (ya Magufuli) iwatafute vigogo na tuone hukumu hii ikitekelezwa ili kumaliza imani hizi zinazowanyima haki baadhi yetu ya kuishi,” alisema Senkoro.
Pamoja na Tanzania kuridhia mapendekezo kadha wa kadha ya haki za binadamu, bado Mei 9 hadi 12 mwaka huu, katika mkutano wa Geneva, Uswisi itaulizwa utekelezaji wa mapendekezo mengine na msimamo wa nchi kuhusu kufuta adhabu ya kifo.
Mkutano huo utahudhuriwa na asasi mbalimbali za utetezi wa haki za binadamu nchini, viongozi wa serikali pamoja na tume za haki za binadamu, ambapo nchi zaidi ya 190 zinatarajiwa kushiriki.
Ripoti mpya ya shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, imeonesha kuwa idadi ya watu waliouawa mwaka 2015 katika utekelezaji wa hukumu ya kifo ni kubwa zaidi tangu mwaka 1990.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watu 1,634 waliuawa mwaka jana sawa na asimilia 50 ya waliouawa mwaka 2014. Aidha takwimu hizo hazihusu utekelezaji wa hukumu hiyo nchini China, ambako takwimu za adhabu hiyo huwa siri ingawa zinatajwa kuwa kubwa.
Nchi zinazotajwa kutekeleza zaidi hukumu hiyo mwaka jana ni Iran, Pakistan na Saudi Arabia ambako asilimia 90 adhabu hiyo ilitekelezwa.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )