Kuna sababu kadhaa kwanini wananchi wengi hawajapendezwa na kipindi hicho. Kubwa na muhimu kabisa, ni kuwa mjadala wa ushoga kwenye vyombo vyetu vya habari hasa redio na runinga bado inatia ukakasi mkubwa kwa wasikiliza/watazamaji. Kwa maadili na mila zetu, shoga ni mtu anayetia hata aibu kumuona akipita mtaani, seuze akihojiwa kwenye runinga ya taifa akijieleza kwa madaha anavyotembea na wanaume wenziwe, wa kila aina.
Mijadala ya ushoga kwenye redio na TV za Tanzania ni sawa na mtoto wa kiume kuongelea mapenzi na mama yake mzazi. Inakera masikioni, wanaudhi machoni na kwa kipindi kama kile kinachoruka saa tatu usiku, muda ambao familia nyingi zinakuwa zimekusanyika sebuleni baada ya chakula cha usiku ni aibu kubwa.
Ninaamini kuwa wengi walihamisha stesheni zao kuepuka fedheha ya kumuona mtu huyo akihojiwa kama si kutamani kujificha uvunguni kwa aibu.
Jambo la pili ni ‘timing’ ya kurushwa kwa kipindi hicho. Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa waislamu ni mwezi muhimu mno. Ni mwezi wanaoutumia kurekebisha mienendo yao, kutubu dhambi zao na kuwa karibu zaidi Mungu. Hivyo kwa kurushwa kipindi kama hicho katika mwezi huu, ilikuwa ni sawa na kukiwekea kidonda chumvi.
THE MEANS DOES NOT JUSTIFY THE END!
Dhumuni la Zamaradi kukirusha kipindi hicho lilikuwa zuri na muhimu mno. Hiyo ni tabia inayokera wengi na ongezeko la vitendo hivyo linatisha. Mtangazaji huyo aliandaa kipindi hicho kutaka kujua chimbuko lake. Kwa maelezo yake alidai muda wa kunyamazia tatizo hilo umepita na ni muda wa kulizungumza bila kificho.
Lakini wakati mwingine njia inayotumika haihalalishi nia njema. Ndio maana pamoja na Zamaradi kueleza kwa kina kwanini aliamua kumhoji jamaa huyo, bado watu hawamwelewi kwasababu ukweli ni kwamba muda wa kuiweka mijadala ya aina hiyo kwa Tanzania haujafika.
Bado ushoga ni kitu cha aibu kukisikia kikijadiliwa. Na jambo baya zaidi ni kuwa shoga huyo alipewa muda mwingi wa kujieleza na kuonesha ufahari wake. Kwake yeye, maisha hayo ni sawa na kwa wengi hiyo ndiyo ilikuwa tafsiri ya kipindi hicho – kwamba kiliuza zaidi dhana ya ushoga badala ya kuikemea kwa kumwalika mtu anayejutia kujiingiza kwenye tabia hiyo ili iwe funzo kwa jamii.
Mwanazuoni mmoja wa masuala ya habari ameandika:
Kwanza,nikili wazi kumualika shoga kwenye kipindi,kama tunavyoshuhudia wanaotumia madawa ya kulevya,si kosa, kosa unamualika aje kufanya nini? Unakwenda kumuuliza nini? Unataka peleka ujumbe gani? Kama unamualika kwa nia ya kuhakikisha anaeleza madhara ya anachokifanya,kwa nia ya kuonesha ubaya wa mchezo huu ili jamii ichukue tahadhari,hakuna shida.
Nimebahatika kukiona hicho kipindi kupitia mitandao ya kijamii,na kuona mapungufu yafuatayo.
1. Mtangazaji alimuachia muda mwingi mgeni wake kueleza jinsi anavyofurahia mazingira ya mchezo huo mchafu,alitumia mbinu dhaifu ya kufanya mahojiano (space interview) wakati kwa mazingira yale alitakiwa kutumia mbinu ya ‘shotgun.’ Tunatakiwa kutumia shotgun pale unapokuwa huna imani na mgeni wako, bahati mbaya Zamaradi aliacha kutumia mbinu hii akatumia ‘space interview’ matokeo yake mgeni akatumia mwanya huo kuharibu kipindi na kuharibu nia njema ya mtangazaji ambayo kwa jinsi nilivyomsikia,asubuhi alisema alilenga kuwaelimisha wazazi juu ya umuhimu wa kumnasua mtoto na hatari. Zamaradi alitakiwa kutumia shotgun ili kutompa nafasi ya kuupamba ushoga kama alivyofanya.
2.Nadhani mtangazaji hakutafakari kabla ni aina gani ya mahojiano anakwenda kuyafanya,siku zote aina ya mahojiano ndiyo huamua aina ya maswali na mbinu za kuuliza. Kama Zamaradi alilenga kuandaa kipindi kinachotaka kuhakikisha ushoga unapigwa vita na kutokomezwa, aina hiyo ya mahojiano huitwa CRITIC INTERVIEW. Aina hii ya mahojiano humtaka mtangazaji kuwa critical kwa mgeni wake na mada. Anatakiwa kumbana mgeni kwa kumuonesha ubaya wa anachokifanya.
ZAMARADI BADO NI MTANGAZAJI BORA WA TV
Maisha yana changamoto nyingi sana na wakati mwingine huja kwa kushtukiza kabisa. Leo hii Zamaradi anaandamwa kwa matusi na kejeli kwenye mitandao wa kijamii kwa kuteleza mara moja kwenye kitu ambacho alipanga kwa nia njema.
Wanasema vyombo vya habari ni ‘mbwa mlinzi’ ama watchdog – kwa maana kwamba hutumika pia kulinda masuala muhimu kwenye jamii. Zamaradi alitumia kipindi hicho kama njia moja wapo ya kutafuta suluhisho la janga hilo na jinsi ya kuwanusuru watoto wetu. Bahati mbaya njia aliyotumia imeleta mrejesho hasi, tofauti kabisa na matarajio yake, na tayari madhara yameonekana.
Zamaradi anafahamika kwa uwezo wake mkubwa katika tasnia hiyo na sisi ni mashahidi, kipindi cha Take One ni miongoni mwa vipindi bora kwenye TV. Juzi tu kabla ya hapo alimwalika Sheikh Kipozeo, ambaye licha ya visa vyake, alitoa mawaidha muhimu kwa waislamu katika mwezi huu wa Ramadhan. Tusimlaumu tu Zamaradi kuteleza mara moja, bali pia tumkumbuke na kumtetea kwa mazuri 100 aliyoyafanya.
TCRA ISITOE ADHABU KWA SHINIKIZO LA WANANCHI, BALI KWA KUZINGATIA NIA HALISI YA KIPINDI HICHO
Kupitia akaunti yake ya Twitter, mamlaka ya mawasiliano Tanzania imeandika: TCRA imepokea malalamiko Kuhusu kipindi kilichorushwa na Clouds TV cha Take1. Kamati ya Maudhui inalifanyia kazi na maamuzi yatatolewa.
Nafahamu kuwa mamlaka hiyo imepokea malalamiko mengi sana kuhusu kipindi hicho na naelewa kuwa ‘kutokujua kosa si kinga katika mambo ya sheria’ lakini ningeshauri ipitie shauri hili kwa kuzingatia nia halisi ya kurushwa kipindi hicho na kutohukumu kwa pressure ya wananchi na madhara yaliyotokea.
FUNZO
Sisi tuliopo kwenye tasnia ya habari tutambue kuwa hakuna mada bomu kama ya ushoga, tuiepuke kwa uwezo wetu wote na kama kuna ulazima wa kuiongelea basi tuwe makini sana.
Pole Zamaradi, hayo ndio machangu ya fani hii ya habari.
Imeandikwa na Fred Bundala
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )