Na: Frank Shija, MAELEZO
TAKRIBANI
shilingi bilioni 1.5 zimechangwa kufuatia matembezi ya hisani
yaliyopewa jina la “Walk for Kagera” yaliyofanyika leo Jijini Dar es
Salaam kwa lengo la kusaidia wahanga wa Tetemeko la Ardhi lililotokea
tarehe 10 septemba mwaka huu mjini Bukoba Mkoani Kagera.
Akizungumza
mara baada ya matembezi hayo Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Mhe Ally
Hassan Mwinyi aliwashukuru wadau mbalimbali waliojitokeza na kushiriki
matembezi hayo ya hisani.
“Nawapongeza
sana wadau wote mlioshiriki katika matembezi haya, mmeonyesha
mshikamano mkubwa kwa umoja wenu mmeweza kuchangisha jumla ya shilingi
1,502,680,000 hii inatia faraja sana muendelee na moyo huo” Alisema Mzee
Mwinyi.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi amewahakikishia
wananchi wa Mkoa wa Kagera kuwa Serikali inafanya kila liwezekanalo
kuhakikisha wahanga wa tetemeko hilo wanapatiwa huduma stahiki na kwa
wakati.
Balozi
Kijazi aliongeza kuwa kutokana na kuguswa na tatizo hilo Serikali
pamoja na Taasisi zake imetoa msaada wake ambao unakadiriwa kuwa zaidi
ya shilingi bilioni moja ikiwa ni kuthamini utu wa wahanga.
“Najua
kuna athari kubwa imetokea kutokana na tetemeko hili, sisi kama
Serikali tunafanya kila jitihada kuhakikisha wahanga wote wanapata
misaada na kurejesha huduma zote katika hali yake” Alisema Balozi
Kijazi.
Awali
akisoma maelezo ya tathmini ya athari za tetemeko hilo Naibu Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na
Walemavu Mhe. Abdallah Posi amesema kuwa hadi kufikia tarehe 16 idadi
ya vifo ni 17, nyumba zilizoanguka zimefikia 840 huku zilizoharibika
zikiwa ni 1264 na majengo 44 mali ya Taasisi za umma yameharibika.
Kwa
upande wake Kiongozi wa Mabalozi nchi, Balozi wa Zimbabwe ametoa pole
kwa wahanga wa tukio hilo na kuahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania
pale panapo hitaji msaada wao.
Matembezi
hayo ya hisani kwa ajili ya kuchangisha fedha za kusaidia wahanga wa
tetemeko la Ardhi yaliandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki ,Ofisi ya Waziri Mkuu na Ikulu.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )