Awali, DPP alikuwa na uwezo wa kuzuia dhamana za baadhi ya watuhumiwa kwa namna alivyoona inafaa licha ya kuwepo kwa malalamiko ya uhalali wa kuzia dhamana hizo.
Miongoni mwa sababu ambazo zimekuwa zikitolewa na DPP ni maslahi ya umma hivyo kusababisha haki ya kupata dhamana kuwa ngumu.
Kwa kuwa hatua hiyo inakiuka Katiba ya Tanzania, Mahakama Kuu imefikia uamuzi wa kumwondolea mamlaka hayo DPP.
Kifungu kilichokuwa kikimpa mamlaka DPP ya kuzuia dhamana ni 148 (4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) na kwamba, kinakwenda kinyume na Ibara ya 13 (6) (a) ya Katiba ya Tanzania.
Uchambuzi wa udhaifu wa kifungo hicho kilichokuwa kikitumiwa na DPP ulitolewa na Majaji Sekieti Kihiyo na Dk. John Ruhangisa wakiongozwa na Jaji Kiongozi Shaaban Lila.
“Imeamriwa mtuhumiwa aliye chini ya ulinzi wa polisi au mtuhumiwa yoyote, anatakiwa kupewa haki yake ya kujitetea kabla ya haki hiyo haijazuiliwa na mkurugenzi wa mashitaka kwa pingamizi la kuwanyima dhamana,” sehemu ya taarifa ya majaji hao imeeleza hivyo.
Kifungu cha 148 (4) kinasema; “bila kujali kitu chochote kilichopo kwenye kifungu hiki, hakuna afisa polisi wala mahakama atakayeweza, baada ya mtu kukamatwa na wakati anasubiri shauri au rufaa, atathibitisha kwa maandishi kwamba kuna uwezekano kwa usalama au maslahi ya Jamhuri.
“…na cheti kilichotolewa na Mkurugenzi wa Mashitaka chini ya kifungu hiki kitaanza kutumika kuanzia terehe kitakapowasilishwa mahakamani au kutaarifiwa kwa afisa msimamizi wa kituo cha polisi na kitaendelea kutumika hadi mwenendo utakapohitimishwa ama mkurugenzi wa mashitaka atakapokiondoa.”
Kuondolewa kwa mamlaka ya DPP kuzuia dhamana za watuhumiwa kulitokana na kupelekwa pingamizi la kikatiba lililowasilishwa na Jeremiah Mtosebya, Mkazi wa Jiji la Dar es Salaam ambaye amesema kifungu hicho kinakiuka Katiba ya Tanzania.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )